MAHAKAMA Kuu Kanda ya Dar Es Salaam leo inatarajiwa kusikiliza utata wa umri wa msanii wa fani ya filamu nchini Elizabeth Michael maarufu kama Lulu, anayekabiliwa na kesi ya mauaji.
Hatua hiyo inalenga
kubaini umri halali wa mshtakiwa huyo, baada ya kuwepo kwa mvutano baina
ya mawakili wanaomtetea wakidai kuwa bado ni mtoto, na upande wa
mashtaka (Jamhuri) unaodai kuwa ni mtu mzima.
Lulu anakabiliwa na
kesi ya mauaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu akituhumiwa kumuua
msanii mwenzake, Steven Kanumba aliyefariki dunia nyumbnani kwake
Sinza, April 7, 2012.
Hata hivyo umri wake umezua utata baada ya
mawakili wanaomtetea kuomba kesi yake isikilizwe katika Mahakama ya
Watoto (Juvenile Court) wakidai kuwa bado ni mtoto kwa kuwa ana umri wa
miaka 17 na si 18 kama hati ya mashtaka inavyoonyesha.
Lakini
Mahakama ya Kisutu iliyakataa maombi hayo ikisema kuwa haina nguvu ya
kisheria kuyashughulikia kulingana na mazingira ya kesi hiyo na hivyo
kushauri maombi hayo yawasilishwe Mahakama Kuu.
Mei 15 mawakili
hao waliwasilisha maombi hayo Mahakama Kuu kwanza wakiiomba Mahakama
hiyo itamke kuwa Mahakama ya Kisutu ilikosea kuyakataa maombi hayo
wakidai kuwa wanaamini mahakama hiyo ilikuwa na uwezo wa
kuyashughulikia.
Pia waliiomba Mahakama Kuu kama itaridhika kuwa
Mahakama ya Kisutu haikuwa na uwezo basi Mahakama Kuu yenyewe ifanye
uchunguzi wa umri halali wa mshtakiwa huyo na iagize mwenendo wa kesi
hiyo katika Mahakama ya Kisutu usimame hadi suala umri litakapoamriwa.
Mahakama
Kuu katika uamuzi wake Juni 11, 2012 kwanza ilisema kuwa Mahakama ya
Kisutu ilikosea kuyakataa maombi hayo kwa kuwa inayo mamlaka ya kisheria
kuyashughulikia.
Hata hivyo katika uamuzi huo Jaji Dk. Fauz Twaib
alisema kuwa maombi hayo yaliwasilishwa kwake bila kufuata vifungu
sahihi vya kisheria, lakini akakubali kuyashughulikia kulingana na
unyeti na uzito wa mashtaka katika kesi hiyo .
Hivyo aliziagiza
pande zote katika kesi hiyo (waombaji yaani Lulu kupitia kwa mawakili
wake) na wajibu maombi (Jamhuri)kuwasilisha mahakamani hapo ushahidi na
vielelezo watakavyovitumia katika hoja zao na kupanga kuyakiliza maombi
hayo leo.
Jopo la Mawakili wanaomtetea Lulu linaundwa na Mawakili
Kennedy Fungamtama(kiongozi wa jopo), Makamu wa Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) Peter Kibatala na Fulgence Massawe kutoka
Kituo cha Msaada wa Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC).
Kwa upande wa Jamhuri unawakilishwa na Mawakili wa Serikali, Elizabeth Kaganda na Shadrack Kimaro.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kunatarajiwa kuibuka kwa mvutano mkali wa kisheria baina ya pande husika kutokana na kila upande kuwasilisha mahakamani vielelezo vinavyoonesha mshtakiwa huyo kuwa na umri tofauti.
Wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo kunatarajiwa kuibuka kwa mvutano mkali wa kisheria baina ya pande husika kutokana na kila upande kuwasilisha mahakamani vielelezo vinavyoonesha mshtakiwa huyo kuwa na umri tofauti.
Wakati
vielelezo vya upande wa muombaji vikionyesha kuwa mshtakiwa huyo ana
umri wa miaka 17, vielelezo ya upande wa mashtaka navyo vinaonesha kuwa
mshtakiwa huyo ana umri wa zaidi ya miaka 18 yaani miaka 21.
Vielelezo
vya upande wa maombi ni pamoja na viapo vya wazazi wa mshtakiwa huyo
mama yake Lucresia Augustin Kalugila, mkazi wa Dar es Salaam na baba
mzazi Michael Kimemeta, mkazi wa Moshi, cheti cha kuzaliwa na cha
ubatizo vya mshtakiwa.
Vielelezo vilivyowasilishwa na upande wa
mjibu maombi ni pamoja na Mkanda wa video aina ya CD, yenye mahojiano
kati ya mshtakiwa huyo na mtangazaji wa kituo kimoja cha runinga nchini.
Vingine
ni maelezo ya mshtakiwa huyo aliyoyatoa polisi wakati alipohojiwa
kuhusiana na tuhuma zinazomkabili, maombi ya hati ya kusafiria
(Passport) na maombi ya leseni ya udereva, pamoja na hati ya kiapo
kinzani (counter affidavit) kilichoapwa na Wakili Kimaro.
Viapo
vyote wazazi wa mshtakiwa, cheti cha kuzaliwa na cha ubatizo vya
mshtakiwa vinaeleza kuwa mshtakiwa huyo alizaliwa April 16, 1995 katika
kituo cha Afya Muhimbili na kupewa cheti cha kuzaliwa namba B.0318479
cha Julai 23, 2004.
Pia viapo hivyo vinaeleza kuwa baada ya
kuzaliwa mshtakiwa mama yake alimpa jina la Diana Michael Kimemeta,
lakini alimpeleka mtoto huyo Moshi mkoani Kilimanjaro kwa ndugu zake,
walimpa jina la Elizabeth, jina la bibi yake Elizabeth Shikana.
Viapo
hivyo vinaendelea kueleza kuwa baada ya majadiliano wote, yeye mama,
baba na ndugu wengine walikubaliana kuwa wamuite Diana Elizabeth Michael
Kimemeta .
“ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika Kanisa la Katoliki Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa
“ Elizabeth Michael Kimemeta alibatizwa katika Kanisa la Katoliki Chang’ombe Septemba 28, 1997 na alichukua majina ya ubatizo Diana Elizabeth Michael Kimemeta;” inasomeka sehemu nyingine ya kiapo hicho cha mama wa mshtakiwa
Chanzo Mwananchi gazeti
Post a Comment