Kipigo cha Ulimboka chamtesa
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda kwa mara nyingine tena jana katika hali
isiyotarajiwa na wengi, aliyumba na kushindwa kutoa tamko zito kuhusu
mgomo wa madaktari kinyume na alivyokuwa ameahidi mbele ya Bunge juzi
mjini Dodoma.
Pamoja na kushindwa kwake, Pinda pia alijikuta katika wakati mgumu
kuelezea ukweli wa kile kinachodaiwa kuhusika kwa serikali katika tukio
la kutekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya kwa kiongozi wa Jumuiya ya
Madaktari Nchini, Steven Ulimboka.
Akijibu swali la Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
(CHADEMA), katika kipindi cha maswali na majibu kwa Waziri Mkuu, ambaye
alitaka kujua hatua ya serikali ya kutotoa tamko wakati juzi alitoa
kauli nzito ya ‘liwalo na liwe’ kuhusu mgomo wa madaktari na kuibua
hofu kubwa kwa wananchi, serikali inalieleza nini taifa kuhusu hali hiyo
na inafanya nini kumaliza mgomo huo.
Akijibu swali hilo, Pinda kwanza alikiri kuahidi kutoa tamko la
serikali akitumia neno la “liwalo na liwe’, lakini akadai kuwa serikali
haitaweza kutoa tamko hilo tena baada ya kupata ushauri wa kisheria kwa
kuwa jambo hilo liko mahakamani.
“Kwa bahati mbaya sana kauli yangu ya ‘liwalo na liwe’ imetafsiriwa
kwa namna tofauti. Hata dada yangu Halima Mdee nilimsikia akitilia shaka
kauli hiyo na kuhusisha na tukio la kutekwa kwa Dk. Ulimboka.
“Nilichoaminisha ni kwamba hili jambo liko mahakamani, lakini
tungetolea tamko la serikali bila kujali kwamba suala hilo liko
mahakamani; ndiyo maana nikasema liwalo na liwe.’
Alisema baada ya mashauriano na wataalamu wa serikali jana usiku
waliona si vyema kuendelea na tamko hilo hadi kesi iliyopo mahakamani
itakapomalizika.
Kuhusu tukio la kutekwa, kupigwa kwa Ulimboka, Waziri Mkuu Pinda
alisema serikali imeguswa na kushtushwa na tukio hilo, na akadai kuwa
amesikitishwa na kuwepo kwa taarifa zinazoituhumu serikali kuhusika na
unyama huo.
Waziri Mkuu aliliambia Bunge kuwa madai hayo ya kuituhumu serikali
yanashangaza kwa sababu, yeye mwenyewe alipata taarifa ya kufanyiwa
vitendo hivyo akiwa bungeni na hata wakati alipoahidi kutoa tamko la
serikali hakuwa anajua chochote.
“Dk. Ulimboka tumekuwa naye kwenye vikao vya ndani vya majadiliano,
tuko naye mahakamani. Leo serikali ihusike kumteka, kumpiga na kumtesa
kwa kiasi kile ili iweje?”
Alisema Waziri wa Mambo ya Ndani, Emmanuel Nchimbi, ameshatoa kauli
juu ya tukio hilo, hivyo alisisitiza kuwa serikali itafanya uchunguzi wa
kina kuwanasa waliohusika.
Akijibu swali la nyongeza la Mbowe aliyetaka kujua hatua za dharula
zilizochukuliwa na serikali kumaliza mgomo huo hasa baada ya kusitisha
tamko lake Bungeni, Pinda alisema serikali itaendelea na majadiliano na
madaktari hao ili kufikia muafaka.
“Hatua nyingine ya dharura tuliyochukua serikali ni kuzungumza na
Hospitali ya Lugalo na zingine ndogo kubeba jukumu hilo kwa sasa, pia
tumeagiza madaktari wastaafu wote warejee kazini katika kipindi hiki cha
mgomo,” alisema Pinda.
Lissu amtaka ajiuzulu
Majibu ya Pinda yalimkoroga Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu,
aliyesimama na kumuuliza sababu gani zinazomfanya aendelee kushikilia
wadhifa wake huku akitambua kuwa ameshindwa kumaliza mgogoro huo.
“Mheshimiwa Waziri Mkuu, Februari mwaka huu wakati wa mgomo wa
madaktari uliahidi kwamba mgomo huo hautatokea tena, leo mgomo umerudi
tena, je, kwa nini usijiuzulu?” alihoji Lissu.
