Tume
ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imeyaondoa majina ya wapiga kura zaidi ya
milioni moja kutoka katika orodha ya awali ya watu milioni 23.7
waliojiandikisha awali kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa mfumo
wa kielektroniki (BVR).
Akizungumza kwenye mkutano wa NEC na viongozi wa vyama vya siasa
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian
Lubuva, alisema hatua ya kupunguzwa kwa idadi ya wapiga kura inatokana
na kukamilika kwa kazi ya uhakiki wa majina ya watu wote
waliojiandikisha.
Alisema kuwa awali, idadi ya watu walioandikishwa kupiga kura ilikuwa 23,782,558.
Hata hivyo, baada ya uhakiki, imebainika kuwa majina 1,031,769
kutoka miongoni mwa orodha ya awali hawastahili kuwamo kwani baadhi yao
ni majina ya watu waliojiandikisha zaidi ya mara moja, wengine siyo
Watanzania na wapo pia waliokosa sifa nyingine muhimu za kupiga kura,
kwa mujibu wa sheria za nchi.
Kwa sababu hiyo, Jaji Lubuva alisema idadi halisi ya watu
watakaokuwa na fursa ya kupiga kura Oktoba 25 ni 22,251,292 kwa Tanzania
Bara na wengine 503,193 wa visiwani Zanzibar.
Jaji Lubuva alieleza zaidi kuwa baada ya uhakiki na uchakataji wa
taarifa za wapiga kura, NEC ilibaini kuwa wananchi 181,452
walijiandikisha zaidi ya mara moja, huku baadhi yao wakitia fora kwa
kujiandikisha hadi mara nane.
Akifafanua zaidi, mwenyekiti huyo wa NEC alisema uhakiki umebaini
kuwa wananchi 845,944 waliandikishwa na waandishaji 74,502 waliokuwa
kwenye mafunzo ya vitendo kabla ya kuanza uandikishaji, hivyo majina yao
yameondolewa, huku majina 3,870 yakibainika kuwa ni ya watu wasiokuwa
raia wa Tanzania na hivyo, taarifa zao pia zimefutwa.
VITUO VYA KURA VYAPANGULIWA
Katika hatua nyingine, NEC imetangaza idadi rasmi ya vituo vya
kupigia kura nchini kuwa ni 65,105, kati yake 1,580 vikiwa visiwani
Zanzibar na vilivyobaki (63,525) vikiwa Tanzania Bara. Idadi hii ni
pungufu kulinganisha na idadi ya vituo vilivyokadiriwa awali kabla ya
kufanyika kwa uhakiki, ambavyo NEC ilitangaza kuwa vitakuwa 72,000 na
kwamba, vinaweza kuongezwa au kupunguzwa kulingana na mahitaji kadiri
itakavyoonekana inafaa. Kadhalika, idadi hiyo iliibua shaka pia kutoka
kwa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vya Chadema,
CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.
Mgombea mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alielezea shaka waliyonayo
wiki iliyopita kwa kudai kuwa wastani wa wapiga kura 450 kwa kila kituo
unahitaji vituo takribani 53,000 tu kuhudumia wapiga kura milioni 23.7
na siyo 72,000. Duni aliongeza kuwa Ukawa wanahofia kuwapo kwa njama za
kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia vituo bandia 20,000
vilivyoongezeka kulingana na mahitaji na uwezo wa kila kituo.
Hata hivyo, NEC ilipuuza madai hayo kwa kueleza kuwa hakuna vituo
vyovyote bandia na kwamba idadi hiyo ni ya makadirio ya awali kabla ya
uhakiki.
Katika hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano wa jana, Jaji Lubuva
alisema kila kituo kinapaswa kuwa na idadi ya wapiga kura kati ya 450
hadi 500, na kwamba ikitokea kuna kituo kinakuwa na wapiga kura zaidi ya
500, watakachofanya ni kukigawanya katika vituo viwili vyenye idadi
sawa ya wapiga kura.
“Hiyo ndiyo idadi ya vituo vitakavyotumika siku ya uchaguzi.
Isipokuwa wananchi wanapaswa kuhakiki taarifa zao siku nane kabla ya
uchaguzi ili kujiepusha na usumbufu utakaotokana na mgawanyo wa vituo,”
alisema.
