Hotuba Ya Waziri Wa Fedha Na Mipango, Mheshimiwa Dkt. Philip I. Mpango (Mb), Akiwasilisha Bungeni Mapendekezo Ya Serikali Kuhusu Makadirio Ya Mapato Na Matumizi Ya Fedha Kwa Mwaka 2016/2017


 UTANGULIZI
1.      Mheshpika, naomba kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17. 

Pamoja na hotuba hii, ninawasilisha vitabu vinne vinavyoelezekina makadirio ya Bajeti. Kitabu cha Kwanza ni Makadirio ya Mapato; Kitabu cha Pili ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali; Kitabu cha Tatu ni Makadirio ya Matumizi ya Kawaida kwa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; na Kitabu cha Nne ni Makadirio ya Matumizi ya Maendeleo kwa Wizara, Idara za Serikali zinazojitegemea, Taasisi na Wakala za Serikali, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, upo Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 pamoja na Muswada wa Sheria ya kuidhinisha matumizi ya Serikali wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

2.Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa napenda kumshukuru Mungu kwa baraka na amani anayoendelea kuijalia nchi yetu na pia kwa kuniruhusu kusimama hapa mbele ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka 2016/17. Aidha, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kuwa Makamu wa Rais na mwanamama wa kwanza kushika nafasi hiyo katika historia ya nchi yetu. 
 Nampongeza pia Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein, kwa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Vilevile, nampongeza Mheshimiwa Kassim M. Majaliwa kwa kuchaguliwa na wananchi wa jimbo la Ruangwa kuwa Mbunge wao na kuteuliwa na Mhe. Rais na kuthibitishwa na Bunge kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Napenda pia kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika pamoja na Naibu Spika kwa kuchaguliwa kuongoza Bunge letu Tukufu.  Kadhalika, natumia fursa hii kumpongeza Mhe. Mohamed Othman Chande, Jaji Mkuu wa Tanzania, kwa kuongoza mhimili wa Mahakama kwa weledi mkubwa.

3.Mheshimiwa Spika, niruhusu pia niwashukuru sana waheshimiwa wenza wa viongozi wetu wa kitaifa: Mama Janet Magufuli, Bwana Ameir Hafidh Ameir (mume wa Mhe. Makamu wa Rais), Mama Mwanamwema Shein, Mama Mary Majaliwa, Mama Fatuma Ramadhani Mganga (mke wa Mhe. Spika), Bwana James Andilile (mume wa Mhe. Naibu Spika) na Mama Saada El-Maamry Othman (mke wa Mhe. Jaji Mkuu) kwa kuwasaidia na kuwatunza viongozi wetu vizuri.  Asante kwenu wote na Mungu awabariki.

4.Mheshimiwa Spika, kwa mara nyingine natoa shukrani za pekee kwa Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Mbunge na Waziri wa Fedha na Mipango. Ninatambua kwamba wananchi wa Tanzania wananidai! Tarehe 29 Februari, 1968 Baba wa Taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliwasilisha hati ya madai kama ifuatavyo, nanukuu: “Tunadai nini basi kwa wale wenzetu waliojaliwa kupata elimu? Tunadai huduma kwa wananchi na huduma ambayo ukubwa wake utalingana na kiasi cha elimu waliyoipata” mwisho wa kunukuu. 

Hivyo, napenda kumuahidi tena Mhe. Rais na Watanzania kwamba nitaibeba dhamana hii kwa bidii na uadilifu ili kulipa deni langu kwa nchi yangu. Vilevile, nawapongeza waheshimiwa Wabunge wote kwa kuchaguliwa kwenu na kuwa sehemu ya Bunge hili.  Napenda pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wenzangu na Naibu Mawaziri kwa dhamana kubwa tuliyopewa na Mheshimiwa Rais kuwatumikia Watanzania. 
Nampongeza pia Dkt. Thomas Kashililah, Katibu wa Bunge na Bw. Hussein Kattanga, Mtendaji Mkuu wa Mahakama kwa kuratibu vyema shughuli za Bunge na Mahakama kwa mtiririko huo. Napenda pia kumpongeza Prof. Mussa Assad, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa kazi nzuri anayoifanya ya kukagua na kutoa taarifa za matumizi ya fedha za umma kwa wakati.

5.Mheshimiwa Spika, ninaishukuru sana Kamati ya Bunge ya Bajeti chini ya uenyekiti wake Mhe. Hawa Abdulrahman Ghasia, Mbunge wa Mtwara vijijini na Makamu Mwenyekiti Mhe. Josephat Sinkamba Kandege, Mbunge wa Kalambo, kwa kuchambua kwa kina bajeti za Mafungu yote na kutoa mapendekezo na ushauri. 
 Aidha, napenda kuwashukuru wenyeviti wa kamati za kisekta kwa ushauri na mapendekezo waliyotoa wakati wakichambua rasimu ya Bajeti hii. Ninamshukuru pia Mhe. George Mcheche Masaju (Mb), Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutayarisha kwa wakati Muswada wa Sheria ya Fedha wa mwaka 2016 na Muswada wa Sheria ya Matumizi wa mwaka 2016 ambayo ni sehemu ya Bajeti hii.

6.Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Mhe. Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji, Mbunge wa Jimbo la Kondoa kwa kuteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango na pia ninamshukuru kwa ushirikiano anaonipatia katika utekelezaji wa majukumu yangu. 
Aidha, napenda kumshukuru Dkt. Servacius B. Likwelile, Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha na Mipango kwa uratibu na usimamizi mzuri wa maandalizi ya Bajeti hii. Kadhalika, nawashukuru Naibu Makatibu Wakuu; Gavana wa Benki Kuu; Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania; Msajili wa Hazina; Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu; Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara; Wakuu wa idara, vitengo na Watumishi wote wa Wizara na taasisi zake kwa kazi kubwa waliyoifanya kukamilisha Bajeti hii.

7.Mheshimiwa Spika, Bajeti hii imezingatia mawazo na mapendekezo ya wadau mbali mbali wakiwemo wenye viwanda, wafanyabiashara na wengine wengi. Nawashukuru wote kwa mawazo na ushauri wao. Kipekee niwashukuru wajumbe wa kamati ya wataalamu na ushauri wa masuala ya kodi (Task Force) na kamati ya kitaifa ya ushauri wa kodi (Think Tank) kwa ushauri wao mzuri walionipa.

Post a Comment

Previous Post Next Post