Pinda alidai kuwa tangu kuanza kwa mgogoro huo, amefanya jitihada za
kutosha kujaribu kuunusuru na kwamba anaamini amefanya kazi kubwa
kuufikisha hapo ulipo.
Hata hivyo, Lissu alisimama na kumwambia Waziri Mkuu, kwamba hapo
alipoufikisha ni pabaya zaidi na haoni sababu ya yeye kuendelea kuwepo
madarakani, kauli iliyoonekana kumkera Pinda ambaye alidai kuwa yapo
mambo ambayo yanaweza kumfanya akajiuzulu, lakini sio katika sakata la
mgomo wa madaktari.
“Mheshimiwa Lissu hii sio lugha nzuri ya kusema, nakuheshimu sana,” alisema Pinda na kuzima swali hilo.
Naye Mbunge wa Viti Maalum, Martha Mlacha (CCM), alihoji endapo
serikali inajua kama kuna kikundi cha watu kinachochochea mgomo huo kwa
kuwapa fedha. Akijibu hoja hiyo, Pinda alikiri kupata taarifa hizo na
akadai kuwa serikali inafanya uchunguzi kubaini ukweli, ikiwa ni kweli
wahusika watachukuliwa hatua.
Juzi Pinda aliahidi kutoa kauli ya serikali wakati akijibu mwongozo
Mbunge wa Mbozi Mashariki, Godfrey Dhambi (CCM), aliyetaka kujua msimamo
kuhusu mgomo wa madaktari.
Madaktari waikataa Tume ya Polisi
Jumuiya ya Madaktari Nchini imesema haina imani na tume iliyoundwa na
Jeshi la Polisi kwa ajili ya kuchunguza unyama aliofanyiwa Dk. Ulimboka
huku wakisisitiza kuwepo kwa chombo huru zaidi.
Licha ya kutaka tume huru, madaktari hao wamesema wataendelea na
msimamo wao wa kuhakikisha wanatetea maslai yao pamoja na mazingira
magumu ya kufanyia kazi yanayowakabili kwa sasa.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya jengo la MOI Katibu wa
Jumuiya hiyo Dk. Edwin Chitage alisema madaktari nchini wanahitaji
chombo kilicho huru kitakachochunguza tukio hilo kwa undani zaidi kuliko
Jeshi la Polisi.
Alisema hawana imani na tume hiyo kwa sababu si huru; wanataka chombo
kitakachopatikana kwa utaratibu unaoeleweka, kuliko polisi hasa
wakizingatia mazingira ya kutekwa na kupigwa kwa mwenzao ingawa hawawezi
kusema kama jeshi la polisi linahusika.
“Tutaendelea kupigania masuala ya mazingira bora ya kazi kwani
hatufurahii kuona msongamano wa wagonjwa wodini, mgonjwa akilala chini,
watoto wachanga kulala zaidi ya watano kitanda kimoja na kukosekana kwa
dawa na vifaatiba,” alisema.
Awali aliwataka madaktari wote nchini kuwa watulivu hasa katika
kipindi hiki kigumu na kusisitiza kwamba tukio hilo limewaimarisha na
kuwazidishia mshikamano.
Afya ya Ulimboka yaimarika
Hali ya afya ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini Dk. Steven
Ulimboka inaendelea kuimarika licha ya maumivu makali yanayomkabili.
Akizungumza kwa taabu na waandishi wa habari kwenye chumba cha
wagonjwa mahututi kwenye Kitengo cha Mifupa (MOI) Dk. Ulimboka alisema,
“Namshukuru Mungu naendelea vizuri tofauti na nilivyofikishwa hapa
jana…bado nina maumivu makali naomba kama kuna watu wanataka kuja
kuniona wasije ili nipumzike,” alisema.
Awali Ofisa Uhusiano wa MOI Jumaa Almas alisema hali ya Dk. Ulimboka
inaendelea vizuri tofauti na alivyoletwa juzi asubuhi kwa kuwa sasa ana
uwezo wa kutambua watu wanaofika kumjulia hali na kuzungumza kidogo.
Almas alisema madaktari wameshauri mgonjwa huyo kupumzika na kutaka
idadi ya watu wanaofika kumjulia hali mgonjwa huyo ipungue ili
kumwepusha na maambukizi zaidi.
“Kwa sasa hali yake ni nzuri na yuko chini ya uangalizi wa jopo la
madaktari linaloongozwa na Profesa Joseph Kahamba,” alisema.
