SIMBA KUJIONDOA LIGI KUU KISA YONDANI NA TWITE?

Mwandishi wa habari za michezo Shaffih Dauda ameripoti kwamba Siku moja baada ya kamati ya sheria, maadili, na hadhi za wachezaji ya TFF kutoa maamuzi juu ya mapingamzi ya Simba dhidi ya wachezaji Kelvin Yondani na Mbuyu Twitte kuichezea klabu Yanga – kwa kuwaidhinisha wachezaji hao kuichezea Yanga. Leo hii klabu ya Simba imesema inafikiria hatua za kuchukua juu ya uamuzi huo wa kamati ya Alex Mgongolwa.
Kwa taarifa za kuaminika alizozipata Shaffih kutoka ndani ya uongozi wa Simba ni kwamba kamati ya utendaji ya klabu hiyo itakutana usiku wa leo kujadili hatua za kuchukua huku baadhi ya wajumbe wakisema kutokana na uonevu wanaotendewa na TFF itabidi wajitoe kushiriki kwenye ligi kuu kwa sababu hawana imani na shirikisho hilo.
Simba inalalamika kwamba wachezaji wote wawili Mbuyu Twitte na Kelvin Yondan wamesajiliwa na Yanga isivyo halali. Kwa upande wa Twitte walitaka walipwe fedha zao $32,000 walizompa mchezaji huyo na akasaini nao mkataba kabla ya Yanga kuwazidi kete na kumsainisha mkataba mpya beki huyo aliyekuwa akiichezea APR ya Rwanda, na pia walitaka Twitte afungiwe kwa sababu alisaini mkataba na kalbu zote mbili kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Kwa upande wa Yondani Simba wanadai mchezaji huyo ni halali yao kwa sababu bado ana mkataba na klabu hiyo, pia wakataka Yanga iadhibiwe kwa kitendo cha kufanya mazungumzo na mchezaji ambaye bado ana mkataba na klabu yake ya zamani lakini jana kamati ya sheria, maadili, na hadhi za wachezaji ya TFF ikatoa maamuzi ya kuwaidhinisha Twite na Kelvin Yondan kwenda Yanga, maamuzi ambayo Simba wamesema sio sahihi.
Source: www.shaffihdauda.com

Post a Comment

Previous Post Next Post