JUMAPILI
ijayo, baada ya hii ya keshokutwa, Watanzania kwa ujumla wetu, tutakuwa
katika vituo mbalimbali vya kupigia kura, tayari kwa zoezi ambalo
limetufanya kuwa na presha kubwa kwa miezi kadhaa sasa, kupiga kura.
Zoezi hilo kwetu ni muhimu sana kwa
sababu ndilo litakaloamua hatima ya maisha yetu kwa kipindi cha miaka
mitano ijayo. Ni muda mchache maana miaka mitano iliyopita tulifanya
kama hivi, lakini leo tunalia kwa kinachoendelea.
Ni siku ambayo wengi tunaamini
tutakwenda kutumia vichinjio vyetu kwa ajili ya kuleta mabadiliko, maana
maisha haya ya sasa, kila mmoja yamemchosha. Ufisadi kila kona,
ubadhilifu serikalini ndiyo usiseme, wapiga dili kila sekta, rushwa nayo
ni hatari, ilimradi kila mtu anayepata nafasi katika utumishi wa umma,
anautumia yeye na wanaomzunguka kujinufaisha.
Kila mmoja anaona jinsi ambavyo
watumishi wa serikali wanavyojipatia utajiri unaokosa maelezo. Mtu
kapata nafasi ya kuitumikia nchi katika cheo f’lani akiwa hana kitu
kabisa, lakini unashangaa kuona kuwa baada ya miaka michache tu, mtu
ameshakuwa na utajiri wa kutisha, anamiliki mali nyingi ambazo kwa
hakika, hazina maelezo.
Nchi yetu imekuwa ya wapiga dili, yaani
mtu yupo sehemu f’lani kule serikalini, basi ndugu zake wanapewa
upendeleo, ardhi yenye rutuba wanachukua wao, tenda wanapeana wao na
vitu vingine chungu nzima. Njoo kwenye utendaji kazi wao sasa, muda
mwingi wanafanya kazi zao binafsi lakini kwa gharama za vifaa na muda wa
serikali. Kifupi nchi yetu inahitaji mabadiliko makubwa. Tunahitaji
kumpata kiongozi ambaye anaweza kusema hapana na ikawa.
Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo
ningependa sana kuwashauri wapiga kura wenzangu ambao Jumapili ile
tutakuwa pamoja vituoni. Kuna baadhi ya wagombea wanatangaza hofu ya
kuibiwa kura. Ili kuhakikisha kura zao zipo salama, wanawahamasisha
wapiga kura wenzangu kubaki vituoni ili kuzilinda.
Sitaki kujadili uhakika walionao kwamba
wana kura nyingi zitakazoibwa, ninachotaka kushiriki na wenzangu ni
kwamba kama viongozi wanasema baada ya kupiga kura tusiende umbali mrefu
zaidi ya mita 100, kisha tukae hapo kuhakikisha kura haziibwi.
Huenda wana hofu hiyo kutokana na uzoefu
wao katika zoezi hili tangu lianze 1992. Lakini katika kutekeleza hili
la kutoondoka umbali mrefu vituoni, nishauri kwamba viongozi wanaohubiri
jambo hili, wawe wa kwanza kukaa na kusubiri umbali huo baada ya kupiga
kura.
Mgombea wa urais, ubunge na udiwani awe
wa kwanza kusimama umbali huo, ili sisi wapiga kura tuwe na uhakika na
wanachokitetea. Akae hapo atuongoze kwa sababu yeye anajua zaidi sheria
na kanuni za uchaguzi, kwani hata mamlaka zingine zitakapokuja kuuliza
kwa nini tupo hapo, awe wa kwanza kutuongoza kuzungumza.
Ninaogopa wapiga kura wanaweza kutumiwa
kama chambo, wao wakae hapo waimbe nyimbo za ushindi, viongozi wao
wakiwa wamekaa sebuleni wanatazama televisheni zao jinsi wanavyopata
usumbufu kwa mamlaka zingine.
Kama kweli viongozi hawa wanamaanisha, basi na iwe hivyo, vinginevyo,
nisingekushauri kufanya hivyo kwa sababu nyingi, lakini muhimu zaidi ni
swali, tangu lini kura moja ikaamua mshindi?
Nilisema na nitarudia tena, kura ya
uhakika ambayo mgombea wako amepigiwa ni yako peke yako, zingine si zako
kwa sababu hujui mwenzako kampigia nani. Kuna watu watajiunga na wewe
kukurubuni kuwa wamempigia chaguo lako kwa sababu wanataka uanzishe fujo
ili wao waanze kupora au kufanya uhalifu mwingine. Chonde mpiga kura,
jukumu lako ni kupiga kura na kuondoka, mambo mengine waachie wenyewe
wanasiasa, wanajuana hao!
Post a Comment