Kuhusu mgomo katika kitengo hicho Almas alisema ni huduma za dharura
pekee zinazotolewa huku zile za kawaida zikiwa hazifanyiki kabisa.
Dk. Ulimboka alifikishwa hospitalini hapo baada ya kutekwa na watu
wasiojulikana kisha kumpiga, kujeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili wake
na kutupwa kwenye msitu wa Pande, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Mwenyekiti huyo ambaye amekuwa akiratibu mgomo ya madaktari
unaoendelea, aliokotwa na msamaria mwema akiwa amefungwa mikono akiwa
amejeruhiwa vibaya.
Vyama vyaendelea kulaani
Kutoka mkoani Mwanza, Sitta Tumma anaripoti kuwa Chama cha
Wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na
Utafiti nchini (RAAWU), Kanda ya Ziwa, kimelaani vikali kitendo cha
kinyama cha kupigwa na kuumizwa vibaya, alichofanyiwa Dk. Steven
Ulimboka, na kuelekeza tuhuma hizo kwa serikali.
RAAWU imesema, ushahidi wa mazingira unaonyesha dhahiri kwamba
serikali imehusika kwa namna moja au nyingine kumdhuru kiongozi huyo wa
madaktari nchini, ikiwa ni lengo la kutaka kuzima mgomo wa madaktari
unaoendelea katika kudai maslahi na huduma bora ya matibabu kwa
Watanzania.
Katibu wa RAAWU Kanda ya Ziwa, Ramadhan Mwendwa, ameiambia Tanzania
Daima ofisini kwake kuwa kuna haja ya serikali kujisafisha kwa sababu
mazingira ya tukio hilo yanaiweka katika hali ya kutuhumiwa.
Mwendwa ambaye pia ni Katibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Nchini (TUCTA), Mkoa wa Mwanza, alizidi kudai kuwa manyanyaso na
ukandamizwaji mkubwa unaofanywa na serikali vinaonyesha wazi kwamba
viongozi wa Tanzania wanawapeleka wananchi wao katika machafuko.
“Tusifike huko kama nchi nyingine zinavyopigana. Viongozi wa
wafanyakazi tuweni wamoja na wafanyakazi wote katika kutetea maslahi ya
taifa. Tusirudi nyuma,” alisema Mwendwa.
CUF, CHADEMA wanena
VYAMA vya CUF na CHADEMA, vimelaani kitendo cha kutekwa na kupigwa
kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka, huku
vikiitaka serikali kuunda tume huru ya uchunguzi.
Mkurugenzi wa Mafunzo na Oganaizesheni wa CHADEMA, Benson Kigaila,
alisema kuwa kitendo hicho ni jitihada za serikali kuwanyamazisha
watetezi wa maslahi ya umma.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, alisema hizo ni dalili za wazi
za serikali ya CCM kushindwa kuhimili demokrasia ya wengine.
“Tumeshuhudia hali hii ikiwakumba wengi, kumbukeni tukio la mhariri wa
Mwanahalisi Sued Kubenea kumwagiwa tindikali, mauaji ya Masudi Mbwana
kule Igunga na hata kuuawa kwa mwenyekiti wa CHADEMA kule Arumeru ni
katika njia za kutaka kuwanyamazisha na kuwatisha wengine,” alisema
Kigaila.
Alisema katika mgomo wa kwanza wa madaktari Rais Jakaya Kikwete
aliuhakikishia umma kuwa watayashughulikia matataizo ya madaktari na
kwamba suala la mgomo kwao litakuwa ni ndoto.
Kwa upande wao CUF, kwa mujibu wa wa Naibu Mkurugenzi wa Itikadi na
Uenezi, Abdul Kambaya, walilitaka jeshi la polisi kuacha kuchunguza
tukio hilo kutokana na kutolitilia maanani tangu awali lilipopewa
taarifa.
Akizungumza jana na Tanzania Daima, alisema kuwa kitendo
alichofanyiwa Dk. Ulimboka ni aibu kwa taifa kwa kushindwa
kufanya ulinzi wa viongozi na watu wake.
Alisema uchunguzi huo wa tukio unatakiwa kufanywa na taasisi
zingine huru ili kutoa majibu sahihi kwa wananchi lakini si jeshi la
polisi.
“Serikali haiwezi kujitoa katika tukio hili la kinyama alilofanyiwa
Dk. Ulimboka hasa ukizingatia ni katika kipindi kifupi ambacho madaktari
wako kwenye mgomo na huyu ni kiongozi wao,” alisema Kambaya
Chanzo:- http://www.freemedia.co.tz
Post a Comment