Ni
siku tatu za hekaheka na kujenga hoja za kujinadi kuanzia kesho wakati
makada wa CCM watakapotangaza kwenye mikutano ya hadhara sababu
zilizowasukumu kuomba kuteuliwa na chama hicho kugombea urais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
CCM ipo kwenye wakati mgumu wa kutafuta mrithi wa Jakaya Kikwete
katika nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe nchini
baada ya Rais huyo wa sasa kuongoza nchi kwa vipindi viwili vya miaka
mitano kila kimoja na hivyo kulazimika kuondoka Ikulu kutokana na utashi
wa kikatiba.
Kutokana na hilo, zaidi ya makada 20 wanatajwa kuwa na nia ya kuomba
ridhaa ya CCM kugombea urais ili kuongoza Serikali ya Awamu ya Tano na
watatakiwa kutangaza, kuchukua fomu na kuzirudisha ndani ya takribani
siku 32 kabla ya Julai 2 ambayo ni siku ya mwisho iliyowekwa na chama
hicho.
Wakati makada hao wa CCM wakijipanga kufanya shughuli kubwa za
kutangaza nia ya kuomba wanachama wao wawape ridhaa ya kugombea urais,
baadhi ya vyama vya upinzani vimeshatangaza ratiba zao lakini
kinyang’anyiro kikubwa kitakuwa wakati vyama vilivyo chini ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa) vitakapofanya mchujo wa kumpata mgombea
atakayewakilisha umoja huo.
Kwa mujibu wa ratiba za makada wa CCM, kesho Waziri Mkuu wa zamani,
Edward Lowassa atafanya mkutano wa hadhara kwenye Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid mjini Arusha kutangaza rasmi nia ya kuomba kuteuliwa na CCM
kugombea nafasi hiyo ya juu nchini.
Timu ya Lowassa, ambaye aliwaambia wahariri wa vyombo vya habari
mwanzoni mwa wiki kuwa atatangaza nia Mei 30, imekuwa ikitoa matangazo
mbalimbali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kutaarifu
tukio hilo la kuanza rasmi kwa safari aliyoiita “ya matumaini”.
Katika mkutano wake na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari
mapema wiki hii, Lowassa alihifadhi majibu ya baadhi ya maswali, akisema
ni sehemu ya masuala atakayozungumzia kwenye hotuba yake ya kutangaza
dhamira yake ya kuomba urais.
Tukio hilo litakalofanyika kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini
Arusha litarushwa moja kwa moja na vyombo vinane vya habari kwa muda wa
saa nne kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 11:00 jioni.
Habari ambazo Mwananchi imezipata kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza
kuwa kumekuwa na maandalizi ya hali ya juu jijini Arusha kuelekea siku
ya tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasili kwa watu mbalimbali
wanaomuunga mkono wakiwamo wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM.
Lowassa, ambaye ni mbunge wa Monduli, alikuwa waziri mkuu wa kwanza
wa Serikali ya Awamu ya Nne, lakini akalazimika kujiuzulu mwaka 2008
baada ya Kamati ya Bunge kuibua kashfa ya kuingia mkataba wa ufuaji
umeme wa dharura na kampuni iliyokuwa haina sifa ya Richmond RDC, uamuzi
ambao anasema aliufanya ili kuiokoa nchi.
Lowassa pia aliwahi kuwania urais mwaka 1995, lakini CCM ikampa nafasi Benjamin Mkapa kuongoza Serikali ya Awamu ya Tatu.
Wakati Lowassa na timu yake wakiwa katika mikakati hiyo, makada
wengine wa CCM ambao nao wanawania nafasi ya kuteuliwa na chama hicho,
pia wamejipanga kutangaza nia zao kila mmoja kwa wakati wake huku wanne
kati ya hao wakitoa taarifa kutangaza nia katika siku mbili tofauti
Jumapili na Jumatatu katika maeneo tofauti.Kusoma zaidi bofya
Makada hao ni mbunge wa Afrika Mashariki, Makongoro Nyerere na Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya
watakaotangaza Juni Mosi (Jumatatu) kila mmoja katika eneo lake.
Taarifa iliyotolea na Makongoro inaeleza kuwa mtoto huyo wa Baba wa
Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, atatangaza nia yake akiwa kijijini
kwao Butiama mkoani Mara.
Makongoro, mbunge wa Afrika Mashariki na ambaye aliwahi kuongoza
Jimbo la Arusha Mjini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi wakati wa uchaguzi mkuu
wa kwanza tangu siasa za vyama vingi zirejeshwe, alidokeza nia yake
mapema juma hili baada ya siku kadhaa za ubashiri kuwa anaandaliwa na
CCM kumrithi JK kutokana na hali ya kambi za urais kutishia mustakabali
wa chama hicho.
Kada mwingine ni Profesa Mwandosya, mbunge wa Rungwe Mashariki (CCM)
ambaye ameeleza kuwa atatangaza nia yake Juni Mosi akiwa mkoani Mbeya na
siku mbili baadaye atachukua fomu.
Mwandosya, ambaye amekuwa mbunge wa Rungwe kwa vipindi vitatu,
aligombea nafasi hiyo mwaka 2005 na kushika nafasi ya tatu akiwa nyuma
ya Kikwete na Dk Salim Ahmed Salim.
Wengine wawili ambao nao watatangaza nia siku moja katika maeneo
tofauti ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira na
Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba.
Wasira, ambaye ni mbunge wa Bunda, ameeleza katika ukurasa wake wa
Facebook kuwa atatangaza nia yake akiwa mkoani Mwanza keshokutwa (Mei
31) huku Mwigulu akitangazia nia yake mkoani Dodoma siku hiyohiyo.
Wasira, mbunge wa Bunda na mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, amekuwa
mbunge na waziri kuanzia mwaka 1970 na ndiye mwanasiasa mkongwe kuliko
wote wanaotajwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Nchemba, ambaye ni mbunge wa Iramba
Mashariki, alitangaza kujivua nafasi yake ya naibu katibu mkuu wa
CCM-Bara ili ajikite zaidi kwenye harakati za kuwania urais.
Naibu waziri huyo wa fedha anatumikia kipindi chake cha kwanza bungeni.
Wakati makada hao wakijipanga kuwaeleza wananchi sababu
zilizowasukuma kuomba kushika nafasi hiyo ya juu kisiasa nchini, makada
wengine wa CCM bado hawajatangaza ratiba zao, huku baadhi wakiwa
wameshatangaza nia na kwa sasa wanasubiri kuchukua fomu na baadaye
kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini.
Waziri Mkuu Mizengo Pinda, pamoja na waziri mkuu wa zamani, Frederick
Sumaye, na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe ni miongoni mwa makada ambao hawajaweka bayana ratiba zao, ingawa
Membe ameweka bayana kuwa atafanya hivyo kijijini kwake Rondo mkoani
Lindi.
Wengine ni mbunge wa Sengerema (CCM), William Ngeleja, Mbunge wa
Songea(CCM), Dk Emannuel Nchimbi, Waziri Mkuu wa zamani, Frederick
Sumaye na Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli.
Ambao tayari walishatangaza nia zao za kuomba kuteuliwa na CCM ni
Pinda, Lazaro Nyalandu, ambaye ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Januari
Makamba (Sayansi na Teknolojia), na Dk Hamisi Kingwangalla (mbunge wa
Nzega).
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Post a Comment