Shambulio lililotekelezwa katika ubalozi wa Ufaransa nchini Libya, 23 April 2013
Mlipuko wa bomu umetokea mapema jumanne hii katika ubalozi wa Ufaransa
mjini Tripoli nchini Libya. Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP,
tukio hilo limesababisha uharibifu mkubwa wa majengo ya ubalozi huo na
kuwajeruhi walinzi wawili waliokuwapo katika eneo hilo.
Rais wa Ufaransa Francois Hollande amesema mamlaka za nchini Libya
inapaswa kueleza kwa kina kuhusu shambulio hilo na kuhakikisha wahusika
wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Wizara ya mambo ya
nje ya Libya imelaani shambulizi hilo na kuliita ni la kigaidi.
Waziri wa mambo ya nje wa Libya Mohammed Abdel Aziz ameiambia AFP kuwa
serikali yake inalaani shambulio hilo ambalo limetekelezwa katika ofisi
za Taifa ambalo liliisaidia nchi hiyo kufanikisha harakati za kuangushwa
kwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Moamer Ghaddafi.
Shambulio la jumanne hii ni la kwanza kutekelezwa katika ofisi za kigeni
za nchini humo kwa mwaka huu, tukio la mwisho ni lile la kushambuliwa
kwa ubalozi wa Marekani mjini Benghazi mwezi septemba mwaka jana ambalo
lilisababisha vifo vya raia wanne wa Marekani akiwamo aliyekuwa balozi
wa Marekani katika nchi hiyo Christopher Stevens.
Tangu kuangushwa kwa utawala wa Ghaddafi nchi hiyo imeendelea kukumbwa
matukio ya kukosekana kwa usalama suala ambalo limechangia raia wengi wa
kigeni kuondoka katika nchi hiyo. Via kiswahili.rfi.fr
إرسال تعليق