SIMBA SC imetoa sare ya pili mfululizo katika Ligi Kuu hya
Vodacom Tanzania Bara, baada ya kutoka 2-2 na Kagera Sugar jioni hii kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 18 na kuendelea kuongoza
Ligi Kuu, kutokana na Azam FC kulazimishwa sare ya bila kufungana na Prisons
kwenye Uwanja wa Sokoine mjini Mbeya.
Hadi mapumziko, Simba SC walikuwa mbele kwa bao 1-0,
lililotiwa kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Zambia, Felix Mumba Sunzu
Jr. dakika ya nane, akiunganisha kwa kichwa krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’
kutoka wingi ya kulia.
Kwa ujumla kipindi cha kwanza timu zote zilishambuliana kwa
zamu, ingawa ni Simba walioonekana kufanya mashambulizi ‘yenye akili’ zaidi.
Kipindi cha pili Simba ilirudi na moto tena na katika dakika
ya 51, Mrisho Khalfan Ngassa aliifungia timu hiyo bao la pili kwa shuti kali
lililowababatiza mabeki wa timu hiyo na kutinga nyavuni.
Hilo lilikuwa bao la tatu kwa Ngassa tangu ajiunge na Simba
katika mechi tisa alizoichezea timu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.
Baada ya hapo, Kagera walizinduka na kuanza kulishambulia
lango la Simba kupitia pembeni na katika dakika ya 64 Themi Felix aliunganisha kwa
kichwa krosi ya George Kavilla na kuifungia Kagera bao la kwanza.
Bao liliwazindua Kagera, ambao waliongeza kasi ya
kulishambulia lango la Simba na katika dakika ya 66, Juma Nyosso alimkwatua
kwenye eneo la hatari Paul Ngwai na Salum Kanoni akaenda kumtungua Juma Kaseja,
akiisawazishia Kagera.
Baada ya hapo timu zilianza kushambuliana kwa zamu na mpira
ulinoga zaidi kutokana na mashambulizi ya pande zote mbili.
Katika mechi nyingine, Mgambo imeshinda mechi ya tatu
mfululizo, baada ya kuifunga Toto African 2-0 kwenye Uwanja wa Mkwakwani,
Tanga. JKT Ruvu imezinduka baada ya kuifunga Polisi Morogoro 2-0 kwenye Uwanja
wa Jamhuri, Morogoro na JKT Oljoro imetoka 0-0 na African Lyon.
Simba SC; Juma Kaseja (Nahodha), Nassor Masoud ‘Chollo’/Uhuru
Suleiman, Amir Maftah, Paschal Ochieng, Juma Nyosso, Mwinyi Kazimoto/Edward Christopher,
Amri Kiemba, Haruna Moshi/Jonas Mkude, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho
Ngassa.
Kagera Sugar; Andrew Ntala, Salum Kanoni, Martin Muganyizi, Amandus
Nesta (Nahodha), Benjamin Effe/Themi Felix, Malegesi Mwangwa, Daudi Jumanne/Kamana
Salum, George Kavilla, Shijja Mkinna, Enyinna Darlington na Wilfred Ammeh/Paul
Nwai.
Katika mchezo wa awali, Simba B iliifunga Moro United mabao
3-0 katika mchezo wa utangulizi kabla ya mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara kati ya Simba na Kagera Sugar, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Simba B inayofundishwa na Suleiman Matola,
akisaidiwa na Amri Said ‘Stam’ yalipatikana yote kipindi cha pili, wafungaji
Ramadhan Salum dakika ya 65 na 70 na Miraj Athumani dakika ya 85. Moro United inajiandaa na Ligi Daraja la
Kwanza, inayotarajiwa kuanza Oktoba 24, mwaka huu.
Post a Comment