Mbowe: Ndoto ya Nyerere kutimia Oktoba

 
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema matamanio ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ya kuwaletea Watanzania mabadiliko waliyoyakosa ndani ya CCM yanaenda kutimia katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Mbowe aliyasema hayo jana katika mkutano wa chama wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Tanganyika Packers, Kawe jijini Dar es Salaam ambako pamoja na mambo mengine alizindua kitabu cha mambo aliyoyafanya mbunge wa jimbo hilo, Halima Mdee na wimbo maalumu wa msanii wa nyimbo za Injili, Flora Mbasha.
Akizungumza katika mkutano huo uliorushwa moja kwa moja na ITV, Mbowe alisema katika maeneo yote ya nchi, watu wamekata tamaa ya maisha kutokana na uongozi mbaya wa chama tawala, hivyo wako tayari kufanya mabadiliko ya mfumo wa utawala.
“Katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu matamanio ya Mwalimu Nyerere yanaenda kutimia. Watanzania wanataka mabadiliko ambayo wameyakosa ndani ya CCM. Nimezunguka nchi nzima na kubaini kuwa wananchi wanazo sababu na uwezo wa kuyaleta mabadiliko kutokana na kiu waliyonayo,” alisema.
Mbowe aliyeanza mkutano huo kwa kukagua gwaride la kikundi cha Red Brigade, alitoa kauli hiyo akimnukuu Mwalimu Nyerere aliyepata kusema kuwa, “Watanzania wanataka mabadiliko. Wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.”
Alitumia fursa hiyo kuzungumzia mchakato wa uandikishaji wapigakura kuwa unahitaji kutazamwa kwa namna nyingine ili kuwatendea haki wananchi ambao wana shauku ya kutimiza haki hiyon ya kikatiba.
“Juzi nilikuwa Mbeya, nimeshuhudia wananchi wakilala katika vituo vya kuandikishia kutokana na hofu waliyonayo kukosa uchaguzi mkuu. Namkumbusha Jaji Lubuva (Damian, mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi) aongeze muda na isiwe siku saba kama ilivyopangwa awali. Kutofanya hivyo atakuwa anajitafutia lawama ambazo hakutakuwa na kiongozi yeyote wa CCM atakayesimama kumtetea pindi wananchi watakapokuwa wanamlaumu hapo baadaye,” alisema.
Mwenyekiti huyo mwenza wa umoja wa Katiba ya wananchi (Ukawa), pia alibainisha mkakati wa umoja huo kugomea na kuipinga rasimu inayotaka vyombo vyote vya habari kujiunga na Shirika la Habari Tanzania (TBC) kwa taarifa ya habari ya saa 2.00 usiku.
“Tutaleta vurugu. Tutasimamisha Bunge kupinga sheria hiyo kwa sababu hiyo ni hujuma ambayo wananchi hawaikubali na mimi kama kiongozi wa upinzani nitalisimamia hilo,” alieleza.
Akimakaribisha Mbowe, Naibu Katibu Mkuu na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika alisema mkutano huo ni muhimu na chama kimeuandaaa ili kuthamini umuhimu wa wanawake katika jamii.
“Mwenyekiti fikiria kama wewe unabeba mimba miezi tisa, ujifungue na kumlea mtoto. Hayo ndiyo wanayoyafanya wanawake hawa. Ni lazima tukubali ujasiri wao kwa kuyajali majukumu yao,” alisema Mnyika.
Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Pwani, Mabere Marando alisema Chadema kimejipanga kuwaleta viongozi wake wote jijini hapa kufanya kampeni ya uandikishaji katika daftari la kudumu ili wapigakura wafike milioni 3.5 na kuiondoa CCM madarakani.

Post a Comment

Previous Post Next Post