MILOVAN AWASILI USIKU WA MANANE, KIKOSI SIMBA CHAREJEA DAR USIKU WA LEO

MILOVAN AWASILI USIKU WA MANANE, KIKOSI SIMBA CHAREJEA DAR USIKU WA LEO


Milovan Cirkovick

Na Princess Asia
WAKATI Kocha Mkuu wa Simba SC, Milovan Cirkovick amewasili alfajiri ya leo kutoka kwa Srebia alipokuwa kwa mapumziko, kikosi cha mabingwa hao wa Ligi Kuu kinapanda ndege ya ATC saa1:00 usiku wa leo mjini Mwanza, kurejea Dar es Salaam kuungana na mwalimu huyo kwa maandalizi ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Ofisa Habari wa Simba SC, Ezekiel Kamwaga ‘Mr. Liverpool’ amesema asubuhi hii kwa simu kutoka Mwanza kwamba timu ikifika itaendelea  na mzoezi Uwanja wa TCC, Chang’ombe, Dar es Salaam chini ya Profesa Milovan, aliyetua kwa ndege ya shirika la ndege la Uturuki saa 8:45 usiku wa jana.
Simba, mabingwa mara sita wa Kombe la Kagame, 1975, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002, walikuwa Kanda ya Ziwa kwa ziara ya mechi mbili za kirafiki sambamba na kutambulisha Kombe lao la ubingwa wa Ligi Kuu kwa mashabiki wao wa huko.
Katika ziara yao hiyo, Simba ilicheza mechi ya mwisho jana Uwanja wa Kambarage Shinyanga na mabingwa wa Uganda, Express ‘Tai Mwekundu’ na kutoka sare ya 1-1, baada ya juzi, kuifunga Toto Africa Uwanja wa CCM Kirumba mabao 2-0.  
Katika mchezo wa jana, kiungo mpya wa Simba SC, Kiggi Makassy aliifungia bao lake kwanza klabu hiyo, tangu ajiunge nayo mwezi huu kutoka kwa mahasimu, Yanga.
Hata hivyo, bao hilo la Kiggi lilidumu kwa dakika 20 tu, kwani dakika ya 40, Joseph Kaira aliwasawazishia Tai Wekundu na hadi kipyenga cha mwisho, timu hizo zilitoka 1-1.
Michuano ya Kombe la Kagame inatarajiwa kuanza Julai 14 hadi 29 mwaka huu, Tanzania ikiwakilishwa na timu tatu, mbali na Simba watakuwepo mabingwa watetezi wa michuano hiyo, Yanga SC na washindi wa pili wa Ligi Kuu, Azam FC.

Post a Comment

Previous Post Next Post