Chama cha Mapinduzi hakijaridhishwa na utaratibu wa kukusanya na
kujumlisha matokeo kwenye baadhi ya majimbo. Katika majimbo manne
kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa utaratibu wa uchaguzi, hasa katika
kujumlisha matokeo, uliopelekea wabunge wa upinzani kutangazwa washindi.
Majimbo hayo ni Iringa Mjini, Mikumi, Ndanda na Kawe. Wasimamizi wa
uchaguzi katika majimbo haya wamevuruga uchaguzi. Kutokana na utata
uliokuwa umejitokeza wakati wa zoezi la kujumlisha kura, CCM iliomba
kura zihesabiwe upya lakini ikanyimwa haki hiyo ya msingi ambayo iko
kwenye sheria. Kwenye baadhi ya majimbo, ikiwemo Nyamagana, wapinzani
walipewa haki ya kura kuhesabiwa upya. Kwa msingi huo, CCM imeamua
kwenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzi katika majimbo haya.
Tunataka sote tujiridhishe kwamba utashi wa wananchi umeheshimiwa.
Bado tunaendelea kukusanya taarifa za maeneo mengine kama kulikuwa na
ukiukwaji mkubwa uliobadilisha matakwa ya wapiga kura. Hata hivyo,
tunakiri kwamba kwenye maeneo mengi tulikopoteza viti vya Ubunge,
tumepoteza kihalali, hatuna malalamiko, tunaheshimu maamuzi ya wananchi,
na tutafanya tathmini baada ya uchaguzi ili tubaini makosa na
kuyarekebisha.
MAONI YA WAANGALIZI WA UCHAGUZI
CCM imepokea maoni ya awali ya waangalizi wa uchaguzi. Tumefarijika
kwamba karibu wote wametoa kauli ya pamoja kwamba uchaguzi huu ulikuwa
wa haki na huru, uliofanyika kwa uwazi na kwa amani – na kwamba
changamoto zilizojitokeza ni ndogo na zimetokea katika maeneo machache
kiasi zisingeweza kubadilisha matokeo ya uchaguzi yanayotangazwa sasa.
Tumepokea mapendekezo waliyoyatoa kwa wadau mbalimbali kuhusu namna ya
kuboresha mchakato wa uchaguzi kwa miaka ijayo, na hivyo kuimarisha
demokrasia nchini mwetu. Kwa kauli za waangalizi hawa, kwamba, kwa jinsi
uchaguzi ulivyoendeshwa, matokeo yanayotangazwa sasa ni kielelezo
sahihi cha utashi wa Watanzania kuhusu viongozi wanaowataka.
MALALAMIKO YA UKAWA
Tumesikia malalamiko ya viongozi wa UKAWA kupitia mkutano wao na
waandishi wa habari jana. Tumeshangazwa na kauli kwamba hawakubali
matokeo ya Urais yanayotangazwa na Tume. Hata hivyo, matokeo ya Ubunge
wanayakubali na, kule wanakoshinda, wanayasheherekea. Tunashangazwa
kwasababu Tume iliyoandaa uchaguzi wa Rais ni hiyo hiyo iliyoandaa
uchaguzi wa Wabunge, wasimamizi ni walewale, vituo ni vilevile, na
sheria na taratibu zilizotumika ni zilezile. Hata fomu ya matokeo
walizosaini wakala wao kwenye vituo vya kupiga kura, zimegawanywa katika
sehemu (columns) tatu: Urais, Ubunge na Udiwani. Mawakala wao walisaini
fomu hizo kwenye vituo vya kupiga kura. Wameanza kuwa na matatizo na
matokeo haya baada ya kuona mwelekeo wa kushindwa. Kama mwelekeo
ungekuwa tofauti, wangekuwa na imani na Tume, wasimamizi na taratibu
zote.
Tunaomba ifike pahala sasa kwamba, katika kuijenga demokrasia yetu na
kuliimarisha taifa letu, tuanze utamaduni mpya wa anayeshindwa kunyanyua
simu kumpigia anayeshinda na kumpongeza. Nafasi ya mwisho aliyonayo
Mgombea wa UKAWA kuendelea kujijengea heshima katika jamii yetu, na kuwa
mwanademokrasia, ni kwa kufanya hivyo siku Dkt. Magufuli
atakapotangazwa mshindi. Kusoma zaidi
Kwetu sisi CCM, kuchagua wagombea bora na kuwanadi na kutengeneza
sera bora na kuzinadi, pamoja na rekodi yetu katika uongozi wa nchi,
ndio njia zetu pekee za ushawishi. Katika uchaguzi huu, wananchi
wamefanya maamuzi yao kwa uhuru na utashi, ikiwemo kuwaangusha mawaziri
sita ambao tuliwasimamisha kama wagombea wetu katika majimbo mbalimbali.
Nguvu na utashi wa wananchi umejidhihirisha katika uchaguzi huu.
Mchakato wa uchaguzi sasa unakaribia kufikia ukingoni, tutawapata
madiwani, wabunge na Rais, tunapaswa kuendelea na maisha na tuwape
nafasi watutumikie. Jitihada tunazoziona sasa za viongozi wa UKAWA za
kuendeleza siasa za uchaguzi kwenye mitaa ya miji yetu kwa njia za
vurugu na maandamano hazikubaliki hata kidogo. Tunalaani kitendo cha
wafuasi wa UKAWA kuchoma ofisi za CCM katika Wilaya ya Mbozi. Amani ya
nchi hii ina thamani kuliko hitaji la madaraka la mtu yoyote. Wenzetu wa
UKAWA wana haki ya kulalamika lakini hawana haki ya kuiingiza nchi yetu
machafukoni kwa kuwakusanya vijana na kuwaingiza mitaani wafanye vurugu
na kuhatarisha maisha, kuharibu mali na kusimamisha shughuli za watu
wengine. Tunawaomba Watanzania waendelee na shughuli zao kama kawaida
huku kila mmoja akitambua wajibu wake wa kuilinda amani ya nchi yetu.
January Makamba
Mjumbe wa Kamati ya Kampeni ya CCM
28.10.2015
Post a Comment