Takukuru kukata rufaa hukumu ya Mhando wa Tanesco


Siku moja baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kumwachia huru aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), inaandaa utaratibu wa kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo. 
Aprili 14, mwaka huu Mahakama hiyo ilimwachia huru Mhando na wenzake wanne akiwamo mkewe, Eva na maofisa watatu wa Tanesco; Francis Mchalange, Sophia Misida na Naftali Kisinga waliokuwa wakikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya fedha. 
Mashtaka mengine yaliyokuwa yakiwakabili ni kughushi  na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa mamlaka za Serikali. 
Hata hivyo, washtakiwa hao waliibwaga Takukuru baada ya mahakama kuona kuwa upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha tuhuma hizo.
 Akisoma hukumu hiyo kwa niaba ya Hakimu Mkazi Mkuu, Kwey Rusema, Hakimu Hellen Riwa alisema kwa mujibu wa ushahidi, suala la msingi lilikuwa ni mkataba kati ya kampuni ya Santa Clara Supply Limited na Tanesco. 
Alisema katika mkataba, Mhando alikuwa mshtakiwa wa kwanza, akituhumiwa kutumia madaraka yake vibaya kwa kushindwa kutangaza masilahi yake kwa kampuni ya Santa Clara inayomilikiwa na Eva ambaye ni mkewe.
 “Suala la msingi ni kujiuliza ni vipi mshtakiwa huyo alihusika katika utoaji wa zabuni na nani aliyekuwa na uamuzi wa mwisho,” alisema. 
 Taarifa iliyotolewa jana na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Tunu Mley ilisema imefikia uamuzi huo baada ya wadau wengi kuhitaji kujua hatua zitakazochukuliwa na chombo hicho baada ya hukumu hiyo. 
“Takukuru inawataka wadau na wananchi kwa ujumla kutambua kwamba ni utaratibu wa kisheria kwamba upande mmoja usioridhika na hukumu iliyotolewa kukata rufaa katika mahakama ya juu,” ilieleza taarifa hiyo.
Baada ya hukumu hiyo juzi, Wakili wa Takukuru, Leonard Swai aliomba Mahakama kuingilia kati.

No comments:

Post a Comment