Wakati wakandarasi
walipokuwa wanajenga daraja hili katika eneo la Miangalua kwenye
barabara ya Tunduma-Sumbawanga mwaka 2011. Barabara hiyo sasa
imekamilika.
Barabara ya Mwanza-Musoma iko katika hali nzuri.
Ujenzi wa barabara ukiendelea katika baadhi ya miradi nchini.
Ujenzi wa barabara ya
Iringa-Dodoma umekamilika kwa asilimia 95, bado maeneo machache tu
likiwemo hili la Mlima Nyang’oro ambapo Wachina wameuchonga ili
kupunguza kona katika umbali wa kilometa 15. (Picha zote na Daniel Mbega
wa www.brotherdanny.com).
Na Daniel Mbega, brotherdannyblog
NAJIWEKA
vyema kwenye kiti na kutazama nje kupitia dirishani. Japokuwa giza
limetanda majira haya ya saa 4:30 usiku, lakini ninaweza kuhisi jinsi
basi hili nililopanda la kampuni ya Majinjah linavyotafuna lami.
Abiria
mwenzangu wa jirani ananiambai tutaingia saa sita kasoro usiku mjini
Sumbawanga mjini. Nafarijika japo uchovu ni mwingi, maana kuketi kwenye
basi kwa saa takriban 15 siyo mchezo ingawa tulipata nafasi mara kadhaa
za kupumzika ‘kuchimba dawa’ na kupata mlo.
“Barabara
yote ni lami tupu ndugu yangu, kasoro tu ni haya matuta kutoka Tunduma
hadi Sumbawanga, lakini yamesaidia kupunguza mwendokasi,” ananieleza.
Tunduma
tumeondoka kama saa tatu hivi kuzikabili kilometa 222 hadi Sumbawanga,
lakini safari hii ya kutoka Dar es Salaam inayokadiriwa kuwa na umbali
wa kilometa 1,000 imekuwa siyo ndefu licha ya uchovu wa kiuno na mgongo
kutokana na kuketi tangu saa 12 alfajiri.
Faraja
pekee ni kwamba ninatumia siku moja tu kufika Sumbawanga, tofauti na
miaka mitano iliyopita ambapo nililazimika kutumia siku mbili huku
nikiingia gharama za ziada za kulala Lodge pale Mbeya kutokana na
kutokuwepo na usafiri wa uhakika kutokana na ubovu wa barabara.
Wakati
huo, ukilala Mbeya unalazimika tena kuamka mapema kuwahi basi ambalo
licha ya kuondoka saa 12 alfajiri, bado litafika Sumbawanga saa 8
mchana.
Jirani
yangu ananiambia kwamba sasa unaweza kwenda na kurudi Sumbawanga mara
mbili ukitokea Mbeya kwani mabasi ni mengi na njia ‘inateleza’.
“Wametukomboa sana, magari hayajazi kama zamani, unasafiri kwa raha na kwa wakati – muda wowote unaotaka,” ananieleza.
Ndiyo.
Nakumbuka safari moja wakati nikitokea Sumbawanga jinsi basi
lilivyokuwa limejaza abiria mpaka sehemu ya kupita ikakosekana.
Walioketi walikuwa wachache kuliko waliosimama, sasa piga hesabu
lilikuwa na abiria wangapi! Hata kondatka mwenyewe alilazimika kupita
kwa kuinama juu ya siti ili kwenda nyuma kuwapanga abiria waliosimama na
kuchukua nauli. Ilikuwa ni hatari.
Lakini
leo barabara hii imetandikwa lami na imekuwa sehemu ya barabara zenye
urefu wa jumla ya kilometa 6,276 ambazo zimetengenezwa na utawala huu wa
Awamu ya Nne, huku sehemu kubwa yabarabara hizo ikiwa imesimamiwa na
Dk. John Pombe Joseph Magufuli kama Waziri wa Miundombinu.
Nimezunguka
karibu nchi nzima nikifanya habari za uchunguzi kwa miaka kumi
iliyopita. Mazingira ya wakati ule na ya sasa ni tofauti kabisa, maeneo
ambayo yalikuwa hayafikiki, hivi sasa hali ni nzuri.
