WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anamwomba Mungu amuoteshe ndoto za kuwa Rais wa Tanzania.
Membe anayetajwa mara kwa mara kuutaka urais wa Tanzania katika
uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2015 alisema iwapo atasikia sauti
inayomsukuma kuwania urais atajitosa kwenye kinyang’anyiro hicho kwa
sababu urais ni wito.
Bila kumtaja mtu, Membe alisema wapo watu walioanza kushona suti
wakijiandaa kwa urais wa mwaka 2015 hivyo aliwashauri kusubiri wito
kutoka kwa Mungu ukiwataka kufanya hivyo.
Akizungumza jana katika kipindi cha ‘Power Breakfast’ kinachorushwa na
kituo cha Redio Clouds cha jijini Dar es Salaam alisisitiza kwamba
urais ni wito unaomhitaji mtu kusikia sauti ya Mungu ndani yake.
“Nikisema nitagombea urais nitapakwa matope puani na machoni hadi
nitashindwa kuchukua na hizo fomu… kuna watabiri wa ajabu na uongo ambao
wamezuka kuwatabiria watu.
“Hata usipoomba wanapata jina lako wanakuchukulia fomu na kukupigia
kura na kukwambia wewe utapata asilimia fulani… mtu anakwambia hivyo
wakati hata hujatamka wala hujachukua fomu.
“Wanamchonga rais wanampa sifa yake na kumwambia atapata asilimia
fulani; sasa mnampataje mtu huyo kama hajaomba na kuweka ‘platform’
yake…
“Maana ukishapata urais unafikiria utaanzia wapi ili watu wajaji
maana huwezi kwenda kwenye uwanja wa mapambano halafu ukishashinda
unasema tuanzie wapi,” alisema Membe.
Mwanasiasa huyo aliwashauri wanaotaka urais mwaka 2015 kwamba huu si
wakati wa kuwalaghai Watanzania wala kupita na kukusanya watu kwenye
mikutano.
“Usikusanye watu wengi ukadhani wanakupenda hata…Iddi Amini alikuwa na
watu wengi sana hata mimi Membe leo naweza kuita watu wengi… wingi wa
watu si hoja ya kukufanya uchaguliwe.
“Nawashauri Watanzania wapime viongozi kwa kutizama nini wamefanya.
Utachaguliwa kwa sera zako unazotaka kuzifanya katika kipindi cha kwanza
kiuchumi.
“Waambie Watanzania kwa nini unadhani wakikuchagua utawafaa na kama
wewe ni mbunge lazima upimwe na ulichokifanya kwenye jimbo lako; usiwe
kasuku wa kukaa bungeni na kupiga kelele wakati jimbo lako linaoza.
“Uongozi na hasa urais ni wito, hukurupuki tu kwa sababu gazeti
limekutaja lazima ujipime na uwe na watu wanaosaidia kukupima kama
unafaa au hufai lakini lazima uisikie sauti ikikuita ikusukume omba…
bwana…...
“Lazima sauti hiyo uipate na kama hujaisikia ile sauti usiombe lakini
ukilazimisha kitakachotokea utakwenda kwa waganga au utakwenda kwa
watabiri na wapo wengi halafu utadanganyika unakuja kuliangamiza taifa,”
alisema Membe kwa msisitizo.
Awali alibainisha iwapo umeitwa lazima uwaambie Watanzania unachotaka
kukifanya kwa kuwaeleza umaskini wao ni upi na utafanya nini kuuondoa.
“Hao wanaotaka urais hii ‘vicious cycle’ wanaikata wapi na hao
wanaotaka urais lazima muwaulize kwanza… waseme kwenye bajeti hii
wanataka kitu gani kikatwe, unasema bajeti mbaya ni kifungu kipi unataka
tukikate na kukiweka kipi.
“Kuna mtu alisema katika Bunge hili kuna wendawazimu….., wendawazimu
ni nini? Halafu akamnukuu mtu kwamba mwendawazimu ni huyo huyo
anayefanya kitu kilekile kila mwaka kwa kurudia halafu huyu mtu ni
mchungaji.
“Halafu Mungu anayeleta jua kila siku masika, jua na mvua naye ni
mwendawazimu? Au mchungaji anayehubiri kila siku anarudia Injili ya
Luka, Mathayo mwaka huu anasema na mwakani anasema ileile naye ni
mwendawazimu?
“Mwendawazimu ni mtu anayeweza kutoa kauli popote bila kuheshimu watu,
umri, rika bila kuheshimu mamlaka wala kumjali mtu popote pale
anaropoka huyo ni mwendawazimu,” alisisitiza Membe.
Akizungumzia rada
Kuhusu mabaki ya fedha za rada waziri huyo alisema akifika bungeni
atawataja wote waliohusika iwapo hawatakuwa tayari kujitaja wenyewe.
“Kuna watu wanadhani tunaficha… si jambo la siri kesi ilisikilizwa kwa
miezi tisa huko Uingereza kimetoka kitabu kinaitwa The Shadow World
Inside the Global Armistead kimeandikwa na Andrew Feintsan.
“Kimeeleza rushwa za BEA duniani kimetoka Machi mwaka huu kina picha zote za watu wanaohusika na rushwa na rada ya Tanzania.
“Nasubiri kama waliotajwa watashtaki au watajisema wenyewe;
wasipofanya hivyo nitawasema nitakapokwenda bungeni maana humo kuna
picha zao na alama ya Tanzania,” alisema Membe
Chanzo:- Tanzania daima
Post a Comment