YANGA, SIMBA BOTI MOJA, URA YAIFUATA MTIBWA FAINALI


BAADA ya Simba kuondolewa na Mtibwa kwenye mchezo wa jioni ya leo wa nusu fainali ya kombe la Mapinduzi baada ya kufungwa bao 1-0, watani zao Yanga nao wameondoshwa na URA kwenye michuano hiyo kwa changamoto ya mikwaju ya penati 4-3
Yanga ndio walikuwa wa kwanza kupata bao katika dakika ya 13 kupitia kwa Amissi Tambwe akimalizia kwa kichwa mpira uliotemwa na kipa Brian Bwete kufuatia mpira wa kichwa uliopigwa na Simon Msuva.

Ikionekana kama pambano hilo lingeisha ndani ya dakika 90 kwa Yanga kuibuka na ushindi wa bao hilo moja, Peter Lwassa aliwainua vitini mashabiki wa URA kwa bao safi la dakika ya 76 na kusababisha mechi hiyo iende kwenye hatua ya penati.
Katika hatua hiyo URA walifanikiwa kushinda kwa penati 4 dhidi ya 3 za Yanga. Waliopata penati kwa upande wa Yanga ni Kelvin Yondan, Simon Msuva na Deogratius Munishi 'Dida' huku Geofrey Mwashiuya na Malimi Busungu penati zao zikiishia mikononi mwa kipa Brian Bwete.
URA wao walipata penati zao kupitia kwa Jimmy Kulaba, Said Kiyeyu, Deo Otieno na Bwete huku penati ya Sam Sekito ikiokolewa na Dida.
URA sasa watapambana na Mtibwa Sugar kwenye fainali itakayopigwa siku ya jumatano Januari 13 kwenye dimba hilo hilo la Amani.

No comments:

Post a Comment