TAARIFA YA SERIKALI KUHUSU VURUGU ZILIZOTOKEA LEO HUKO ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao kama kawaida na kwamba vyombo vya ulinzi na usalama vimedhibiti hali ya ulinzi na imeimarishwa katika maeneo yote ya Zanzibar.
 
Taarifa ya Serikali iliyotolewa leo usiku na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohammed Aboud Mohammed imesema Zanzibar bado ni shwari na inaendelea kuwa katika hali ya amani na utulivu.
 
Akizungumzia tukio la vurugu zilizofanywa na wananchi wachache, Waziri Mohamed Aboud alisema vikundi vya vijana vinavyosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vurugu hizo katika mitaa ya Darajani,Michenzani,Muembeladu,Magomeni,Amani wakidai Sheikh wao haonekani na kudhani amekamatwa na vyombo vya Dola na kuwekwa ndani.

Waziri Mohamed Abud alisema Serikali imewasiliana na vyombo vya Dola ikiwemo Polisi,Jeshi la wananchi wa Tanzania, Idara ya Usalama wa Taifa, Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,KMKM,JKU,Chuo cha Mafunzo,Zimamoto na Valantia ambapo vyombo vyote hivyo vimeeleza kutoelewa chochote kuhusu Sheikh Farid.
 
Waziri huyo alisema kwamba Jeshi la Polisi limepokea taarifa ya kutoonekana kwa Sheikh Farid ambapo kwa sasa Jeshi hilo linaendelea kumtafuta na kufanya uchunguzi juu ya tukio hilo ili kupata ukweli wake na kuchukua hatua zinazofaa.
 
Alisema kwamba wakati Jeshi la Polisi likiendelea na upelelezi wake, wananchi wameombwa kutoa taarifa kuhusu tukio hilo kwa vituo vya Polisi au kupitia Masheha, Ofisi za Wilaya na Mikoa katika maeneo yao.
 
Waziri Mohamed Aboud amesema Serikali inawasihi wananchi waache kujiingiza katika vitendo vya fujo na vurugu kwani kutenda hivyo ni kosa kwa mujibu wa sheria na Serikali haitovumilia vitendo hivyo.
 
Katika tukio la  mchana, vijana hao wanaosadikiwa kuwa ni wafuasi wa Sheikh Farid Hadi walifanya vitendo vya vurugu ikiwemo kuchoma moto Maskazini za CCM,kuvunja maduka,kupora mali za watu na kuharibu miundombinu ya barabara na kusababisha hasara kubwa.
 
IMETOLEWA NA:
IDARA YA HABARI(MAELEZO) ZANZIBAR
17/10/2012
ZANZIBAR,TANZANIA

Post a Comment

أحدث أقدم