MISHAHARA na posho zilizotengwa na serikali kwa ajili ya wajumbe 34
wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Katiba inayoongozwa na Jaji Joseph Warioba
inatisha na imezidi kuibua mjadala miongoni mwa wabunge mjini hapa.
Kwa mujibu wa kasma ya tume hiyo iliyoko kwenye bajeti ya serikali ya
mwaka wa fedha 2012/2013, serikali imetenga sh bilioni 40 kwa tume hiyo
ambapo sh bilioni 10 zimetengwa kwa ajili ya posho ya mwaka mmoja tu.
Malipo hayo yataanza kutolewa Julai mosi hadi hapo tume hiyo inayofanya kazi nyeti nchini itakapomaliza muda wake.
Kasma hiyo inaonyesha kuwa wajumbe hao 34 watalipwa posho y ash
450,000 kwa siku ambapo ni sawa na sh milioni 13.5 kwa mwezi na kwa
mwaka kila mjumbe ataibuka na kitita cha milioni 300 wakati madereva, na
watumishi wengine wa tume wametengewa sh bilioni 4.8 na kila mfanyakazi
atalipwa posho ya sh 50,000 kila siku.
Posho ya Mwenyekiti na Makamu wake, imeongezewa fedha za viburudisho, hivyo fungu lao ni kubwa zaidi.
Gharama zingine zinazoonekana kwenye bajeti hiyo pamoja na sh milioni
250 zitakazotumika kwa ajili ya ulinzi na usalama wa ofisi za tume ni
sh milioni 10 zilizotengwa kwa ajili ya shughuli za mazishi endapo mmoja
kati ya wajumbe hao atapoteza maisha.
Mbali ya posho hiyo, kila mjumbe atapewa shangingi pamoja na nyumba ya kuishi wakati uhai wa tume hiyo ni miezi 18.
Tume hiyo inaongozwa na Mwenyekiti, Jaji Warioba, akisaidiwa na
Makamu Mwenyekiti Jaji Mkuu mstaafu, Jaji Augustino Ramadhan, ina
wajumbe 30, ikiwa ni wajumbe 15 kutoka kila moja ya pande mbili za
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Wajumbe wa tume hiyo kutoka Tanzania Bara ni Profesa Mwesiga Baregu,
Riziki Shahari Mngwali, Dk. Sengodo Mvungi, Richard Shadrack Lyimo, John
Nkolo, Alhaji Hamad Saidi El Maamry na Jesca Sydney Mkuchu.
Wajumbe wengine wa tume hiyo kutoka bara ni Profesa Palamagamba
Kabudi, Humphrey Polepole, Yahya Msulwa, Esther Mkwizu, Maria Malingumu
Kashonda, Mheshimiwa Al-Shaymaa Kwegyir, Mwantumu Jasmine Malale na
Joseph Butiku.
Wajumbe wa tume hiyo kutoka Tanzania Visiwani ni Dk. Salim Ahmed
Salim, Fatma Saidi Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Suleiman Hamad, Awadh Ali
Saidi, Ussi Khamis Haji na Salma Maulidi. Wengine kutoka Visiwani ni
Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Saidi, Muhammed Yussuf Mshamba,
Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed, Abubakar
Mohammed Ali na Ally Abdullah Ally Saleh.
Shughuli za tume hiyo zitaratibiwa na sekretarieti ambayo katibu wake
atakuwa Assaa Ahmad Rashid na Naibu Katibu atakuwa Casmir Sumba Kyuki
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment