Chama
cha Mapinduzi
kinapenda kutoa taarifa kuhusu masuala kadhaa.
Mwenendo
wa Kampeni
Kwa kifupi, Mgombea
Urais, Ndugu John Pombe Magufuli na Mgombea-Mwenza Ndugu Samia Suluhu Hassan,
wanaendelea vizuri na kampeni. Kila mmoja anafanya mikutano na wananchi kati ya
8 hadi 11 kwa siku na kukutana na maelfu kwa maelfu ya wananchi. Tunawashukuru
wananchi wanaokuja kwenye mikutano yetu. Tunawashukuru pia makada wa CCM
wanaojitolea kwa hali na mali kukipigania Chama cha Mapinduzi na kumtafutia
kura Ndugu Magufuli.
Tunaridhika sana na
mwenendo wa kampeni yetu. Katika nusu hii ya pili ya kampeni tutaongeza kasi na
msukumo wa kuwafikia wananchi wengi zaidi kwa mbinu na mikakati mipya.
Midahalo
ya Wagombea
Tumeshangazwa na
kauli ya Ndugu Kajubi Mukajanga, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania
kwamba CCM haijathibitisha kushiriki mdahalo. CCM ilipokea mwaliko wa MCT na
kuijibu kwa barua ya tarehe 13 Septemba 2015 yenye kumbukumbu CMM/OND/M/190/132
iliyosainiwa na Ndugu Stephen Msami, Msaidizi wa Katibu Mkuu. Barua hiyo
ilipelekwa na kupokelewa kwa dispatch ambayo nakala yake tunayo. Baada ya hapo,
Katibu Mkuu wa CCM, Ndugu Abdulrahman Kinana, alifanya kikao na wawakilishi wa
MCT katika Ofisi Ndogo ya CCM Lumumba ili kutaka kujua zaidi na kutoa maoni ya
CCM kuhusu utaratibu mzima wa mdahalo. Katika kikao hicho, ambapo MCT iliwakilishwa
na Afisa wake, Ndugu Allan Lawa, pamoja na Ndugu Tido Mhando, CCM ilithibitisha
tena kushiriki mdahalo. Tatu, tarehe 16 Septemba 2015, CCM ilitoa kauli rasmi,
iliyosainiwa, ikithibitisha kushiriki mdahalo. Kauli ya Ndugu Mukajanga
inalenga kuwasaidia kisiasa wale ambao hawajathibitisha au hawana nia ya
kuthibitisha kushiriki. Kwa msingi huu, tunaamini ni vyema mdahalo huu
ukaandaliwa na ushirika wa taasisi mbalimbali zilizokuwa na nia ya kuandaa
midahalo, (kama vile CEO Roundtable, UDASA, Twaweza) ili kuiondolea uwezo
taasisi moja, au kikundi cha watu wachache, kuhodhi na kuwa na ukiritimba
kwenye jambo hili kubwa na muhimu.
CCM
inapenda kusisitiza yafuatayo:
1. Ndugu Magufuli
amekubali kushiriki mdahalo wa wagombea Urais
2. Mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na sio wawakilishi wao.
3. Wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki.
2. Mdahalo uwashirikishe wagombea wenyewe na sio wawakilishi wao.
3. Wagombea wote, hasa wa vyama vikuu, wawepo na washiriki.
Tunapozungumzia
mabadiliko katika nchi maana yake ni utayari wa kufanya mambo mapya yenye tija
ambayo hayajawahi kufanyika, ikiwemo mdahalo wa wagombea Urais. Wanaohubiri
mabadiliko huku wakiogopa kushiriki mdahalo wanahubiri mabadiliko hewa.
Utafiti
wa TWAWEZA
CCM haikushangazwa na
matokeo ya utafiti wa taasisi huru ya Twaweza yaliyotangazwa jana ambayo
yanatoa ushindi wa asilimia 65 kwa Ndugu John Pombe Magufuli dhidi ya asilimia
25 za Mgombea wa UKAWA. Hatukushangazwa na matokeo ya utafiti huu kwasababu
tano:
1. Siku UKAWA
walipomteua Ndugu Edward Lowassa kuwa mgombea wao ndio siku CCM
ilipohakikishiwa ushindi katika uchaguzi wa mwaka huu. CCM hatukumteua kwasababu
tuliamini hakuna namna ambapo Watanzania wengi watamchagua.
