Makubaliano kuhusu muundo wa baadaye wa mpango wa nyuklia wa Iran,
yamefikiwa baada ya mazungumzo na mataifa sita makubwa yaliyokuwa
yakifanyika nchini Uswisi.
Mawaziri
wa mambo ya naje wa mataifa sita makubwa duniani pamoja na Iran
wakijadili mpango wa nyuklia wa Iran mjini Lausanne, Uswisi
Kwa mujibu wa mkataba huo, Iran
itapunguza uwezo wake wa kurutubisha madini ya urani huku ikiahidiwa
kuondolewa vikwazo kwa awamu.
Rais Barack Obama amesema ni "uelewano wa kihistoria" uliofikiwa na Iran.
Mataifa makubwa ya dunia na Iran sasa yanalenga kuandika mkataba kabambe ifikapo Juni 30.
Muundo wa mkataba ulitangazwa na Umoja wa Ulaya na Iran baada ya siku nane za majadiliano mjini Lausanne.
Mazungumzo
kati ya mataifa makubwa matano jumlisha moja yaani-Marekani, Uingereza,
Ufaransa, China na Urusi pamoja na Ujerumani- na Iran katika mkutano
uliofanyika mjini Lausanne, uliendelea na kupitiliza muda uliopangwa wa
kufikia tarehe 31 Machi.
Mwandishi wa BBC kutoka mjini Lausanne,
Barbara Plett Usher, anasema baada ya kupitiliza muda uliopangwa na siku
mbili za majadiliano ya kina kati ya Iran na mataifa sita makubwa
duniani wameelezea muundo wao uliofikiwa katika mkutano huo kama
mafanikio makubwa.

Mwanadiplomasia wa ngazi ya juu
wa Umoja wa Ulaya,Federica Mogherini, alisoma taarifa ya pamoja
ikielezea vipengele vikuu, ambavyo ni kupunguza vinu vya uchakataji wa
fito za nyuklia, kubadili zana za kutengenezea nyuklia na ahadi ya
kuondolewa vikwazo vya kimataifa dhidi ya Iran.
Makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano huo si ya maandishi, sio rasmi, bali yanajenga msingi wa kufanyika mazungumzo ya kina.
Lakini waanzilishi wa mazungumzo haya wanasherehekea mafanikio makubwa yaliyofikiwa, ambayo wanasema ni ya kihistoria.
Iran
imekuwa ikikana madai ya mataifa ya magharibi kuwa mpango wake wa
nyuklia unalenga kutengeneza silaha za nyuklia. Iran imeingia katika
mazungumzo haya ili kuona inaondolewa vikwazo.

Katika mahojiano na BBC, waziri
wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry amesema ilifikia hatua
alishawishika kujitoa katika mazungumzo hayo lakini anasema cha msingi
wameweza kupenya vikwazo vilivyojitokeza katika awali.
Rasimu ya
mazungumzo hayo pia imepongezwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban
Ki-moon, ambaye amesema anaamini "yatachangia hali ya amani na utulivu
katika eneo hilo".
Mkuu wa sera ya nje wa Umoja wa Ulaya Federica
Mogherini ametangaza mkataba huo katika mkutano na waandishi wa habari
akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Iran Javad Zarif, akisema hiyo
ni "hatua ya maamuzi" iliyofikiwa.

Urusi imepongeza mkataba huo kuwa ni hatua ya kutambua mpango wa nyuklia wa Iran usio na masharti na ambao ni salama.
Lakini
kiongozi wa Israel, Benjamin Netanyahu amemwaambia Rais Obama kwa njia
ya simu kwamba mkataba huo ambao umejikita katika muundo uliokubaliwa,
unatishia uwepo wa Israel.
Kwa upande wake Rais Obama amemwambia
Bwana Netanyahu kwamba mkataba huo kwa namna yoyote ile unaondoa
wasiwasi kwao kuwa Iran ni kinara wa kufadhili ugaidi na vitisho dhidi
ya Israel.
Mkataba huo pia umekosolewa na wajumbe wa baraza la
Congress la Marekani ambao wanataka wabunge wa Marekani kuwa na haki ya
kupitia kila makubalino ya mwisho yanayofikiwa katika mkataba huo.
Nao wananchi wa Iran wanaoishi nchini Uswisi wameelezea kufurahishwa na mpango huo.

Post a Comment