Mawakili wa Gwajima ( Peter Kibatala ) Waiandikia Barua Polisi Kuhoji Uhalali Wa Nyaraka 10 Zlizoombwa na Vifungu Vya Sheria Vilivyotumika

Mawakili wa Askofu wa kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, wameandika barua kuliomba Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kuandika kimaandishi nyaraka wanazozihitaji azipeleke pamoja na vifungu vya sheria vinavyomtaka awasilishe nyaraka hizo.
 
Barua hiyo iliyosainiwa na Wakili Peter Kibatala iliwasilishwa jana mchana katika jeshi hilo, ikiwa ni siku moja baada ya jeshi hilo kumtaka Askofu Gwajima kuwasilisha nyaraka 10, Aprili 16 mwaka huu watakapoendelea na mahojiano.
 
Gwajima aliitwa kuhojiwa na jeshi hilo mara mbili kutokana na kufunguliwa jalada la malalamiko ya kumkashifu Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
 
Katika barua hiyo, mawakili hao kwa niaba ya mteja wao wanaliomba jeshi la polisi kumwandikia barua rasmi kimaandishi, Gwajima wakiainisha nyaraka wanazozihitaji pamoja na vifungu vya sheria vinavyotumika na jeshi hilo kutaka nyaraka hizo.
 
Mawakili hao wanasema watashukuru kupata hati hiyo ambayo hawaijui jina lakini wanaamini jeshi la polisi litafahamu jina la kisheria la nyaraka husika inayotumika kumtaka Gwajima awasilishe nyaraka wanazozihitaji.
 
Aidha wanasema Askofu Gwajima atakapopata nyaraka anayoihitaji atatimiza wito na kuchukua hatua stahiki za kisheria.

Post a Comment

Previous Post Next Post