Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Dodoma jana, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akizungumzia kuhusu adhabu za wabunge watano wa chama chake kupewa adhabu kwa utovu wa nidhamu, amekiri kuwa mmoja wa wabunge wa chama chake, walidharau mamlaka ya Spika lakini kanuni zilizotumika hazikustahili na zilikuwa kiini macho.
Alisema Naibu Spika, Job Ndugai, hakustahili kutumia kanuni hizo za kifungu cha 2.2 na 5 za Bunge toleo la mwaka 2013, ambazo zinamtaka Spika atoe uamuzi kuhusu jambo litakalotokea bungeni endapo katika kanuni zilizopo hazina Mwongozo.
“Ukweli ni kwamba vurugu zilizotokea bungeni na kitendo cha mbunge wetu Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Tundu Lissu kinachodaiwa kuwa amedharau mamlaka ya kiti, kanuni zake zipo pamoja na adhabu yake,” alisema.
Alisema katika kanuni hizo za Bunge, vifungu 74 na 76 zimebainisha wazi adhabu zinazotakiwa kutolewa kwa mbunge atakayebainika kudharau mamlaka ya Spika au kuwa chanzo cha vurugu ndani ya Bunge.
“Ni kweli hakuna shaka kabisa Mbunge wetu alidharau mamlaka ya Spika, lakini zipo adhabu stahiki za kushughulikia suala hilo, na kwa namna kanuni hizo zilivyo kama zingetumika vizuri, huenda adhabu ingekuwa kubwa zaidi ya hii iliyotolewa, huku akiongeza kuwa wabunge hao walioadhibiwa hawakupewa haki ya kusikilizwa,” alisisitiza.
Adhabu hizo ni pamoja na Spika kutaja jina la Mbunge husika hadharani kuwa amedharau kiti na kumpeleka mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka na Bunge na kwa upande wa fujo zinapotokea ndani ya ukumbi huo wa Bunge, kabla ya kutoa hoja ya nguvu, hutakiwa kwanza kuahirisha Bunge.
“Siku ile kweli vurugu zilitokea na kulikuwepo na vitendo vya kudharau mamlaka ya Spika, lakini Naibu Spika alitakiwa kwanza aahirishe Bunge, ndipo atumie nguvu, sasa badala yake waliingia askari wa kila aina ndani ya ukumbi jambo ambalo ni kinyume na Kanuni za Bunge,” alisisitiza.
Aidha, alisema kuhusu suala la adhabu kwa mbunge anayedharau kiti au kuhusika na vurugu, hutakiwa kwanza Spika amfikishe mbunge husika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ambayo baada ya kushauriana ndipo hutoa adhabu ambayo ni kutohudhuria Bunge vikao 10 iwapo kosa ni la kwanza na vikao 20 iwapo kosa ni la pili.
“Adhabu yoyote inayotolewa bungeni hutolewa kwanza na Azimio la Bunge na si Spika mwenyewe, endapo kanuni zilizopo zingefuatwa, huenda wahusika kama wangethibitika kabisa kuwa wamekosa, wangepata adhabu kali zaidi kama zilivyoainishwa kwenye kanuni,” alisema Mbowe.
Wabunge wa CHADEMA walioadhibiwa kutokana na vurugu zilizotokea bungeni humo hivi karibuni pamoja na Lissu, ni Ezekiah Wenje (Nyamagana), Highness Kiwia (Ilemela), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Peter Msigwa (Iringa Mjini).
---
via HabariLeo
إرسال تعليق