Shirika
la Umeme nchini (TANESCO) linatarajia kubadilisha mfumo wa huduma ya
Lipia Umeme Kadri Utumiavyo (Luku) na kuuweka wa kisasa ili kuwaondolea
usumbufu wateja wake.
Imeelezwa
kuwa mfumo unaotumika sasa ni tatizo kutokana na mabadiliko hayo, mfumo
mpya huenda ukaanza kutumika mwezi ujao. Hayo yalisemwa jana na Meneja
Uhusiano wa Tanesco, Adrian Severin.
Alisema
mfumo utakaowekwa, utakuwa wa kisasa na kwamba utawasaidia watumiaji
kupata haraka huduma ya Luku. Alisema mfumo huo ni wa kompyuta, wa
kisasa na wa haraka, utakaotibu kero wanayoipata watumiaji wa huduma ya
Luku.
‘’Mfumo
huo utakuwa una uwezo wa kuhudumia wateja wengi zaidi na kwa haraka
ndani ya sekunde tatu, ikilinganishwa na mfumo wa zamani ambao ulikuwa
unatumia zaidi ya dakika moja au sekunde 30,’’ alisema Severin.
Aliongeza
maandalizi ya mfumo huo, yamekamilika na kwamba watakaokuwa wanatumia
simu za mikononi na mawakala wanaouza Luku, wataendelea kutoa huduma
hiyo.
‘’Mawakala
wa MaxMalipo na simu zote za mikononi kama Tigo, Airtel, Zantel na
Vodacom wataendelea kutoa huduma hiyo, lakini itakuwa kwa haraka na
kwamba hakutakuwa na shida ya mitandao,’’ alisema.
Akizungumzia
suala la kutopatikana kwa huduma ya Luku tangu juzi jioni, Severin
alisema huduma hiyo haikupatikana, kutokana na tatizo la mtandao.
‘’Wakati
mwingine simu za mikononi zinakuwa hazina tatizo la mitandao, lakini
unakuta Tanesco mitandao yao ipo chini, vivyo hivyo na kwamba Tanesco
inakuwa ipo sawa kwa mtandao, lakini simu zinasumbua,’’ alisema Severin.
Alisisitiza
kuwa ili kupatikana haraka kwa huduma ya Luku, inatakiwa Tanesco na
simu zote zinazotoa huduma hiyo kuwa na mitandao iliyo sawa. Hata hivyo,
alisema huduma hiyo inapatikana kwa sasa.
Kwa
muda mrefu, watumiaji wa huduma ya Luku, wamekuwa wakilalamikia uduni
wa huduma, kiasi cha kuwafanya wateja wake kushindwa kuwa na umeme kwa
siku kadhaa, kutokana na tatizo la kimfumo katika mitambo ya huduma za
Luku.
Post a Comment