Membe: Nikioteshwa nitagombea urais

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anamwomba Mungu amuoteshe ndoto za kuwa Rais wa Tanzania.
Membe anayetajwa mara kwa mara kuutaka urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 alisema iwapo atasikia sauti inayomsukuma kuwania urais atajitosa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa sababu urais ni wito.
Bila kumtaja mtu, Membe alisema wapo watu walioanza kushona suti wakijiandaa kwa urais wa mwaka 2015 hivyo aliwashauri kusubiri wito kutoka kwa Mungu ukiwataka kufanya hivyo.
Akizungumza jana katika kipindi cha ‘Power Breakfast’ kinachorushwa na kituo cha Redio Clouds cha jijini Dar es Salaam alisisitiza kwamba urais ni wito unaomhitaji mtu kusikia sauti ya Mungu ndani yake.
“Nikisema nitagombea urais nitapakwa matope puani na machoni hadi nitashindwa kuchukua na hizo fomu… kuna watabiri wa ajabu na uongo ambao wamezuka kuwatabiria watu.
“Hata usipoomba wanapata jina lako wanakuchukulia fomu na kukupigia kura na kukwambia wewe utapata asilimia fulani… mtu anakwambia hivyo wakati hata hujatamka wala hujachukua fomu.
“Wanamchonga rais wanampa sifa yake na kumwambia atapata asilimia fulani; sasa mnampataje mtu huyo kama hajaomba na kuweka ‘platform’ yake…
“Maana ukishapata urais unafikiria utaanzia wapi ili watu wajaji maana huwezi kwenda kwenye uwanja wa mapambano halafu ukishashinda unasema tuanzie wapi,” alisema Membe.
Mwanasiasa huyo aliwashauri wanaotaka urais mwaka 2015 kwamba huu si wakati wa kuwalaghai Watanzania wala kupita na kukusanya watu kwenye mikutano.
“Usikusanye watu wengi ukadhani wanakupenda hata…Iddi Amini alikuwa na watu wengi sana hata mimi Membe leo naweza kuita watu wengi… wingi wa watu si hoja ya kukufanya uchaguliwe.
“Nawashauri Watanzania wapime viongozi kwa kutizama nini wamefanya. Utachaguliwa kwa sera zako unazotaka kuzifanya katika kipindi cha kwanza kiuchumi.
“Waambie Watanzania kwa nini unadhani wakikuchagua utawafaa na kama wewe ni mbunge lazima upimwe na ulichokifanya kwenye jimbo lako; usiwe kasuku wa kukaa bungeni na kupiga kelele wakati jimbo lako linaoza.
“Uongozi na hasa urais ni wito, hukurupuki tu kwa sababu gazeti limekutaja lazima ujipime na uwe na watu wanaosaidia kukupima kama unafaa au hufai lakini lazima uisikie sauti ikikuita ikusukume omba… bwana…...
“Lazima sauti hiyo uipate na kama hujaisikia ile sauti usiombe lakini ukilazimisha kitakachotokea utakwenda kwa waganga au utakwenda kwa watabiri na wapo wengi halafu utadanganyika unakuja kuliangamiza taifa,” alisema Membe kwa msisitizo.
Awali alibainisha iwapo umeitwa lazima uwaambie Watanzania unachotaka kukifanya kwa kuwaeleza umaskini wao ni upi na utafanya nini kuuondoa.
“Hao wanaotaka urais hii ‘vicious cycle’ wanaikata wapi na hao wanaotaka urais lazima muwaulize kwanza… waseme kwenye bajeti hii wanataka kitu gani kikatwe, unasema bajeti mbaya ni kifungu kipi unataka tukikate na kukiweka kipi.
“Kuna mtu alisema katika Bunge hili kuna wendawazimu….., wendawazimu ni nini? Halafu akamnukuu mtu kwamba mwendawazimu ni huyo huyo anayefanya kitu kilekile kila mwaka kwa kurudia halafu huyu mtu ni mchungaji.
“Halafu Mungu anayeleta jua kila siku masika, jua na mvua naye ni mwendawazimu? Au mchungaji anayehubiri kila siku anarudia Injili ya Luka, Mathayo mwaka huu anasema na mwakani anasema ileile naye ni mwendawazimu?
“Mwendawazimu ni mtu anayeweza kutoa kauli popote bila kuheshimu watu, umri, rika bila kuheshimu mamlaka wala kumjali mtu popote pale anaropoka huyo ni mwendawazimu,” alisisitiza Membe.
Akizungumzia rada
Kuhusu mabaki ya fedha za rada waziri huyo alisema akifika bungeni atawataja wote waliohusika iwapo hawatakuwa tayari kujitaja wenyewe.
“Kuna watu wanadhani tunaficha… si jambo la siri kesi ilisikilizwa kwa miezi tisa huko Uingereza kimetoka kitabu kinaitwa The Shadow World Inside the Global Armistead kimeandikwa na Andrew Feintsan.
“Kimeeleza rushwa za BEA duniani kimetoka Machi mwaka huu kina picha zote za watu wanaohusika na rushwa na rada ya Tanzania.
“Nasubiri kama waliotajwa watashtaki au watajisema wenyewe; wasipofanya hivyo nitawasema nitakapokwenda bungeni maana humo kuna picha zao na alama ya Tanzania,” alisema Membe
Chanzo:- Tanzania daima

Post a Comment

أحدث أقدم