Mchungaji Christopher Mtikila,
ameiondoa mahakamani kesi ya kupinga serikali kupeleka bungeni Muswada
wa kuanzishwa kwa Mahakama ya Kadhi, baada ya jopo la majaji kumshauri
kufanya hivyo kutokana na taarifa za kuondolewa bungeni.
Kesi hiyo ilifunguliwa na Mtikila dhidi ya Mwanasheria Mkuu, Watendaji wakuu wa serikali akiwamo Warizi Mkuu, Mizengo Pinda.
Hatua
hiyo ilifikiwa jana mbele ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na
Mwenyekiti, Richard Mziray, akisaidiana na Jaji Lawrence Kaduri na Said
Kihio katika Mahakama Kuu Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji
Kaduri alihoji kama kuna haja ya kuendelea na kesi hiyo mahakamani
wakati Ikulu imesema serikali haina mpango wa kuanzisha Mahakama hiyo na
Bunge limeshauondoa muswaada huo.
Alisema
kusikiliza kesi inayozungumzia muswada huo uliondolewa bungeni haina
maana na hata maamuzi yake yatakuwa hayana mashiko kisheria.
“Watanzania
hatujaelimishwa nini kinaanzishwa na kitakuwa na majukumu gani hali
ambayo imetuacha tumechanganyikiwa … kuna mgawanyiko mkubwa mara
maaskofu wanasema hili mara wabunge na wananchi pia wanasema mengine ili
mradi tu kila pande inashindwa kuelewa nini haswa kipo mbele yetu,” alisema Mwenyekiti na kuongeza:
“Tuache
kwanza wananchi wapate elimu ya kutosha ili wajue nini kinajadiliwa na
hata kitapopitishwa wajue kuna faida gani wanapata.”
Akizungumza
na Majaji hao, Mtikila alidai kuwa lengo la kufungua kesi hiyo ni
pamoja na kunyoosha mkondo wa sheria kwa sababu wapo wanaovunja sheria
na kupuuza kazi za Mahakama.
Jopo
hilo lilimshauri Mtikila kwamba kama ana nia ya kuendelea na maombi
mengine yaliyopo kwenye kesi hiyo aiondoe mahakamani na kwenda kuandaa
upya maombi yake yasiyokuwa na kipengele cha Muswada wa Mahakama ya
Kadhi.
Mtikila alikubaliana na ushauri wa jopo hilo liliondoa kesi iliyosajiliwa kwa namba 14, ya mwaka huu.
Mtikila
alisema baada ya kuliondoa shauri hilo mahakamani anatarajia kuandaa
maombi mapya dhidi ya Waziri Mkuu, Pinda na wenzake ili waende waieleze
mahakama kwa nini waliandaa muswada huo.
Post a Comment