Tangu
Januari hadi Juni 2015 pekee nimezunguka karibu kilometa 20,000 hapa
nchini. Nimezunguka nikitokea Iringa kwenda Arusha kupitia
Dodoma-Singida hadi Manyara; nimezunguka kutoka Dar es
Salaam-Kiteto-Kondoa hadi Babati; nimepita Babati-Kondoa-Mayamaya hadi
Dodoma; nimepita Mwanza-Shinyanga-Tabora-Mpanda hadi Sumbawanga mpaka
Mbeya; nimetoka Dar es Salaam-Njombe-Songea hadi Mbambabay; nimetoka
Mwanza-Musoma hadi Sirari; nimezunguka Mwanza-Sengerema-Geita hadi
Bukoba; nimetoka Bukoba kupita Kahama hadi Dar es Salaam; nimetoka
Shinyanga-Maswa-Bariadi hadi Lamadi; na maeneo mengine mengi kwa miezi
sita.
Hakika
nilichokiona kinastahili kupongezwa kwamba kimefanyika. Ingawa barabara
kadhaa zimesimama kutokana na kukosekana kwa fedha kufuatia msukosuko
wa wafadhili kushindwa kutoa fungu, lakini nyingi kati ya hizo
zimekamilika na kuiunganisha vyema Tanzania.
Nilipita
wakati fulani ilipoanza kutengenezwa barabara hii, nadhani ilikuwa
mwaka 2011 nikiwa katika harakati zangu za kuandika habari za maendeleo
vijijini. Barabara hii ilimegwa katika vipande vitatu ili kuharakisha
ujenzi wake na kuzingatia ubora.
Kipande
cha kwanza kilikuwa kutoka Tunduma hadi Ikana chenye urefu wa kilometa
63.2 ambacho kilijengwa na kampuni ya Consolidated Contractors Group kwa
gharama ya Dola 82.521 milioni; Kipande cha pili chenye urefu wa
kilometa 64.2 kilikuwa kutoka Ikana hadi Laela na kilijengwa na kampuni
ya China Newera (64.2km Ikana-Laela) kwa Dola 46.812 milioni; na kipande
cha mwisho kilikuwa kutoka Laela hadi Sumbawanga chenye urefu wa
kilometa 95.31 ambacho kilijengwa na kampuni ya Aarsleff-Interbeton J.V
kwa gharama ya Dola 130.038 milioni. Kwa hiyo kilometa zote 222.71
ziligharimu jumla ya Dola 259.371 milioni ambazo ni fedha za wahisani na
fedha za ndani.
Ni
fedha nyingi sana lakini haziwezikuzidi thamani halisiya barabara hii
ambayo licha ya kuwakomboa wananchi wa pembezoni hasa katika mikoa ya
Mbeya, Rukwa na Katavi, lakini pia itasaidia kuiunganisha Tanzania na
nchi jirani ya Jamhuri ya
Kidemokrasia
ya Congo kwa sababu ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 112
kutoka Sumbawanga-Matai hadi bandari ya Kasanga katika Ziwa Tanganyika
unaendelea chini ya kampuni ya China Railway 15th Bureau Group
Corporation – CR15G kwa gharama ya Dola 80.912 milioni.
Dk.
Magufuli, ambaye sasa ni mgombea urais kupitia Chama cha Mapinduzi
(CCM), anazifahamu karibu barabara zote nchini na hatua zilikofikia.
Alipoingia kwa mara ya kwanza bungeni mwaka 1995 baada ya kushinda
katika jimbo la Chato akiwa na miaka 36 tu, Rais Benjamin Mkapa
akamteua kuwa Naibu Waziri katika Wizara ya Miundombinu. Kazi ya Ubunge
na unaibu waziri ilimpeleka salama hadi mwaka 2000.
Uchaguzi
wa mwaka 2000 ulipoitishwa, Dk. Magufuli aligombea na kushinda kwa mara
ya pili. Rais Mkapa akamteua kuwa Waziri wa Wizara ya Miundombinu,
wadhifa aliodumua nao hadi kipindi cha uongozi wa Mkapa kilipomalizika.
Mwaka
2005 alishinda ubunge kwa mara ya tatu, lakini safari hii aliingia
katika orodha ya wabunge waliopita bila kupingwa. Rais Jakaya Kikwete
akamteua kuongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi
mwaka 2008 alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza
hadi mwaka 2010.
