Dodoma. Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi
amewataka wabunge kuwa kitu kimoja katika viti dhidi ya ufisadi na
ugaidi na nchi yake itakuwa mstari wa mbele kushirikiana na Tanzania
kupambana na maovu hayo.
Akizungumza wakati akilihutubia Bunge la Jamhuri
ya Muungano jana mjini Dodoma, Rais huyo aliyechaguliwa Januari 15,
alitumia dakika 15 kuzungumzia masuala mbalimbali muhimu, alisisitiza
zaidi kuhusu ufisadi na rushwa.
Kutokana na ujio huo, ratiba za shughuli za Bunge
jana zilisitishwa kwa muda ili kumpa nafasi ya kuhutubia, huku muda wa
mawaziri kuwasilisha bajeti ya Ofisi ya Makamu wa Rais mwaka 2015/16
ukipunguzwa kutoka saa moja, hadi dakika 40 huku hotuba za kamati za
Bunge na kambi ya upinzani zikiwasilishwa kwa dakika 20 badala ya 30.
“Tumekuja kujifunza demokrasia na namna ya
kuendesha shughuli za Bunge katika masuala mbalimbali kama bajeti na
kupinga ufisadi. Sasa hivi tumeweza kushiriki chaguzi za kidemokrasia na
ujumbe wangu hapa unawakilisha makundi ya watu mbalimbali kisiasa,”
alisema.
Aliongeza, “Serikali ya Msumbiji inafanya kazi
pamoja na Bunge katika kupinga ufisadi. Tumeona tuje kujifunza kwa Bunge
la Tanzania.”
Alisema wabunge wapo kwa ajili ya kuwawakilisha
wananchi, hivyo jukumu kubwa walilonalo mbali na siasa, ni kufanya kazi
ya kuendeleza uchumi, elimu, utalii na shughuli nyingine.
Huku akiishukuru Tanzania kwa kusaidia vita ya
ukombozi kusini mwa Afrika na juhudi za ushiriki wake wa kuzuia vita
barani Afrika, Rais Nyusi alisema Serikali yake itaendeleza uhusiano wa
karibu na wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizo mbili.
“Tanzania ni nchi inayoendeshwa kizalendo na
demokrasia, tumekuja kuona jinsi mnavyofanya kazi kwa uzalendo na
mnavyoendesha nchi yenu kidemokrasia,” alisema.
Alisema katika kuimarisha uhusiano uliopo katika
ya nchi mbili hizo, Serikali yake imefungua milango kwa Watanzania
kwenda Msumbiji kufanya biashara.
Akitoa neno la shukrani, Spika wa Bunge, Anne
Makinda alimpongeza Rais Nyusi kwa kuweka historia ya kuwa mkuu wa
kwanza wa nchi hiyo kulihutubia Bunge la Tanzania.
Kabla ya kulihutubia Bunge, Rais Nyusi akiwa na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete alitembelea Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Post a Comment