Leo Nimesaini Hati Ya Makubaliano Na Kutimiza Moja Ya Ndoto Zangu.



Ndugu zangu,

Asubuhi ya leo, kwa nafasi yangu kama Mkurugenzi Mtendaji wa Jumuiya ya Karibu Tanzania Association ( KTA), nimesaini hati ya Makubaliano ( MoU) ya ushirikiano wa miaka minne, kati ya KTA na TEWW ( Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima). Kwa upande wa TEWW, hati hiyo imesainiwa na Mkurugenzi wa TEWW, Dr. Fidelice Mafumiko.

Ushirikiano wetu, mbali ya maeneo mengine, utakuwa ni kwenye kuendesha kozi ya masafa ya diploma kwa wakufunzi wa Vyuo Vya Maendeleo ya Wananchi hapa nchini, na baadae kwa walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kwa kushirikiana na Chama Cha Walimu Tanzania, TTU. Kwa hapa nchini kuna vyuo vipatavyo 55 vya Maendeleo ya Wananchi.

Tukio la leo linatimiza moja ya ndoto zangu za kuona watu wazima walio makazini na hususan walimu, wakijiendeleza kwa njia ya masafa na kutumia vituo vyao vya kazi kama sehemu ya kufanyia mazoezi kwa maarifa mapya wanayoyapata. Binafsi nilishiriki kuanzisha wazo la kozi hii.

Hatua itakayofuata sasa ni kuanzisha kozi ya masafa kwa ngazi ya Certificate kwa walio makazini. Vile vile, kuona kuwa programu tunayoiendesha KTA ya ' Mama Course' kwa maana ya akina dada waliokatishwa masomo yao kwa sababu ya uja uzito, kuwa nayo inaingizwa kwenye ushirikiano huu na hivyo kuwawezesha wasichana hao kumalizia masomo yao ya sekondari kwa kushirikiana na Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima.

Pichani nikitia saini hati hiyo na kwa kuongozwa na Mkuu wa Idara ya Elimu ya Masafa, TEWW, Bw. Baraka Kiwonyaki. Kwangu ni moja ya kumbukumbu njema katika kuitumikia jamii.

Siku Njema.
Maggid,
http://www.kaributanzania.or.tz/

Post a Comment

أحدث أقدم