Mwaka
2010 akagombea tena ubunge, lakini safarihii akapambana na mgombea wa
Chadema, Rukumbuza Vedastus Albogast ambaye alitoa upinzani mkubwa
ingawa hatimaye Magufuli alishinda kwa asilimia 66.39 dhidi ya asilimia
26.55 za mpinzani wake.
Rais Kikwete akamrudisha katika Wizara ya Ujenzi ambako yuko hadi hivi sasa.
Tangu
kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, wengi walikuwa wakimtaja Magufuli
kwamba anafaa kuwania urais, lakini yeye alikaririwa akisema wakati huo
kwamba hana mpango huo.
Hata
makada wenzake walipoanza kuonyesha nia kwa ajili ya uchaguzi wa mwaka
huu, yeye hakuwa na papara na iliwashangaza wengi Mei 29 alipoamua
kujitosa kimya kimya, akachukua fomu na kuondoka, bila mbwembwe wala
madoido kama walivyofanya wengine.
Wanaomfahamu
wanasema nguvu yake kubwa iko kwenye elimu yake, lakini kukaa muda
mrefu kwenye wizara zake na mambo makubwa aliyoyafanya katika wizara
alizopata kuziongoza, pamoja na uwezo wake wa kutoa maamuzi magumu kila
mara vinampa sifa ya kuwa rais anayefaa katika kipindi hiki ambacho
rushwa, ufisadi na ukosefu wa maadili vimetamalaki.
Udhaifu
wake pekee unaotajwa na walio karibu yake ni kufanya maamuzi ya haraka,
jambo ambalo linaweza kurekebishwa kwa kuwa ndani ya Taasisi ya Urais
kuna washauri makini.
UJENZI WA BARABARA
Katika
kipindi cha uongozi wa Serikali ya awamu ya nne, barabara zenye urefu
wa jumla ya 6,276.82km zimejengwa kwa gharama ya Dola 102,654.98
milioni, nyingi kati ya hizo zikiwa za lami na hivyo kuutengeneza
mtandao imara wa miundombinu ya barabara.
Kujengwa
kwa barabara hizo kumerahisisha hata usafiri ambapo leo hii magari ya
abiria na mizigo kutoka Dar es Salaam kwenda Musoma, Mwanza, Kagera na
Kigoma hayahitaji kuzunguka Nairobi bali yanakwenda moja kwa moja.
Hivi
sasa usafiri wa kutoka Dar es Salaam kwenda Sumbawanga ni wa siku moja
badala ya siku mbili, kama ilivyo kwa usafiri wa Dar es Salaam kwenda
Mbinga, jambo ambalo miaka 10 iliyopita lilikuwa ndoto.
Asilimia
90 ya miradi hiyo imesimamiwa na Dk. Magufuli akiwa Waziri wa
Miundombinu katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2015na bado miradi
mingine inaendelea kujengwa japo imesimama kidogo kutokana na ufinyu wa
bajeti.
Kampuni
za Kichina zimepata mikataba mingi ya ujenzi. Kwa mujibu wa taarifa
kutoka Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), katika kipindi cha miaka 10
iliyopita, kampuni 14 kutoka China zimeingia jumla ya mikataba 58 ya
ujenzi wa kilometa 3,140.85 yenye thamani ya Dola 1.75 bilioni.
Kampuni
ya China Henan International Cooperation Group Co., Ltd. (CHICO) ambayo
ilipata mkataba wenye thamani ya Dola 206 milioni kutoka Wakala wa
Barabara Zambia kujenga barabara ya Mansa-Luwingu yenye urefu wa
kilometa 175, peke yake imeingia mikataba 13 nchini Tanzania ya barabara
zenye urefu wa kilometa 705.2 zikiwa na thamani ya Dola 490.26 milioni.
