Na Flora Martin Mwano
Israel na Palestina watakutana tena katika kipindi cha miezi miwili
ijayo kuendeleza jitihada za kusaka suluhu ya mzozo wao uliodumu kwa
muda mrefu.
Mpatanishi wa mgogoro wa Israel na
Pelestina, John Kerry (katikati) akiwa na wawakilishi wa pande zote
jijini Washington. REUTERS/Jonathan Ernst
Mpatanishi wa mzozo huo Waziri Mkuu wa mambo ya nje wa Marekani John
Kerry amesema mkutano ujao wa wawakilishi wa pande hizo utafanyika
nchini Israel au Palestina kutokana na watakavyokubaliana.
Akiongea baada ya kumalizika kwa siku mbili za mazungumzo jijini
Washington, Kerry ameeleza kuwa pande zote zimejidhatiti katika kujadili
maswala muhimu ili kupata suluhu inayokusudiwa.
Kerry amesema ingawa changamoto ni kubwa lakini huu ni wakati muafaka
kwa majirani hao kupatana baada ya kuzozana kwa kipindi kirefu.
Awali Rais wa Marekani, Barack Obama alikutana na wajumbe wa Israel na
Palestina wanaoshiriki mazungumzi hayo, Isarel inawakilishwa na Waziri
wake wa Sheria Tzipi Livni na Palestina inawakilishwa na Saeb Erekat.
Mara baada ya kumalizika kwa kikao cha kwanza, Mjumbe wa Israel Livni ameeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya mchakato huo.
Katika kipindi cha miezi mitano iliyopita, Kerry amefanya ziara sita
tofauti katika eneo la Mashariki ya Kati akihimiza pande zote kukubali
kurejea katika mazungumzo hayo ambayo yaliyovunjika mwezi Septemba mwaka
2010.
Via kiswahili.rfi.fr
إرسال تعليق