Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete na Waziri Mkuu wa Thailand, Yingluck
Shinawatra leo, Jumanne, Julai 30, 2013 wameshuhudia utiaji saini mikataba
minne ya kuimarisha ushirikiano na uhusiano kati ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao wawili wameshuhudia
utiaji saini huo katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam mchana
wa leo ikiwa sehemu ya shughuli za Mheshimiwa Shinawatra katika Tanzania wakati
wa ziara yake ya siku tatu nchini.
Mikataba ambayo viongozi hao
wameshuhudiwa ikitiwa saini ni pamoja na ule wa kubadilisha wafungwa uliotiwa
na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Silima Pereira kwa niaba
ya Tanzania na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Thailand,
Mheshimiwa Surapong Tovichachakul,.
Mikataba mingine ni mkataba wa Kuimarisha
na Kulinda Uwekezaji (Promotion and
Protection of Investments) na mkabata wa Ushirikiano katika Masuala ya
Ufundi iliyotiwa saini na Mheshimiwa Tovichachakul na Waziri wa Fedha wa
Tanzania, Mheshimiwa William Mgimwa.
Mkataba wa nne kutiwa saini ni
Makubaliano kati ya Wizara ya Nishati na Madini na Chuo cha Madini cha Thailand
kwa niaba ya Wizara ya Biashara ya Thailand uliotiwa saini na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Madini Bwana Eliakim Maswi na Mkurugenzi Mkuu wa Chuo cha Madini cha
Thailand Bi. Prom Sawatwatthanakul.
Mapema leo Waziri Mkuu wa Thailand
ambaye aliwasli nchini akitokea Mozambique katika ziara yake ya nchi tatu za
Afrika amepokelewa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA)
na pia akalakiwa Ikulu, Dar Es Salaam na mwenyeji wake Rais Kikwete.
Viongozi hao wamekutana na kufanya
mazungumzo ya faragha na baadaye kufanya mazungumzo rasmi ya Kiserikali kati ya
Sserikali hizo mbili.
Kubwa ambalo limekubaliwa katika
mazungumzo hayo ni umuhimu wa nchi hizi mbili kuimarisha uhusiano na
ushirikiano kati yao kwa manufaa ya wananchi wa Tanzania na Thailand.
Baadaye viongozi hao wawili wamekwenda
kwenye Hoteli ya Hyatt Regency-Kilimanjaro mjini Dar Es Salaam ambako
Mheshimiwa Shinawatra ametangaza Mpango Mpya wa Ushirikiano kati ya Afrika na
Thailand.
Mama huyo ameuambia mkutano huo wa
maofisa wa Serikali, wafanyabiashara wa sekta binafsi, wasomi, mabalozi na
wanadiplomasia pamoja na wawakilishi wa taasisi zisizokuwa za Kiserikali kuwa
Mpango huo una misingi yake katika ushirikiano wa Nchi Zinazoendelea za Kusini (South-South Cooperation).
Chini ya Mpango huo, Thailand
itaitisha mkutano wa kwanza wa wakuu wa nchi za Afrika na Thailand mwanzoni mwa
mwaka ujao na amemwalika Rais Kikwete kuhudhuria mkutano huo wenye nia ya
kujenga mahusiano ya karibu zaidi kati ya Afrika na Thailand.
“Kwa kutilia maanani usawa wa ujuzi wa
jitihada za maendeleo nchi za Afrika na Thailand, nchi yangu itaongeza kasi ya
mahusiano ya maendeleo na Afrika katika maeneo ambako uhusiano huo unaweza
kuongeza faida kwa pande zote mbili, kwa jamii zetu na watu wetu hasa katika
sekta za kilimo, afya, elimu na maendeleo ya watu kwa jumla.”
Ameongeza mama huyo: “Wakati
huo huo, Thailand inatangaza leo kuanzishwa kwa Mpango wa Wanathailand
Kujitolea ambako wataalam wa Thailand watafanya kazi na wenzao wa Afrika katika
nchi za Afrika kwenye miradi iliyoko chini ya ushirikiano wa kiufundi.”
Baadaye leo, Waziri Mkuu Shinawatra
atahudhuria dhifa ya kitaifa ambayo imeandaliwa kwa heshima yake na Rais
Kikwete na itakayofanyika Ikulu, Dar Es Salaam.
Kesho,
Waziri Mkuu huyo atakwenda kwenye Mbunga ya Taifa ya Serengeti ambako atakutana
na maofisa wa Wizara ya Maliasili na Utalii watakaomwelezea hali halisi,
changamoto na umuhimu wa kulinda mbunga za wanyama. Aidha, akiwa Serengeti,
mama huyo atashuhudia utiaji saini wa Makubaliano ya Kushirikiana Katika
Kulinda Hifadhi na Wanyamapori kati ya Serikali za Tanzania na Thailand, ikiwa
ni pamoja na kushirikiana katika kupambana dhidi ya ujangili.
Mama huyo atarejea Dar Es Salaam
keshokutwa kumalizia ziara yake na kuondoka kurejea nyumbani.
Imetolewa na:
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar
es Salaam.
30
Julai, 2013
إرسال تعليق