Kocha wa Serengeti Boys, Jakob Michelsen |
Na Boniface Wambura
TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti
Boys inaendelea vizuri na kambi ya mazoezi mkoani Mbeya ambapo tayari imecheza
mechi moja ya kujipima nguvu.
Ilicheza mechi hiyo jana (Septemba 8 mwaka huu) dhidi ya
Tanzania Prisons iliyoko Ligi Kuu ya Vodacom kwenye mji wa Nakonde ulioko
mpakani mwa Tanzania na Zambia. Timu hizo zilitoka sare ya 1-1 huku bao la
Serengeti Boys likifungwa na Miraji Selemani.
Serengeti Boys leo jioni (Septemba 9 mwaka huu) inatarajia
kucheza mechi nyingine wilayani Mbozi dhidi ya Mbozi United. Itacheza mechi ya
tatu Jumanne (Septemba 11 mwaka huu) jijini Mbeya dhidi ya timu ya daraja la
kwanza ya Mbeya City.
Kwa mujibu wa Kocha wa timu hiyo, Jakob Michelsen kambi hiyo
inaendelea vizuri, na anatarajia kupata mechi moja ya kirafiki ya kimataifa
kabla ya kucheza mechi ya mashindano na Misri, Oktoba 13 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Wakati huo huo: Kozi ya wakufunzi wa waamuzi (Futuro III
Refereeing Course) ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) inaanza
kesho (Septemba 10 mwaka huu) jijini Dar es Salaam.
Jumla ya washiriki katika kozi hiyo itakayoanza saa 3 asubuhi
kwenye hoteli ya Holiday Inn ambao wanatoka katika nchi 21 za Afrika ni 69.
Kozi hiyo inayotarajiwa kumalizika Septemba 22 mwaka huu inafanyika katika
maeneo mawili ya ufundi (technical) na utimamu wa mwili (fitness).
Nchi washiriki ni Afrika Kusini, Botswana, Eritrea, Ethiopia,
Gambia, Ghana, Kenya, Lesotho, Liberia, Malawi, Mauritius, Namibia, Nigeria,
Seychelles, Sierra Leone, Somalia, Swaziland, Tanzania, Uganda, Zambia na
Zimbabwe.
Washiriki kutoka Tanzania kwenye kozi hiyo ni Joan Minja,
Leslie Liunda na Soud Abdi (technical) na Riziki Majalla (fitness).
Baadhi ya wakufunzi wa kozi hiyo wanaotoka FIFA na Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) ni Carlos Henriques anatoka Afrika Kusini,
Fernando Gracia (Hispania), Steve Bennett (Uingereza), Tarek Bouchamaoui
(Tunisia), James Sekajugo (Uganda), Bester Kalombo (Malawi), Felix Tangawarima
(Zimbabwe) na An-Yan Lim Kee Chong (Mauritius).
Kozi hiyo itafunguliwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Leodegar Tenga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la
Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), mjumbe wa Kamati ya
Utendaji ya CAF na mjumbe wa Kamati ya Vyama (Associations Committee) ya FIFA.
Aidha, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linatoa pongezi kwa
uongozi mpya wa Chama cha Soka Iringa (IRFA) uliochaguliwa katika uchaguzi
uliofanyika jana (Septemba 9 mwaka huu) mjini Iringa.
Ushindi waliopata viongozi waliochaguliwa kuongoza chama
hicho unaonesha jinsi wajumbe wa Mkutano Mkuu wa IRFA walivyo na imani kubwa
kwao katika kusimamia mchezo huo mkoani Iringa.
TFF inaahidi kuendeleza ushirikiano wake kwa Kamati ya
Utendaji ya IRFA chini ya uenyekiti wa Cyprian Kuyava ambaye amechaguliwa
kuongoza chama hicho kwa mara ya kwanza.
Uongozi huo mpya una changamoto nyingi, kubwa ikiwa ni
kuhakikisha unaendesha shughuli za mpira wa miguu mkoani Iringa kwa kuzingatia
katiba ya IRFA pamoja na vyombo vya mpira wa miguu vilivyo juu yake.
Pia tunatoa pongezi kwa Kamati ya Uchaguzi ya IRFA na Kamati
ya Uchaguzi ya TFF kwa kuhakikisha uchaguzi huo unaendeshwa kwa mujibu wa
kanuni za uchaguzi za wanachama wa TFF.
Viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi huo ni Cyprian Kuyava
(Mwenyekiti), Stanford Mwakasala (Makamu Mwenyekiti), Eliud Mvella (Katibu) na
John Ambwene (Katibu Msaidizi).
Wengine ni Ramadhan Mahano (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF),
Coaster Magoloso (Mwakilishi wa Klabu TFF), Abdallah Kiyumbo (Mhazini), wakati
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Maulid Tofi na David Mwamalekela.
(Wambura ni Ofisa Habar wa TFF)
Post a Comment