Hizi
ni pamoja na barabara za Singida-Iguguno (76km) yenye thamani ya Dola
20.55 milioni; Sekenke-Shelui (33km) yenye thamani ya Dola 12.51
milioni; Mwandiga-Manyovu (60km) wenye thamani ya Dola 32.54 milioni;
Kigoma-Kidahwe (35.7km) kwa Dola 19.56 milioni; Bonga-Babati (19.20km)
kwa Dola 11.95 milioni; Tabora-Urambo (42km) kwa Dola 31.17 milioni;
Kyaka-Bugene (59.1km) kwa Dola 51.6 milioni; Dareda-Minjingu (84.6km)
kwa Dola 51.6 milioni); Kidahwe-Uvinza-Ilunde (76.6km) kwa Dola 47.5
milioni; Isaka-Ushirombo (132km) kwa Dola 88.223 milioni; Kilwa Road
Phase III (1.5km) kwa Dola 3.4 milioni; Nyanguse-Musoma (85.5km) kwa
Dola 3.3 milioni; na Kagoma-Lusahunga (154km ) kwa ubia na kampuni ya
CRSG kwa gharama ya Dola 116.2 milioni.
China
Sichuan International Cooperation Co., Ltd (SIETCO) inajenga barabara
zenye urefu wa 283.9km zenye thamani ya Dola 123.03 milioni ambazo ni
Isuna-Singida (63km) kwa Dola 18.5 milioni; Tarakea-Rongai-Kamwanga
(32km) kwa Dola 8.8 milioni; Iringa-Migori (95.1km) kwa Dola 51.123
milioni; na Migori-Fufu Escarpment (93.8km) kwa Dola 44.7 milioni,
wakati kampuni ya CICO inajenga barabara ya Nangurukuru-Mbwemkuru yenye
95km kwa thamani ya Dola 23.82 milioni.
Kampuni
ya China Geo-Engineering Corporation International Ltd (CGC INT’L)
inajenga barabara zenye urefu wa 525.9km zikiwa na thamani ya Dola 151.2
milioni. Barabara hizo ni Shelui-Nzega (112km) kwa
Dola
12.6 milioni; Kyamorwa-Buzirayombo (120km) kwa Dola 29.822 milioni;
Manyoni-Isuna (54km) kwa Dola 18.4 milioni; Arusha-Namanga (104.2km) kwa
Dola 49.64 milioni; Chalinze-Tanga Phase I (125km ) kwa Dola 25.9
milioni na ndiyo kampuni iliyojenga Daraja la Mkapa (Daraja la Umoja
10.7km) linalounganisha Tanzania na Msumbiji kwa gharama ya Dola 14.9
milioni.
Katika
orodha hiyo, ipo kampuni inayomilikiwa na serikali ya China, Hydropower
Engineering and Construction Company (SINOHYDRO) ambayo ilipata
mikataba 12 nchini Tanzania ya ujenzi wa barabara zenye urefu wa jumla
ya 779.95km zenye thamani ya Dola 434.36 milioni.
Barabara
hizo ni Sengerema-Usagara (40km) kwa gharama ya Dola 21.724 milioni;
Buzirayombo-Geita (100km) kwa Dola 25 milioni; Geita-Sengerema (50km)
kwa Dola 24.034 milioni; Dodoma-Mayamaya (43.65km) kwa Dola 25 milioni;
Manyoni-Itigi-Chaya (89.3km) kwa Dola 66.56 milioni; Puge-Tabora
(56.1km) kwa Dola 35.085 milioni; Handeni-Mkata (54km) kwa Dola 34.81
milioni; Korogwe-Handeni (65km) kwa Dola 38.4 milioni; Katesh-Dareda
(73.8km) kwa Dola 38.94 milioni; Singida-Katesh (65.1km) kwa Dola 31.34
milioni; Tanga-Horohoro (65km) kwa Dola 42.43 milioni; na Peramiho
Junction-Mbinga (78km) kwa Dola 48.444 milioni.
CHIKO
ilijenga barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es Salaam yenye urefu wa 4km
kwa thamani ya Dola 7.9 milioni, China Civil Engineering Construction
Corporation (CCECC) ilipata mikataba minne ya kujenga barabara zenye
urefu wa 145.6km kwa thamani ya Dola 95 milioni.
Barabara
hizo ni Magole-Turiani (48.6km) kwa Dola 25.43 milioni; Tabora-Urambo
(52km) kwa Dola 36.3 milioni; Dumila-Rudewa (45km) kwa Dola 25.5 milioni
na Jangwani Depot kwa ajili ya mradi wa mabasi yaendayo kasi Dar es
Salaam (BRT) kwa Dola 7.81 milioni
Post a Comment