Mbunge CCM ngangari
WAKATI bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2012/2013 ya sh trilioni
15, ikipita kwa kura 225 za ndiyo na 72 za hapana, mbunge wa Kisesa,
Luhaga Mpina (CCM), ameshikilia msimamo wake wa kuipinga na kuamua
kutoka nje ya ukumbi wakati wa kupitisha.
Mbali na Mpina wabunge wengine wawili wa CCM, Kangi Lugora (Mwibara)
na Deo Filikunjombe (Ludewa) ambao waliikosoa vikali bajeti hiyo nao
halikwepa upigaji kura kwa kutofika kabisa ukumbini.
Mpina aliikataa waziwazi bajeti hiyo mara baada ya kuwasilishwa
bungeni na hata wakati alipochangia juzi, alisema kuwa inakinzana na
Mpango wa Maendeleo wa Taifa.
Muda mfupi kabla ya upigaji kura kuanza, mawaziri William Lukuvi na
Stephen Wassira, walionekana wakihaha kumshawishi mbunge huyo bila
mafanikio.
Wakati Mpina akiwa nje na jina kutajwa mara mbili bila kuitikia,
wabunge wote wa kambi ya upinzani walimshangilia kwa kupiga makofi.
Akizungumza nje ya ukumbi wa Bunge, Mpina alisema anayo mambo mengi ya
kusema kuhusu bajeti hiyo aliyoikataa tangu awali na kusisitiza kuwa
leo ataweka wazi tena sababu za kutopiga kura katika mkutano wake na
waandishi wa habari.
Vilevile wabunge wote wa kambi ya upinzani walipiga kura ya hapana
isipokuwa mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo (UDP), pekee ndiye
aliyeunga mkono bajeti hiyo.
Pia mbunge wa kuteuliwa na Rais, James Mbatia, ambaye pia ni
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, alishangiliwa kwa nguvu na wapinzani baada
ya kuitwa jina na kusema hapana.
Akitangaza matokeo hayo, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah,
alisema: “Idadi ya wabunge inapaswa kuwa 357 lakini waliopo ni 351 na
waliopiga kura ni 297 ambapo kura za ndiyo ni 225 na hapana ni kura 72.”
Baada ya hapa Spika Makinda alitangaza kuwa waliopiga kura ya ndiyo
wameshinda na hivyo bajeti hiyo imepita, lakini akawapongeza wabunge
wote kwa pamoja akisema wamefanya kazi nzuri licha ya kusigana katika
hoja.
“Waheshimiwa wabunge nawapongeza sana kwa kazi kubwa, lakini muelewe
kuwa kutofautiana kifikra kwa Bunge kama hili si jambo baya ni kulenga
kuwatetea wale waliowatuma,” alisema.
Wakizungumza na Tanzania Daima baada ya Bunge kuahirishwa, baadhi ya
wabunge Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mbatia na Cesilia Paresso (Viti
Maalum), walisema waliikataa bajeti kwa kuwa haina jipya.
“Bajeti ni ile ile na wabunge wa CCM ni wataka maslahi wala hawako kwa ajili ya kuwatetea wananchi,” alisema Lissu.
Naye Mbatia, alisema kuwa bajeti haijafafanua mgawanyo halisi wa fedha
na kwamba serikali imeshindwa kuonyesha ni namna gani itadhibiti mapato
yanayopotea.
“Mathalan jijini Dar es Salaam, serikali inapoteza sh bil. nne
kutokana na msongamano wa magari, watu wanapoteza muda mwingi bila
kufanya kazi lakini bajeti haisemi ni hatua gani zinachukuliwa,”
alisema.
Aliongeza kuwa hata kauli ya waziri kuwa serikali inayapokea maoni ya
wapinzani kwa ajili ya kuyafanyia kazi ni hadaa inayofanyika miaka yote.
Kwa upande wake Paresso, alisema kuwa bajeti hiyo haijaeleza wazi ni
kwa namna gani serikali itawawezesha vijana kupata mikopo ili waweze
kuwekeza katika ujasiriamali.
Waziri Mgimwa anena
Mapema akijibu hoja za wabunge, Waziri Mgimwa alisema kuwa anapokea
na kuyachukua maoni ya kambi ya upinzani ili kuyafanyia kazi yale
mazuri.
Alisema kuwa kuhusu kima cha chini cha mishahara kupandishwa, hilo
litategemea kiasi cha fedha za serikali lakini akasisitiza kuwa
mishahara mipya itaanza kulipwa kuanzia mwezi ujao.
Kuhusu uhamisho wa fedha kutoka eneo moja kwenda lingine, alibainisha kuwa ni lazima Bunge lifahamu na kuidhinisha.
Pia Mgimwa aligusia kilio cha wakulima wa pamba kuondolewa kodi kwenye
viwanda vinavyotumia pamba inayozalishwa ndani akisema kuwa amepokea
hoja yao na wataichambua kisha matokeo yake yatatolewa ndani ya Bunge
wakati watakapowasilisha muswada wa fedha.
Mgimwa aliongeza kuwa katika kuwawezesha zaidi vijana wengi waendesha
bodaboda kujiajiri, serikali imekubali kupandisha tozo ya kodi ya mapato
kwenye sekta hiyo kutoka kipato cha sh milioni tatu za awali hadi hadi
nne
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment