Wema Sepetu anaswa wizi wa maji jijini Dar!
Ufisadi? Wakati soo lake la kubambwa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) akidaiwa kuliibia umeme kwa figisufigisu za kimjini, staa wa sinema za Kibongo, Wema Isaac Sepetu, wikiendi iliyopita amenaswa tena akidaiwa kuifanyia ufisadi wa aina hiyo Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka ya jijini Dar es Salaam, Pwani na Bagamoyo (Dawasa).

NI SIKU CHACHE
Wema amekumbwa na msala huo uliofananishwa na ufisadi wa makontena bandarini, ikiwa ni siku chache baada ya gazeti ndugu la hili, Amani kuandika habari inayohusu mrembo huyo kuiibia Tanesco umeme.

KUTOKA KWENYE MAMLAKA
Akizungumza na Ijumaa Wikienda, Mkurugenzi wa Biashara wa Dawasa, Everade Maswile Balati alisema kuwa baada ya kusoma habari ya Wema na Tanesco, aliwatuma wafanyakazi wa mamlaka hiyo kwenda kufanya ukaguzi wa mita ya maji nyumbani kwa mwanadada huyo maeneo ya Kijitonyama, Dar.

“Baada ya kusoma ile habari ambayo mliandika kupitia moja ya magazeti yenu (Amani), niliwasiliana na Meneja wa Dawasa wa Area ya Kinondoni, Judith Singinika aende na vijana wakafanye ukaguzi wa mita yetu nyumbani kwa Wema,” alisema mkurugenzi huyo.

NYUMBANI KWA WEMA
Alimwaga ‘ubuyu’ kuwa, baada ya wafanyakazi hao waliongozwa na meneja huyo wa Area ya Kinondoni kufika nyumbani kwa Wema, walimkuta mlinzi ambaye aliwawekea ngumu kuingia lakini hata hivyo, walifanikiwa kuingia ndani kwa njia waliyoijua wao.

Mkurugenzi huyo alisema, kwa mujibu wa wafanyakazi hao, walipoingia ndani waliwakuta wasaidizi wa Wema ambao walipowaona walijua palikuwa na tatizo hivyo wote wakakimbilia ndani, wakafunga milango na kuanza kuwachungulia kupitia madirishani.

WAKUTA MITA IMEGEUZWA
“Walipoingia ndani waliwakuta wasaidizi wa Wema nahisi alikuwepo na huyo sijui anayeitwa Petit Man, walipogundua palikuwa na tatizo, wote wakaingia ndani, wakafunga milango na kuanza kuwachungulia wafanyakazi wa Dawasa madirishani, walipoigagua mita wakabaini ilikuwa imegeuzwa hivyo ikawa inasoma kwa kurudi nyuma, yaani inafuta matumizi halisi ya maji,” alisema Balati.

MLINZI AKIMBIA
Aliongeza kuwa baada ya kuona wahusika wameitelekeza nyumba, waliamua kuondoa mita baada ya kukata maji kisha wakatoka ili kumkamata mlinzi waondoke naye lakini wakakuta naye amekimbia.

MENEJA AREA YA KINONDONI
Akizungumza na Ijumaa Wikienda kuhusu oparesheni hiyo, Meneje wa Area ya Kinondoni, Judith Singinika alisema walipofika walibaini kugeuzwa kwa mita ndipo waliamua kukata maji.

Singinika aliongeza kuwa mwaka 2013 mwishoni Wema alikuwa akidaiwa shilingi milioni 1.52,000 na baada ya kulipa alisema hahitaji tena maji atakuwa akinunua.
Aliongeza kuwa licha ya kufuatwa mara kadhaa na kushawishiwa awe analipa kidogokidogo alikataa.

ADHABU
Akizungumzia adhabu anayotakiwa kupewa alisema kama wangemkuta wangemfungulia kesi polisi kisha kumpeleka mahakamani kwa sababu alichokifanya ni sawa na uhalifu mwingine.

ADAIWA MAMILIONI
“Tangu alipoacha kulipia maji (tangu akiwa anaishi na Diamond), kwa sasa deni lake linafikia shilingi milioni 9,” alisema Singinika.

Kwa upande wake Balati alisema kitendo alichokifanya Wema hakikubaliki na Dawasa kwani akiwa staa anapaswa kuwa mfano bora katika jamii na kwamba ameitia hasara kubwa mamlaka yetu ambayo kila kukicha inatumia gharama kubwa kununua madawa lakini kuna watu kama akina Wema wanaihujumu Dawasa.

“Wema hana tofauti na wakwepa kodi wengine huko TRA wanaotumbuliwa majipu hivyo tutapambana na kila anayefanya hivyo kumuunga mkono Rais John Pombe Magufuli,” alisema mkurugenzi huyo.

WEMA YUPO MOMBASA
Alipotafutwa Wema ili kusikia upande wake hakupatikana kwenye simu na alipofuatwa nyumbani kwake hakuwepo kwa maelezo kwamba alikuwa amesafiri kwenda Mombasa, Kenya hivyo jitihada za kusikia upande wake zinaendelea.

CHANZO: GPL

No comments:

Post a Comment