Kaimu
mkurugenzi wa Idara ya Kinga wa Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii Bw.
Elias Chanamo (katikati) akitoa ripoti kwa waandishi wa habari juu ya
utafiti kuhusu maambukizi ya Ukimwi miongoni mwa wanawake wanaofanya
biashara ya ngono jijini Dar es salaam leo. Picha na Aron Msigwa – MAELEZO.
Na Aron Msigwa – MAELEZO.
Dar es salaam.
……………………………….
Watanzania wametakiwa kujiepusha na vitendo vinavyochangia kueneza Ugonjwa wa Ukimwi kufuatia matokeo ya utafiti wa kibiolojia na kitabia uliofanywa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi ( NACP) kuonyesha kuwa maambukizo ya ugonjwa huo kwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono jijini Dar es salaam yapo juu kwa asilimia 31.4.
Kauli hiyo imetilewa leo jijini Dar es salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kinga, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii Bw. Eliasi Chinamo wakati akifungua mkutano wa kuwasilisha ripoti ya utafiti ya mwaka 2009/2010 kuhusu maambukizi ya Ukimwi miongoni mwa wanawake wanaofanya biashara ya ngono jijini Dar es salaam.
Amesema kiwango hicho cha maambukizi kwa mujibu wa matokeo ya utafiti huo kinaenda sambamba na ongezeko la magonjwa mengine yakiwemo Kaswende ambayo ni 2.0%, Gonorea 10.5% , Pangusa 6.3% na Trakoma ya via vya uzazi ambayo ni 15% na kukifanya kiwango hicho kufikia asilimia 31.4 ikilinganishwa na asilimia 10.4 ya kiwango cha maambukizi kwa wanawake wote wa mkoa huo.
Amesema wanawake waliohusishwa katika utafiti huo jijini Dar es salaam umri wao ulikua kati ya miaka 15 – 50 na kuongeza kuwa shughuli nzima ya utafiti iliwahusisha wanawake 7500.
Kuhusu mazingira yaliyosababisha maambukizo miongoni mwa wanawake hao Bw. Chinamo amesema kuwa wengi wao wamekuwa wakifanya biashara hiyo na wateja tofauti tofauti bila kuchukua tahadhari yoyote, matumizi ya madawa ya kulevya kwa kujidunga sindano na matumizi ya pamoja na vitendo vya mashambulio ya mwili na kulazimishwa kufanya ngono.
“Wanawake wanaofanya biashara ya ngono wametaarifu kuwa na wateja wa aina tofauti takribani robo tatu ambayo ni sawa na asilimia 72.6 na wengi wao wametaarifu kuwa na wastani wa wateja watatu kwa siku ya mwisho kabla ya kufanyiwa usaili” amesema.
Aidha amesema kufuatia matokeo hayo kutokua mazuri katika jiji la Dar es salaam juhudi mbalimbali zinaendelea kufanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya VVU pamoja na kuandaa mkakati wa kuongeza na kuimarisha huduma za ushauri nasaha , upimaji wa VVU pamoja na huduma za kliniki za tiba na mafuzo.
Kwa upande wake mkuu wa Shirika la Kimarekani la Kudhibiti Maradhi na Kinga nchini (CDC) Dkt. Mary Kibona ameeleza kuwa shirika la CDC litaendelea kuwafikia watu walio katika mazingira hatarishi ya kupata maambukizi ya VVU na kuendelea kusaidia tafiti mbalimbali zinazohusisha makundi mbalimbali nchini Tanzania
Amesema kuna kazi kubwa ya kuwafikia watu wengi wanaohitaji kusaidiwa na ambao bado hawajapata huduma hizi katika maeneo mbalimbali nchini na kupongeza juhudi za serikali za kuhakikisha kuwa asilimia kubwa ya watanzania wanapata huduma bora za afya.
Naye Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi (NACP) Dkt. Robert Mwanzi amefafanua kuwa juhudi mbalimbali zinaendelea kufanyika kuhakikisha kuwa elimu ya kupunguza maambukizi ya VVU inatolewa kwa wananchi wote na kusisitiza kuwa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi unashirikiana na wadau mbalimbali katika kukabiliana na janga la Ukimwi nchini.
Ametoa wito kwa watanzania kuifanyia kazi elimu ya kupambana
na maambukizi ya VVU inayotolewa na kusisitiza kuwa elimu kuhusu na
namna ya kupambana na maambukizi ya VVU itaendelea kutolewa kupitia
makundi nchi nzima.
إرسال تعليق