Ipitie Hotuba ya kuanza rasmi kutumika kwa sheria ya makosa ya mtandao hapa nchini


unnamed (22) Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Prof. Makame Mbarawa (Mb), akiongea na waandishi wa habari kuhusu kuanza kutumika rasmi kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao na ya Miamala ya Kieletroniki za mwaka 2015. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bwana John Mngodo
Ndugu Wandishi wa Habari,  Mabibi na Mabwana,
Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru nyote hasa waandishi wa habari kwa kutenga muda wenu na kujumuika nasi kwa lengo la kutangaza rasmi kuanza kutumika kwa Sheria ya Makosa ya Mtandao, 2015 ambayo ilitangazwa kwenye gazeti la Serikali  la tarehe
14/08/2015 na kupewa Na. 328. Pia Sheria ya Miamala ya Kielektroniki, 2015
ambayo  ilitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la tarehe hiyo hiyo na
kupewa Na.329.
Ndugu Wananchi, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) ni nyenzo ya kisasa inayotumika kubeba na kusafirisha ujumbe, taarifa,
takwimu, picha na sauti kwa kutumia njia na mifumo mbalimbali ya mawasiliano
iliyopo, kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine au eneo moja kwenda eneo
lingine kwa uharaka, ufasaha, kwa wakati na kwa kiwango cha ubora ule ule bila
kujali umbali na mipaka iliyopo ya kijiografia.
Matumizi ya TEHAMA yameleta
mafanikio katika kuharakisha, kuboresha na kurahisisha utoaji wa huduma kwa
wananchi na kuchangia kukuza uchumi na kuleta maendeleo nchini. Mathalani,
wananchi walio wengi sasa wanapata huduma mbalimbali za kifedha, kulipia huduma
(leseni, kodi, Ankara), matumizi ya mitandao ya kijamii, barua pepe na huduma
mtandao kama vile Serikali mtandao, afya mtandao, kilimo mtandao, biashara
mtandao, Elimu mtandao, n.k
Ndugu Wananchi Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo
kumekuwepo na changamoto mbalimbali kama vile wizi wa fedha kwa njia ya
mtandao, uvujaji wa taarifa, kusambazwa kwa ujumbe wa matusi, picha chafu,
uchochezi, udhalilishaji, vitisho kupitia mitandaoni.
Vile vile kuna watu wachache ambao wanaharibu miundombinu ya mawasiliano, kwa mfano wanakata mkongo
wa Taifa wa mawasiliano na mikongo mingine ya mawasiliano na hili lina athari
kubwa sana kwa nchi yetu na kwa nchi za jirani ambazo zimeunganishwa kwenye
mkongo wa Taifa wa mawasiliano.
Ndugu Wananchi , Mtakumbuka kuwa, mnamo tarehe 1
Aprili 2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha Sheria ya
Makosa ya Mtandao ya Mwaka 2015 na Sheria ya Miamala ya Kielektroniki ya Mwaka
2015. Pamoja na masuala mengine, sheria hizi zinabainisha makosa, kutambua
ushahidi wa nyaraka za kielektroniki na pia kuainisha adhabu zinazokwenda
pamoja na makosa mbalimbali ya kimtandao.
Sheria hizi ni muhimu sana na zina
manufaa makubwa kwenye jamii yetu haswa katika nyakati hizi ambapo matukio ya
uhalifu wa mtandao yamekuwa yakiongezeka na kukosekana kwa Sheria hizi
kumefanya Wananchi kutokuwa na mahala pa kukimbilia pale wanapokumbana na
uhalifu kupitia mitandaoni.
Aidha, ninatambua ya kuwa Sheria
hizi zimepokelewa kwa hisia tofauti kutokana na uelewa mdogo kwa wengi wetu
kuhusu sheria hizi. Vilevile ni ukweli usiopingika kuwa kumekuwa na tafsiri
hasi kwa baadhi ya wananchi juu ya maudhui ya sheria hizi na kuzifanya
zitafsiriwe kama kandamizi zaidi kitu ambacho ni tofauti na dhana na maudhi ya
sheria hizi.  
Kwa kutambua hilo, Wizara ya
Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia mara baada ya kupitishwa kwa SHERIA
hizi  ilianza kuwaelimisha wananchi kupitia vyombo mbalimbali vya
habari na kuwa na mikutano na makundi mbalimbali ya watekelezaji wa Sheria hizi
ili kuwajengea uelewa ikiwemo Jeshi la Polisi, Waendesha Mashtaka, Wachunguzi,
Wapelelezi, Mahakimu na Majaji kuhusu Sheria hizi kwa pande zote mbili za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania yaani Bara na Zanzibar.
Aidha, ili kuhakikisha kuwa usimamizi na utekelezaji wa Sheria hizi unakwenda vizuri, Wizara itaendelea
kuwajengea uelewa Wadau mbalimbali. 
Ndugu Wananchi Tanzania siyo nchi ya kwanza kutunga
sheria kama hizi. Kuna nchi mbalimbali duniani ambazo zimetunga sheria kama
hizi, kwa mfano nchi ya Uingereza (UK Computer Misuse Act, 1990), India (IT
Act, 2000), Malaysia (Computer Crime Act), Uganda (Computer Misuse Act, 2010),
Korea ya Kusini (Information and Communications Network Act na Information and
Communication Infrastructure Protection Act), Singapore (The Computer Misuse
and Cyber security Act), Mauritius (Computer Misuse and Cybercrime Act, 2003),
Marekani (Computer Fraud and Abuse Act, 1984) na nyingi nyenginezo. 
Ndugu Wananchi, Serikali baaada ya kujiridhisha kuwa
maandalizi yote muhimu ikiwemo elimu kwa umma na kujenga uelewa kwa watekeleza
wa sheria hizi yamefanyika. Sasa, Sheria hizi zitaanza kutumika rasmi tarehe
01/09/2015. 
Kwa hivyo, natoa rai na wito kwa
wananchi wote kuwa tuzingatie “Matumizi Salama na sahihi ya Huduma za
Mawasiliano na Mtandao kwa manufaa ya kila  mmoja  na kwa maendeleo
ya Taifa letu. Mitandao ikitumiwa vema ina faida kubwa sana katika jamii yetu.
AHSANTENI KWA KUNISIKILIZA.

Post a Comment

Previous Post Next Post