Mkuu wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu (kushoto) akimhoji dereva
wa lori aliyejitambulisha kama Bw. Kabyemela (mwenye tisheti jekundu)
baada ya kuwekewa mtego na kukamatwa na shehena ya ngozi ya magendo
iliyokuwa ikisafirishwa kuelekea nchi jirani. Shehena hiyo ilikamatwa
katika kizuizi cha Kyaka.
Baadhi
ya ngozi ya magendo iliyokamatwa baada ya Mkuu huyo wa Wilaya kuweka
mtego kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama. Shehena hiyo ya
ngozi ya magendo inakisiwa kufika uzito wa takribani tani 10.
Mkuu
wa Wilaya ya Missenyi Mh. Fadhil Nkurlu amekamata shehena kubwa ya
ngozi ya magendo yenye uzito unaokisiwa tani 10 ikisafirishwa kwenda nje
ya nchi bila kibali wala nyaraka zozote za serikali.
Kutokana
na taarifa za ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Missenyi ngozi hiyo ilitokea
Kahama ikiwa inaelekea nchini Uganda na ilikamatwa katika kizuizi cha
Kyaka, wilayani Missenyi.
“Tulipata
taarifa kutoka kwa raia wazalendo tangu jana yake kwamba kuna bidhaa za
magendo ambayo huwa yanapita usiku, ndipo nikawapanga vijana kutoka
vikosi vyote vya ulinzi na usalama kuweka mtego huu,” alisema DC Nkurlu.
“Hiki
ni kipindi ambacho magendo ya kahawa husafirishwa kwa wingi kwenda nje
ya nchi na hivyo hukosesha serikali mapato yake stahiki. Lakini
tumejipanga ipasavyo na tutahakikisha tunakamata kila aina ya magendo.
Hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa yeyote atakayejihusisha katika
biashara hii,” alisisitiza.
“Napenda
kutoa rai kwa wananchi wote wa Missenyi kuendelea kutoa ushirikiano wao
kwa serikali ili kuweza kukamata bidhaa hizi za magendo na kudhibiti
mtandao huu haramu,” alisema Mh. Nkurlu.
Hii
ni mara ya pili ndani ya wiki hii magendo yanakamatwa ambapo Jumatatu
shehena kubwa ya mbao zilikuwa zikisafirishwa kinyemela zilikamatwa na
bado zinashikiliwa katika kituo cha polisi cha Kyaka
Post a Comment