Mwanza. Kiongozi wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zitto Kabwe
amesema iwapo Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa anataka kugombea
urais kupitia chama hicho afuate taratibu za chama ikiwamo kutangaza
mali zake.
Akiwahutubia mamia ya wakazi wa Jiji la Mwanza
kwenye Viwanja vya Furahisha juzi, Zitto alisema hawezi kumzuia mtu
anayetaka kujiunga ACT - Wazalendo ikiwa atafuata taratibu zilizowekwa
na chama hicho.
“Naomba niwaambie Watanzania kwamba ACT siyo chama
cha kumtengenezea mtu mazingira ili agombee urais, lakini kama Lowassa
anataka kugombea urais kupitia huku lazima atangaze mali zake na kueleza
wapi amezipata kama taratibu za chama zinavyosema,” alisema Zitto na
kuongeza:
Zimekuwapo taarifa kwenye vyombo vya habari na
mitandao ya kijamii kuwa baadhi ya wagombea akiwamo Lowassa ambaye
anatajwa kuwania urais kupitia CCM, wana mpango wa kutimkia ACT iwapo
watakatwa majina yao katika mchujo wa wagombea.
Kwa mujibu wa habari hizo, ACT - Wazalendo imepewa
fedha na Lowassa ambazo inatumia katika mikutano hiyo kumwandalia
nafasi ya kuwania urais, madai ambayo pande zote zimeyakanusha.
Akizungumzia taarifa hizo kwenye mkutano huo,
Zitto alisema chama chake kinaongozwa kwa kufuata taratibu na kitampokea
yeyote atakayefuata taratibu hizo.
Kiongozi huyo ambaye hivi karibuni alitangaza mali
na madeni yake, alisema iwapo Lowassa atataka kujiunga na chama hicho
itambidi atangaze mali zake na kueleza jinsi alivyozipata, kama yeye
(Zitto) alivyofanya.
Hata hivyo, akizungumzia kuhusu kauli ya Zitto,
msemaji wa Lowassa, Aboubakary Liongo alisema: “Hakipo kitu kama hicho
na hakitakuwapo, hatujui habari hii inatoka wapi? Mzee (Lowassa) amekuwa
akitumikia CCM maisha yake yote tangu enzi za TANU … yupo na anaendelea
kutumikia kifungo chake. Maisha yake yote ni mtumishi wa chama.”
Lowassa pamoja na makada wengine watano wa chama
hicho walipewa adhabu ya onyo kali baada ya Kamati Kuu ya CCM kuwatia
hatiani kwa kuanza kampeni za urais mapema na kukiuka maadili ya chama.
Mbali ya Lowassa, wengine waliofungiwa ni Waziri
Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye; Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja;
Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira; Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe; na Naibu Waziri wa
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.
Licha ya muda wa adhabu hiyo kufikia tamati tangu
Februari mwaka huu, chama hicho kilisema kinaendelea kuchunguza mienendo
yao na hakijaeleza hatma yao.
Juzi, gazeti hili liliripoti kuwapo kwa mkakati wa
chama hicho kukata majina ya baadhi ya wagombea wanaoaminika kuwa na
makundi yanayokihatarisha, wakilengwa Lowassa na Membe ili kipitishe
mgombea asiyekuwa na kundi.
Post a Comment