MAJIMBO, KATA
Lubuva alisema NEC imetekeleza wajibu wake wa kuongeza majimbo
mapya 25 na pia Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (Tamisemi) imeanzisha kata mpya 622, hivyo jumla ya majimbo
yatakayogombewa kwa nafasi za ubunge ni 264 na kata zote ni 3,957.
Aliongeza kuwa uchaguzi wa wabunge katika majimbo matatu
umeahirishwa baada ya kutokea kwa vifo vya wagombea. Majimbo hayo ni
Ulanga Mashariki lililompoteza mgombea kutoka CCM, Celina Kombani; Jimbo
la Lushoto lililompoteza mgombea kutoka Chadema, Mohamed Mtoi na Jimbo
la Arusha Mjini lililoondokewa na mgombea ubunge kutoka ACT-Wazalendo,
Estomiah Mallah.
Aliongeza kuwa uteuzi wa wagombea umeshafanyika katika majimbo ya
Ulanga Mashariki na Lushoto na kwamba jana na kwamba, kampeni zitaanza
leo hadi Novemba18 huku uchaguzi wao ukitarajiwa kufanyika Novemba 22.
Ratiba ya uchaguzi wa Jimbo la Arusha mjini bado haijatolewa.
MNYIKA AISHNGAA NEC
Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), ambaye pia ni mgombea ubunge
wa Jimbo la Kibamba, John Mnyika, alisema chama chake kiliandika barua
wakidai kuwa wapatiwe orodha ya majina ya wapigakura pamoja na idadi ya
vituo vya kupigia kura, lakini anashangaa kuona kuwa hilo
halikufanyika.
“Nashangaa barua hiyo nimekabidhiwa leo, lakini haijaeleza ni lini orodha hiyo itapatikana,” alisema.
Mgombea urais wa Zanzibar kupitia Tadea, Juma Ali Khatibu,
alielezea wasiwasi wao juu ya kutegemea mawasiliano kwa njia ya mkongo
wa taifa katika utoaji wa matokeo, akisema kuwa kufanya hivyo ni sawa na
kuchelewesha matokeo na kusababisha usumbufu kwa wapigakura.
Mwenyekiti wa ADC, Said Miraji, alisema kuwa changamoto iliyopo kwa
NEC ni kutoaminika kutokana na historia ya viongozi wao waliotangulia,
hivyo aliwataka waliopo kuacha tabia ya kulalamika na badala yake
watatue matatizo yaliyopo.
Mgombea ubunge wa Jimbo la Ubungo ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa
Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Kabendera Eugen, alisema hakuna
sababu ya kuwa na hofu na NEC, bali chombo hicho kinapaswa kufuata
taratibu na haki.
Akijibu maswali na hoja mbalimbali zilizoibuliwa na viongozi wa
vyama, Mkurugenzi wa NEC, Kailima Ramadhan, alisema kuwa baada ya
kutangaza idadi ya wapigakura na vituo, sasa kila kitu kimekamilika na
kuwataka viongozi wa vyama vya siasa kuwasiliana na NEC ili kupatiwa
orodha hizo.
Pia, Kailima aliwatoa hofu viongozi wa vyama vya siasa kwa kuwaleza
kuwa mfumo watakaoutumia kutoa matokeo umehakikiwa na Shirika la Umoja
wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP) kupitia wataalamu mbalimbali,
baadhi wakitoka nchini Ufaransa.
“Kila kitu kitafanyika kwa uwazi. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu... kila kitu kitakuwa salama,” alisema
Aidha, alisema uchaguzi ni kazi kubwa na muhimu na kuhusisha wadau
wengi, vikiwamo vyama vya siasa, hivyo mafanikio yanategemea ushirikiano
mzuri wa NEC na vyama.
Alisema wao wamejipanga kusimamia na kuhakikisha kuwa daima haki
inatendeka ili kulinda amani na utulivu na kwamba, kwa sababu hiyo, ni
wajibu wa vyama vya siasa kutumia majukwaa yao kuwaelimisha wafuasi wao
kutokusanyika jirani na vituo vya kura, bali watekeleze wajibu wao wa
kupiga kura na kuondoka.
Mkutano wa jana kati ya NEC na vyama vya siasa ulikuwa na lengo la
kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya
Uchaguzi Mkuu na pia kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya uchaguzi.
CHANZO:
NIPASHE

Post a Comment