Dar es Salaam. Kitendo cha Chama cha Wananchi
(CUF) kufanya uchaguzi wa Kura za Maoni katika majimbo ya Kawe na Ubungo
yanayoshikiliwa na wabunge wa Chadema, kimeibua hisia tofauti miongoni
mwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).
Mvutano huo unatokana na kinachoelezwa ni
makubaliano ya vyama hivyo kuwa kila kimoja kiandae wagombea wake katika
majimbo yote ambao watashindanishwa katika Ukawa, bila kuhusisha
majimbo ambayo tayari yana shikiliwa na vyama vinavyounda umoja huo.
Mbali na kigezo hicho, mgawanyo wa majimbo
unazingatia matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, idadi ya madiwani kwa
kila chama, matokeo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014, mtandao wa
chama nchini na nguvu ya mgombea iwapo Chadema kitamsimamisha katibu
mkuu wake, Dk Willibrod Slaa kwa mara ya pili.
Juzi, CUF ilifanya uchaguzi wake wa kura za maoni
katika Mkoa wa ya Dar es Salaam ambapo pamoja na majimbo mengine,
iliwapitisha Leila Hussen kukiwakilisha chama hicho katika Jimbo la Kawe
na Mashaka Ngole katika Jimbo la Ubungo.
Mvutano wenyewe
Kutokana na hatua hiyo, vyama vya NCCR-Mageuzi na
NLD vimesema CUF imeanza kwenda kinyume na makubaliano ya Ukawa, ingawa
CUF na Chadema wameeleza kuwa haikuwa kosa kufanya kura ya maoni kwenye
majimbo hayo.
Ingawa viongozi hao wametofautiana kimtazamo
kuhusu hatua hiyo ya CUF, wamesisitiza kuwa kuweka mgombea mmoja wa
upinzani kupitia Ukawa bado ni njia sahihi na pekee itakayowezesha
kuiondoa CCM.
Kauli ya NLD
Mwenyekiti wa NLD, Dk Emmanuel Makaidi alisema
Ukawa haijafikia uamuzi wa kuiachia Chadema majimbo ya Ubungo na Kawe,
lakini CUF imekosea kuwasimamisha wagombea katika majimbo hayo kwa kuwa
vikao vya kuwapata wagombea wa upinzani bado vinaendelea.
“Ukweli ni kwamba hakuna kikao cha Ukawa
kilichopitisha kuyaacha majimbo hayo kwa Chadema, ila CUF wamefanya kosa
moja tu, kutangaza wagombea wake hadharani. Kama ni mchakato wa
maandalizi, walipaswa kuwaanda wagombea hao ndani ya chama chao ili
kusubiri uamuzi wa vikao vya Ukawa,” alisema Dk Makaidi na kuendelea;
“Hata sisi NLD tuna wagombea wetu Dar es Salaam, lakini hatuwezi kuwatangaza kwa sababu tunasubiri vikao vya Ukawa.”
Alipoulizwa kuna tatizo gani kumtangaza mgombea
sasa huku wakiendelea kusubiri vikao vya Ukawa alijibu, “Huku ni
kuwachanganya wananchi. Kama kila chama kitatangaza mgombea wake sasa
halafu Ukawa ikaja na mgombea mmoja, huku ni kuchanganya watu.”
- Mwananchi
- Mwananchi
Post a Comment