index2
Katibu Mkuu Kiongozi  Mhe. Balozi Ombeni Sefue akiwaonyesha waandishi wa Habari (hawapo pichani) beji yenye jina lake ambayo amewaagiza watumishi wa Umma kuivaa wanapokuwa  katika maeneo  yao ya  kazi. Balozi Sefue alifanya mkutano na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam jana na kutoa taarifa ya Serikali kuhusu kesi ya Serious Fraud Office (SFO) dhidi ya Standard Bank. (Picha na Maelezo).
11-460x300
Na Anna Nkinda – Maelezo
Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. Balozi Ombeni Sefue ameendelea kuwasisitiza watumishi wa Umma kuvaa beji zinazowatambulisha majina yao wanapokuwa  katika maeneo  ya  kazi.
Mhe. Balozi Sefue aliutoa mwito huo jana wakati akijibu swali la Mwandishi wa Habari aliyemuuliza ni kwanini alikuwa amevaa beji yenye jina lake ambayo imemfanya kuonekana tofauti na siku zingine.
Alisema mwishoni mwa mwezi wa kumi na moja alifanya ziara ya kutembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili na kuagiza  watumishi wote wa Umma kuvaa beji zinazowatambulisha majina yao.
“Nimeamua kuonyesha mfano kwa vitendo kufuatia agizo nililolitoa kwa watumishi wa Umma kwa kuvaa beji inayonitambulisha jina langu , nilisema nitakuwa wa kwanza kuvaa jina langu nimevaa. Kama mtumishi wa umma atakuwa na mashaka ajue mimi nimeshalivaa”.
“Mtumishi wa umma anapomuhudumia mwananchi ni lazima ajue amehudumiwa na nani, mtumishi wa Umma akifanya  kazi zake kwa kutenda haki sidhani kama ataogopa kuvaa beji inayomtambulisha jina lake hivyo basi kama nilivyoagiza watumishi wote wa Umma mvae beji zinazowatambulisha majina yenu”, alisisitiza Mhe. Balozi Sefue.
Mhe. Balozi Sefue alifanya mkutano na waandishi wa habari Ikulu jijini Dar es Salaam na kutoa taarifa ya Serikali kuhusu kesi ya Serious Fraud Office (SFO) dhidi ya Standard Bank.