2. Katika uchaguzi wa
mwaka huu CCM tunafanya utafiti wetu wa ndani wa kisanyansi kila wiki kujua
mwenendo na mwelekeo wa kampeni na maeneo yanayohitaji nguvu mahsusi. Tangu
tuanze utafiti wetu mwishoni mwa mwezi Agosti, karibu kila wiki asilimia za
ushindi wa CCM hazijawahi kushuka chini ya asilimia 60 na zimekuwa zinapanda.
3. Kazi kubwa
anayofanya mgombea wetu, Ndugu John Pombe Magufuli, na mgombea-mwenza, Ndugu
Samia Suluhu Hassan, kuzunguka nchi nzima kwa barabara na kuongea moja kwa moja
na wapiga kura inazaa matunda. Wanawafikia wapiga kura wengi, hasa wa vijijini,
na wapiga kura hao wanawaelewa.
4. Kampeni kubwa
zinazofanywa na wagombea Ubunge na Udiwani wa CCM na makada na viongozi wa Chama
katika ngazi zote nchi nzima kila siku kumuombea kura Magufuli nazo zinazaa
matunda.
5. Tunaamini pia
migogoro ndani ya UKAWA katika kipindi hiki cha uchaguzi iliyopelekea
mitafaruku katika kuachiana majimbo na, baadaye, kutokana na uteuzi wa Mgombea
Urais wa UKAWA, kupelekea kujiuzulu kwa viongozi wa muda mrefu na maarufu wa
UKAWA, Profesa Ibrahim Lipumba na Dr. Wilbrod Slaa, na migongano ndani ya
NCCR-Mageuzi, yote haya yamepunguza imani ya wananchi kuhusu uwezo wa vyama
hivi kushika dola.
Lakini vilevile
matokeo ya utafiti huu ni ishara kwamba Watanzania wamempokea na kumuelewa
Ndugu Magufuli na wako tayari kumkabidhi nchi.
Sisi kama CCM kuna
baadhi ya mambo tumeyachukua katika utafiti huu na tutayafanyia kazi ili
kujihakikishia ushindi.
Tumeshangazwa na
taharuki, hasa kutoka miongoni mwa wasomi na wanaharakati, kuhusu matokeo ya
utafiti huu. CCM ilitegemea kwamba jamii ya wasomi na wanaharakati ingefurahia
utamaduni wa tafiti za kisiasa unaoanza kujitokeza hapa nchini ili siku zijazo
tujikite katika kurekebishana kwenye kanuni za utafiti na ithibati na uhakiki
wa ubora. Tunasikitika kwamba yanawekwa mazingira ya kutisha na kukatisha tamaa
(atmosphere of intimidation) kwa watu wanaotaka kufanya tafiti za kisiasa
nchini.
Utafiti ni sayansi.
Matokeo ya utafiti hupingwa kwa matokeo ya utafiti mwingine, sio kwa kuponda tu
au kwa matusi na vitisho. Ni vyema tukajifunza kupokea habari mbaya bila
taharuki.
Itakumbukwa kwamba,
mwezi Agosti 2010, taasisi ya utafiti ya kimataifa ya Synovate ilitoa utafiti
ikionyesha kwamba CCM itashinda Uchaguzi Mkuu wa 2010 kwa asilimia 61. Baadhi
ya wana-CCM hawakufurahishwa na matokeo ya utafiiti huo kwasababu waliamini
kwamba ushindi wetu ulikuwa ni mkubwa zaidi. Wapinzani waliwalaani, kuwatukana
na hata kutaka kuwashtaki Synovate. Kwenye matokeo halisi ya kura, CCM ilipata
asilimia zilezile 61 zilizotabiriwa na Synovate.
Ni vyema kuweka akiba
ya maneno kwenye masuala haya.
Imetolewa na:
January Makamba
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
23.09.2015
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
23.09.2015
Post a Comment