STORY TANO MUHIMU KUTOKA TFF LEO




Mzunguko wa raundi ya sita ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (VPL) unatarajiwa kuendelea kesho Jumamosi na Jumapili kwa timu 10 kucheza kusaka alama 3 muhimu.
Jijini Tanga Mgambo Shooting watakua wenyeji wa Coastal Union katika uwanja wa Mkwakwani, Majimaji FC watawakaribisha Mwadui FC uwanja wa Majimaji mjini Songea.
Jumapili Stand United chama la wana watawakaribisha watoza ushuru wa jiji la Mbeya (Mbeya City) katika uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga, huku Kagera Sugar wakiwa wenyeji wa Tanzania Prisons uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora na Toto Africa watakua wenyeji wa JKT Ruvu jijini Mwanza uwanja wa CCM Kirumba.

Kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) inayodhaminiwa na bia ya Kilimanjaro Premium Lager kimeanza mazoezi leo mchana katika uwanja wa Taifa kujiandaa na mchezo dhdi ya Malawi utakaocheza Jumatano Oktoba 7, 2015 kuwania kufuzu kwa Fainali za Kombe la Dunia mwaka 2018 nchini Urusi.
Stars inayonolewa na kocha mkuu mzawa Charles Mkwasa, akisaidiwa na Hemed Morroco, Peter Manyika na mshauri wa Ufundi Abdallah Kibadeni wameingia kambini jana katika hoteli ya Urban Rose iliyopo Kisutu jijini Dar es salaam.
Wachezaji wote wameripoti kambini isipokuwa wachezaji wa kimataifa wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi, Mrisho Ngasa, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaotarajiwa kuungana na wenzao mwishoni mwa wiki baada ya kumaliza michezo inayowakabili wikiendi hii.
Wachezaji waliopo kambini ni magolikipa All Mustafa, Aishi Manula, Said Mohamed, walinzi Juma Abdul, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Haji Mwinyi, Hassan Isihaka, Kelvin Yondani na nahodha Nadir Haroub “Cannavaro”.
Wengine ni viungo Himid Mao, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Said Ndemla, Salum Telela, Deus Kaseke, Saimon Msuva, Farid Musa, washambuliaji John Bocco, Rashid Mandawa na Ibrahim Hajibu

Ligi Daraja la Kwanza nchini (StarTimes First League) inaendelea wikiendi hii kwa makundi yote matatu kucheza, michezo 11 itachezwa mwishoni mwa wiki siku za Jumamos na Jumapili katika viwanja mbalimbali nchini.
Jumamosi Kundi A, Ashanti United watakua wenyeji wa Mji Mkuu (CDA) katika uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, KMC watawakaribisha Polisi Dodoma katika uwanja wa Mabatini – Mlandizi.
Kundi B, Lipuli FC watawakaribisha Polisi Morogoro katika uwanja wa Wambi mkoani Iringa, Kimondo FC watakuwa wenyeji wa JKT Mlale kwenye uwanja wa CCM Vwava – Mbozi, huku Burkinafaso ya Morogoro ikiwakaribisha Njombe Mji katika uwanja wa Jamhuri.
Kundi C, JKT Kanembwa watakuwa wenyeji wa Panone FC katika uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, JKT Oljoro watawakaribisha Polisi Moro uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Geita Gold watacheza na Rhino Rangers uwanja wa Nyankumbu mkoani Geita na Polisi Tabora watawakaribsiha Mbao FC mjini Tabora uwanja wa Ali Hassa Mwinyi.
Ligi hiyo itaendelea siku ya Jumapili kwa michezo miwili ya Kundi A, Friends Rangers watacheza dhidi ya African Lyon uwanja wa Karume jijini Dar es salaam, na Polisi Dar watakua wenyeji wa Kiluvya FC katika uwanja wa Mabatini Mlandizi.

Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu wa nchini (TFF), Jamal Malinzi ametuma salam za pongezi kwa Alberto Simago Junior wa Shirikisho la Mpira wa Miguu la Msumbiji (FMF) na Sidiki Tombi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini Cameroon (FECAFOOT) kufuatia kuchaguliwa kuwa marais wa mashiriksho ya mpira miguu.
Katika salam zake kwenda FMF na FECAFOOT, Malinzi amesema kuchaguliwa kwao kuogoza mashirikisho hayo kumetokana na imani ya wanafamilia wa mpira miguu.
Kwa niaba ya Kamati ya Utendaji ya TFF na familia ya mpira wa miguu nchini, anawapa pongezi kwa kucgahuliwa kwao.
TFF inaahidi kushirikiana na uongozi mpya wa FMF na FECFOOT katika maendeleo ya mpira wa miguu Afrika na Dunia kote.

Timu ya Taifa ya Tanzania bara (Kilimanjaro Stars) imedhibitisha kushiriki michuano ya timu za Taifa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Chalenjji) itakayofanyika nchini Ethiopia kuanzia Novemba 21 – 06 Disemba, 2015.
Michuano ya CECAFA Chalenji ndio michuano mikongwe zaidi barani Afrika ambapo jumla ya nchi 12 wanachama hushirki michuano hiyo iliyofanyika mara ya mwisho mwaka juzi nchini Kenya na wenyeji kutwaa Ubingwa huo.
Nchi wanachama wa CECAFA ni Tanzania Bara, Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Ethiopia, Eritrea, Djibouti, Somali, Sudan, Sudan Kusini na Zanzibar.

Post a Comment

Previous Post Next Post