Wakenya watoa wito kwa waaandaji wa mdahalo wa pili wa urais kutumia Kiswahili

Wagombea wa urais wa Kenya wanapaswa kufanya mdahalo wa pili siku ya Jumatatu (tarehe 25 Februari) kwa Kiswahili ili raia wote waweze kuelewa, wanazuoni na raia wasema.

Na Rajab Ramah, Nairobi

Wagombea wa urais wa Kenya wanapaswa kufanya mdahalo wa pili siku ya Jumatatu (tarehe 25 Februari) kwa Kiswahili ili raia wote waweze kuelewa, wanazuoni na raia wasema.


Profesa Clara Momanyi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki alisema Chakita, asasi anayoiongoza ambayo inahamasisha Kiswahili nchini Kenya, imeandika barua kwa waandaaji wa mdahalo ikiwataka kubadilisha lugha kuwa ya Kiswahili, lugha inayozungumzwa kwa sehemu kubwa nchini Kenya.

Lugha zote mbili Kiswahili na Kiingereza zimeorodheshwa katika katiba ya Kenya kama lugha rasmi, lakini ni Wakenya waliopitia mfumo rasmi wa elimu tu ambao wanajifunza na kuongea Kiingereza.

"Uchaguzi wa kutumia Kiingereza kwa mdahalo wote wa [tarehe 11 Februari] ulikuwa wa kupendelea upande mmoja," Momanyi aliiambia Sabahi. "Inaweka kando sehemu kubwa ya Wakenya ambao hawajui [Kiingereza]. Hii ni aina ya ubaguzi ambao ni kinyume na katiba yetu ambayo inatoa uhakikisho wa uhuru kwa raia wote wa kutotendewa isivyo halali kwa kuegemea lugha au ukabila."

"Kwa hiyo tunataka mdahalo unaokuja watangazaji waulize maswali kwa Kiswahili na wagombea wa urais wajibu kwa kutumia lugha hiyo hiyo," alisema.

Wachira Waruru, mkurugenzi mkuu wa Royal Media Services na mwenyekiti wa kamati ya mdahalo wa urais, alisema wasiozungumza Kiingereza wana malalamiko ya kweli.

"Wakenya wengi waliofuatilia mdahalo katika redio zao na televisheni wanaweza kuwa hawakuelewa kutokana na kikwazo cha lugha," aliiambia Sabahi. "Tulipokea malalamiko kutoka kwa wasomi na tunatafuta njia za kushirikiana na timu ya maandalizi kuhusu jinsi ya kujumuisha lugha ya Kiswahili kwenye mdahalo."


Kuondoa vikwazo vya lugha
Peter Otieno, mwenye umri wa miaka 39, dereva wa taksi wa kitongoji ya Westlands mjini Nairobi, aliiambia Sabahi hakuridhika na mdahalo wa kwanza.

"Niliusubiri mdahalo kwa hamu kwa sababu [nilifikiria] nitapata taarifa zaidi kuhusu wagombea urais na wana faida gani kwa Kenya," alisema Otieno, ambaye hakuwahi kuenda shule. "Lakini nilipowasha redio ya gari langu kusikiliza mdahalo, nilikatishwa tamaa kwamba kwa saa tatu zote, sikuweza kuelewa kilichokuwa kikijadiliwa kwa sababu sielewi Kiingereza."

Alisema ilibidi awategemee rafiki zake ambao "wanaielewa lugha kidogo" kumueleza kilichokuwa kinajadiliwa kwenye mdahalo.

"Hii ndiyo maana napenda duru ya pili ifanyike kwa Kiswahili ili nipate taarifa moja kwa moja," Otieno alisema.

Salome Nduku, anayefanya kazi na Google Kenya kama mtaalamu wa lugha, aliiambia Sabahi Wakenya wengi wanakabiliwa na matatizo yanayofanana kuhusu vyombo vya habari vya kijamii.

Nduku, ambaye hutafsiri ujumbe wa Kiswahili kwa Kiingereza, alisema Google ilifuatilia taarifa zinazotumwa katika vyombo vya habari vya kijamii baada ya mdahalo wa kwanza na kugundua kwamba "Wakenya wengi wanataka [kufuatilia] mdahalo unaofanyika kwa Kiswahili ili waweze kuelewa".

Kithakawa Mbiera, mhadhiri wa Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Nairobi, alisema mdahalo wa urais unawakilisha fursa pekee ya Wakenya wengi kujifunza masuala muhimu kuhusiana na ardhi na kugawana rasilimali na kupima wagombea wa ofisi.

"Wanasiasa wanahutubia umma kwa Kiswahili [katika mikusanyiko ya kampeni] kwasababu wanakiri ukweli kwamba Wakenya wengi hawaelewi Kiingereza," alisema Mbiera, akiongeza kwamba lugha hiyo hiyo inapaswa kutumika katika mdahalo.

Alisema kwamba kushindwa kutumia Kiswahili katika majukwaa maarufu kama hayo kutasababisha kupotea kwa utambulisho na umoja wa Wakenya.

"Tuko jinsi tulivyo kwa sababu ya lugha tunayoongea, ambayo ni Kiswahili, ambayo tunaitumia katika makabila mbalimbali kama nyenzo ya mawasiliano. Kwa hivyo, mdahalo kama ule unapaswa kuipa kipaumbele kama alama ya utaifa na umoja wetu," alisema.

Post a Comment

أحدث أقدم