Ndugu zangu,
Moja ya jambo nililotaka kulisema ni hili la vyama vya siasa na utaratibu wa kujiundia vikundi au vikosi vya ulinzi.Naamini tulifanya makosa makubwa kama taifa tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi 1992 bila kufanya mabadiliko ya kimsingi kwenye katiba yetu.
Ilipaswa pia kuwekwa wazi kuwa vyama vya siasa kwenye mfumo wa vyama vingi havitakiwi kuunda vikosi au vikundi vyake vya ulinzi. Kazi ya ulinzi na usalama iachwe kwa polisi na vyombo vingine vya usalama vyenye kutambulika na visivyo na sura za kiitikadi.
Nilishauri vyama hivi vya siasa viachane na ujima huu wa kuwa na vikundi vya ulinzi. Nikaonyesha hofu yangu kuwa vyama hivi vya siasa vinataka kuturudisha nyuma miaka 50. Kuturudisha kwenye ujima. Kwamba kwa tulipofikia sasa msajili wa vyama na hata katiba yetu ijayo ipige marufuku ya vyama kuwa na vikundi vya ulinzi.
Maana, haya ya ' Blue guards, green guards, red brigade na sijui yellow guards ni mambo ya ' kijima' yasiyotakiwa kuwepo katika wakati tulio nao. Iliwezekana katika mfumo wa chama kimoja. Sasa leo itakuwaje pale mtaani kukawepo na ' chipukizi' wa CCM, Chadema, CUF , NCCR ...Jamani tuwaache watoto wetu waishi katika kufurahia utoto wao. Hayo ya ukakamavu watafundishwa mashuleni, mgambo na JKT.
Tukianza sasa kuwapandikiza watoto wetu mbegu za chuki na kubaguana tutakuwa tunachangia kuharakisha kazi ya kuliangamiza taifa letu wenyewe.Nikatoa pia mfano wa kongamano la chuo kikuu majuzi kuhusu amani; kwamba sikuwaona vijana wengi pale Nkrumah Hall.
Badala ya vyama kupoteza muda na rasilimali kufyeka mapori ya kuwaweka vijana kwenye makambi ya ukakamavu kiukweli wanachohitaji vijana wetu kwa sasa ni ' ukakamavu wa akili'. Na mahali kama pale Nkrumah Hall kwenye makongamano ndipo tungeweza kuwanoa vijana wetu kuwa na uwezo wa kujenga hoja na kubomoa hoja za wengine.
Hayo ni machache, niliongea mengine pia...
Maggid
إرسال تعليق