Wagombea wa urais wa Kenya wanapaswa
kufanya mdahalo wa pili siku ya Jumatatu (tarehe 25 Februari) kwa
Kiswahili ili raia wote waweze kuelewa, wanazuoni na raia wasema.
|
Na Rajab Ramah, Nairobi
Wagombea wa urais wa Kenya wanapaswa kufanya mdahalo wa pili siku ya
Jumatatu (tarehe 25 Februari) kwa Kiswahili ili raia wote waweze
kuelewa, wanazuoni na raia wasema.
Profesa Clara Momanyi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki
alisema Chakita, asasi anayoiongoza ambayo inahamasisha Kiswahili nchini
Kenya, imeandika barua kwa waandaaji wa mdahalo ikiwataka kubadilisha
lugha kuwa ya Kiswahili, lugha inayozungumzwa kwa sehemu kubwa nchini
Kenya.
Lugha zote mbili Kiswahili na Kiingereza zimeorodheshwa katika katiba ya
Kenya kama lugha rasmi, lakini ni Wakenya waliopitia mfumo rasmi wa
elimu tu ambao wanajifunza na kuongea Kiingereza.
"Uchaguzi wa kutumia Kiingereza kwa mdahalo wote wa [tarehe 11 Februari]
ulikuwa wa kupendelea upande mmoja," Momanyi aliiambia Sabahi. "Inaweka
kando sehemu kubwa ya Wakenya ambao hawajui [Kiingereza]. Hii ni aina
ya ubaguzi ambao ni kinyume na katiba yetu ambayo inatoa uhakikisho wa
uhuru kwa raia wote wa kutotendewa isivyo halali kwa kuegemea lugha au
ukabila."
"Kwa hiyo tunataka mdahalo unaokuja watangazaji waulize maswali kwa
Kiswahili na wagombea wa urais wajibu kwa kutumia lugha hiyo hiyo,"
alisema.
Wachira Waruru, mkurugenzi mkuu wa Royal Media Services na mwenyekiti wa
kamati ya mdahalo wa urais, alisema wasiozungumza Kiingereza wana
malalamiko ya kweli.
"Wakenya wengi waliofuatilia mdahalo katika redio zao na televisheni wanaweza kuwa hawakuelewa kutokana na kikwazo cha lugha," aliiambia Sabahi. "Tulipokea malalamiko kutoka kwa wasomi na tunatafuta njia za kushirikiana na timu ya maandalizi kuhusu jinsi ya kujumuisha lugha ya Kiswahili kwenye mdahalo."
Kuondoa vikwazo vya lugha
Peter Otieno, mwenye umri wa miaka 39, dereva wa taksi wa kitongoji ya
Westlands mjini Nairobi, aliiambia Sabahi hakuridhika na mdahalo wa
kwanza.
"Niliusubiri mdahalo kwa hamu kwa sababu [nilifikiria] nitapata taarifa
zaidi kuhusu wagombea urais na wana faida gani kwa Kenya," alisema
Otieno, ambaye hakuwahi kuenda shule. "Lakini nilipowasha redio ya gari
langu kusikiliza mdahalo, nilikatishwa tamaa kwamba kwa saa tatu zote,
sikuweza kuelewa kilichokuwa kikijadiliwa kwa sababu sielewi
Kiingereza."
Alisema ilibidi awategemee rafiki zake ambao "wanaielewa lugha kidogo" kumueleza kilichokuwa kinajadiliwa kwenye mdahalo.
"Hii ndiyo maana napenda duru ya pili ifanyike kwa Kiswahili ili nipate taarifa moja kwa moja," Otieno alisema.
Salome Nduku, anayefanya kazi na Google Kenya kama mtaalamu wa lugha,
aliiambia Sabahi Wakenya wengi wanakabiliwa na matatizo yanayofanana
kuhusu vyombo vya habari vya kijamii.
Nduku, ambaye hutafsiri ujumbe wa Kiswahili kwa Kiingereza, alisema
Google ilifuatilia taarifa zinazotumwa katika vyombo vya habari vya
kijamii baada ya mdahalo wa kwanza na kugundua kwamba "Wakenya wengi
wanataka [kufuatilia] mdahalo unaofanyika kwa Kiswahili ili waweze
kuelewa".
Kithakawa Mbiera, mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi,
alisema mdahalo wa urais unawakilisha fursa pekee ya Wakenya wengi
kujifunza masuala muhimu kuhusiana na ardhi na kugawana rasilimali na
kupima wagombea wa ofisi.
"Wanasiasa wanahutubia umma kwa Kiswahili [katika mikusanyiko ya
kampeni] kwasababu wanakiri ukweli kwamba Wakenya wengi hawaelewi
Kiingereza," alisema Mbiera, akiongeza kwamba lugha hiyo hiyo inapaswa
kutumika katika mdahalo.
Alisema kwamba kushindwa kutumia Kiswahili katika majukwaa maarufu kama
hayo kutasababisha kupotea kwa utambulisho na umoja wa Wakenya.
"Tuko jinsi tulivyo kwa sababu ya lugha tunayoongea, ambayo ni
Kiswahili, ambayo tunaitumia katika makabila mbalimbali kama nyenzo ya
mawasiliano. Kwa hivyo, mdahalo kama ule unapaswa kuipa kipaumbele kama
alama ya utaifa na umoja wetu," alisema.
Chanzo: sabahionline.com
Post a Comment