Rais
Jakaya Mrisho Kikwete akiwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Bole jijini Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 23, 2013 kuhudhuria
utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na
Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).(PICHA NA
IKULU).
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete
amewasili Addis Ababa, Ethiopia, leo Februari 23, 2013 kuhudhuria
utiwaji saini Mpango wa Umoja wa Mataifa wa Amani, Usalama na
Ushirikiano katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mpango
huo unatarajiwa kutiwa saini kesho Februari 24, 2013 na Wakuu wa Nchi
kutoka Ukanda wa Maziwa Makuu, ikiwa ni pamoja na Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Jamhuri ya Uganda, Jamhuri ya Afrika ya
Kati, Jamhuri ya Angola, Jamhuri ya Burundi, Jamhuri ya Kongo
(Brazaville), Jamhuri ya Zambia, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja
na Jamhuri ya Afrika Kusini.
Aidha,
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. Ban Ki Moon, Mwenyekiti wa
Kamisheni ya Umoja wa Mataifa, Dkt. Nkosazana Dlamini-Zuma, pamoja na
wenyeviti wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Ukanda
wa Maziwa Makuu (ICGLR) watatia saini Mpango huo kama mashahidi na
wadhamini.
Mpango
huo una nia ya kuchangia juhudi ambazo zimefanywa na Ukanda wa Maziwa
Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika
kutafuta amani Mashariki ya Kongo na ukanda wote wa Maziwa Makuu kwa
ujumla.
Mpango
huo pia umetilia maanani mapendekezo muhimu yaliyokubalika baada ya
mashauriano kati ya wakuu wa nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Katibu Mkuu wa Umoja
wa Mataifa.
Imetolewa na:
Muhidin Issa Michuzi,
Mwandishi wa Habari wa Rais, Msaidizi,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
23 Februari, 2013
إرسال تعليق