Mgomo wa Walimu wazidi kusambaa

Wimbi la mgomo wa walimu limeendela kutandaa katika mikoa ya Kanda ya Ziwa na sasa mkoa mpya wa Simiyu baada ya Chama Cha Walimu (CWT), wilayani Bariadi kuanza kutoa elimu ya jinsi ya kupiga kura ya kuafiki au kukataa kwa kujaza fomu namba moja inayokusudia kuwepo kwa mgomo huo mapema mwezi ujao.

Mwenyekiti wa CWT Wilaya ya Bariadi, Julius Mategemeo, jana aliiambia NIPASHE mjini Bariadi kuwa elimu ya jinsi ya kujaza fomu hizo maalum inatolewa baada ya kusambazwa kwa fomu namba moja kwa walimu wote katika shule za msingi, sekondari, vyuo na taasisi wilayani humo.

Mwenyekiti huyo alisema upigaji wa kura unalenga kuishinikiza serikali kutimiza ahadi yake na kuitaka iwaongeze mishahara walimu kwa mwezi kwa asilimia 100 na itoe posho ya kufundishia kwa walimu wanaofundisha masomo ya Sayansi kwa asilimia 55 na walimu wa masomo ya Sanaa kwa asilimia 50.

Pia kura hiyo ni pamoja na kuitka serikali itoe posho ya mazingira magumu kwa walimu wanaofanya kazi kwenye wilaya zenye mazingira magumu kwa mwezi kwa kiwango cha asilimi 30.

Katibu wa CWT Wilaya ya Bariadi, Posian Gervas, alisema Mratibu na Msimamzi wa zoezi la upigaji kura ni Mwakilishi wa Chama cha Walimu Tanzania katika shule, chuo au taasisi.

Aidha, Gervas amehimiza walimu kujitokeza kwa wingi kushiriki zoezi hilo na kupiga kura zao za siri kuafiki au kutaa kuwepo kwa mgomo huo.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Bariadi, Deogratius Hella, akizungumzia utekelezaji wa madai mbalimbali ya walimu hao, alisema katika barua yenye kumbukumbu namba E.10/34/Vol.III/10 ya Mei 29 mwaka huu alifafanua kuwa walimu 367 wa shule za msingi na 118 wa sekondari walirekebishiwa mishahara yao na kubakia 164.

Mgomo huo wa walimu unatarajiwa kuanza mwezi ujao na utahusisha walimu nchi nzima.
 
CHANZO: NIPASHE

Post a Comment

أحدث أقدم