press
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia chama cha ukombozi wa Umma (CHAUMA) Hashim Rungwe akizungumza na waandishi wa habari wa Star TV, TBC na ITV juu ya hali ya kampeni ilivyo hadi sasa.(PICHA NA HILLARY SHOO).
Na Hillary Shoo, SINGIDA
ZIKIWA zimebaki siku 27 kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu, Mgombea Urais wa Tanzania kwa tiketi cha Chama  cha Ukombozi wa Umma CHAUMA, Hashim Rungwe, ametoa tathimini yake juu ya mwenendo wa kampeni pamoja na matumaini yake katika kuibuka mshindi.
Rungwe alisema ingawa ziko changamoto zinazojitokeza lakini kwa ujumla kampeni  zinakwenda vizuri na anamatumaini makubwa ya kuingia Ikulu  kutokana na watanzania kuhitaji mabadiliko.
Akiwa Mkoani Singida ambao ni mkoa wa 10 katika mwendelezo wa ziara yake ya kuwaomba Watanzania  wamchague kuwa Rais, baada ya kumaliza mkutano wake Mgombea huyo wa CHAUMA Hashim Rungwe alikutana na waandishi wa habari kutoa tathimini juu ya mwenendo wa Kampeni.
Aidha  alisema kuwa Matumaini yake  makubwa ni  kuibuka mshindi na kuwa Rais wa Tanzania katika awamu ya tano kwa kuwa wananchi wamechoka na ahadi za kila siku kutoka chama tawala ambazo hazitekelezeki na huku maisha yakizidi kuwa magumu.
“Huu ni wakati sasa wa mabadiliko,tuwapumzishe hawa CCM wamechoka , wanatuita malofa na wapumbavu sasa ni wakati wa malofa na wapumbavu kuongoza nchi hii, uwezo wao wa kuongoza ni mdogo, betri hazina chaji wapuuzeni hawa, mimi betri ina chaji imejaa full, nipeni miaka mitano muone kazi yangu.” Alisema.
Aidha pamoja na matumaini aliyonayo, mgombea huyo anakiri kuwa mazoea na umaarufu bado ni changamoto kubwa kwani watu wakisikia kuwa kuna mgombea fulani wa chama  watu wanajazana kuwasikiliza na wengine wanataka tu kuwaona sura zao zikoje lakini ukweli unabaki kwenye mioyo yao.
“Mafuriko kitu gani bwana wengine wanasikia tu fulani ni fisadi na hajawahi kuona fisadi anafananaje na ndio maana wanafurika kwenye mikutano,hili mimi halinitishi sera tu ndio jambo la maana kwangu na nina imani kubwa kuwa nitaibuka kidedea. ‘ Alijigamba Rungwe.
Hata hivyo Rungwe alisema kipindi alichokuja Papa John Paul II watu wengi walijitokeza,wengine hata wasio Wakristo walifurika kumwona hata yeye alikwenda kumwona, hivyo suala mafuriko kwake halimpi shida.
Ingawa kila Mgombea wa Udiwani, Ubunge na Urais anamatumaini ya kushinda katika uchaguzi mkuu, lakini  jibu la ukweli linabaki kuwa kwenye sanduku la kupigia kura siku ya Jumapili ya  tarehe 25  mwezi ujao.