MICHELSEN KOCHA MPYA WA VIJANA TANZANIA
Jakob Michelsen |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi leo
mbele ya waandishi wa habari kocha mpya wa timu za Taifa za vijana, Jakob
Michelsen kutoka Denmark ambaye amechukua nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi
sasa anainoa Taifa Stars.
Michelsen ambaye amepewa mkataba wa mwaka mmoja
alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na kusema falsafa yake ni
kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda wote wa mchezo.
Kabla ya kuja Tanzania, Michelsen alikuwa kocha wa timu ya
daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana leseni A ya ukocha kutoka
Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya ukocha wa vijana kutoka
Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja ya mafanikio yake ni kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya
Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri chini ya miaka 18. Ubingwa huo
aliupata msimu wa 2005/2006.
Wakati huo huo: Ruvuma imeanza vizuri michuano ya Copa
Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0 katika mchezo
wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kigoma ambayo iliifunga Lindi mabao 2-0 katika mechi ya
ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele ya Ruvuma na kuruhusu
bao katika kila kipindi.
Mabao yote ya washindi yalifungwa na mshambuliaji Edward
Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la kwanza dakika ya 34 wakati la pili
alilipachika dakika ya 84.
Katika mechi nyingine zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na
Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika mchezo uliofanyika Uwanja wa
Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es Salaam.
Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0 kwenye Uwanja wa
Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro katika mchezo
uliochezwa Uwanja wa Tamco.
Aidha, TFF itawazawadia wapiga picha za magazetini
watakaoripoti mashindano ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea
kwenye mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Mashindano hayo yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na
kushirikisha mikoa 28 yanafanyika viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya
Karume mkoani Dar es Salaam, na viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.
Zawadi ya sh. 250,000 itatolewa kwa picha bora katika maeneo
matatu; action picture, fair play picture na mpiga picha ambaye ameripoti
matukio mengi ya mashindano hayo yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya
miaka 17. Washiriki wanatakiwa kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) TFF
Post a Comment