Uchochoro wa kuvusha dawa za kulevya Dar huu hapa
RIPOTI MAALUMU
*Ni Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
*Matajiri wauteka, waharibu mfumo wa ukaguzi
MFUMO wa ukaguzi wa wasafiri na mizigo yao katika
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA) umetekwa na sasa uko mikononi mwa
matajiri na wanasiasa wanaofanya biashara ya dawa za kulevya hapa nchini.
Vyanzo vya habari vya kuaminika vilivyo ndani ya
serikali vinavyofanya kazi bega kwa bega na dawati
la habari za siasa na uchunguzi vimedokeza kuwa,
baadhi ya watoto wa viongozi wakuu wa nchi,
wafanyabiashara wenye ukwasi wa kutisha na wanasiasa wenye utajiri ambao umekuwa ukitiliwa
shaka kwa muda mrefu, wamebainika kuingilia
mfumo wa kiitelejensia wa JNIA kwa kuupandikizia
watu ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa
maelekezo yao.
Ripoti ya uchunguzi wa kikachero iliyo mikononi
mwa maofisa wa juu serikalini na ambayo
waliinukuu katika mazunguzo yao na gazeti hili,
inaeleza kuwa mtandao wa matajiri wauza dawa za
kulevya umewaondoa wafanyakazi kadhaa watiifu
waliokuwa katika kitengo cha ukaguzi wa abiria na mizigo cha JNIA na kupachika watu wao walio
kwenye mfumo wa malipo wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Sambamba na hilo, walieleza kuwa kitengo cha
kupambana na biashara ya dawa za kulevya nchini
kimedhoofishwa na hata mbwa wa polisi waliokuwa
wakitumika kukagua mizigo ya wasafiri wanaotumia
uwanja wa JNIA wameondolewa katika mfumo wa
ukaguzi na sasa watumika kwa nadra, hasa zinapovujishwa taarifa za usafirishaji wa dawa za
kulevya ambazo hutolewa aghalabu
wafanyabiashara hao wanapohitilafia na kibiashara na kuamua kuumbuana.
Taarifa hizi zimethibitishwa na kauli ya Mkurugenzi wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Kamishna
Mwandamizi wa Polisi (SACP) Godfrey Nzowa,
ambaye katika mahojiano yake, alieleza kuwa
mtandao wa wafanyabiashara wa dawa za kulevya hapa nchini una pesa nyingi zinazouwezesha
kufanya jambo lolote ili kufanikisha biashara hiyo. Kamishina Nzowa, ambaye alitakiwa na gazeti hili
kutoa taarifa ya uchunguzi kuhusiana na matukio
hayo ya dawa za kulevya, likiwemo lile la Watanzania
wawili waliokamatwa nchini Afrika Kusini wakiwa na
kiasi kikubwa cha dawa za kulevya pamoja na
uwezo wa kitengo chake wa kupambana na wauza dawa za kulevya, alisema kazi hiyo ina changamoto
kubwa katika kufanikiwa kwake, kwa sababu
inawahusisha watu wenye fedha nyingi hapa nchini.
Alisema, Watanzania wawili, Agnes Gerald (25) na
Melisa Edward (24), waliokamatwa na kilo 150 za
dawa za kulevya katika Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Oliver Tambo nchini Afrika Kusini, Julai
5, mwaka huu, walifanikiwa kupita JNIA bila
kugundulika kutokana na watu waliokuwa kwenye mashine za ukaguzi wa abiria na mizigo.
“Hawa Watanzania waliopita kwenye Uwanja wa
Ndege wa Julius Nyerere na kukamatwa Afrika
Kusini, waliweza kupita kwa sababu inategemea na
watu waliokuwepo kwenye mashine za ukaguzi siku
hiyo. Unajua hakuna ushirikiano wa karibu baina ya
watendaji wanaohusika na udhibiti wa dawa za kulevya. Hilo ni tatizo kubwa linalosababisha
vikwazo katika kupambana na mtandao wa dawa
hizo.
“Sisi tunategemea kupata taarifa za wauza dawa za
kulevya kutoka kwa watu, wakiwemo wakaguzi wa
mizigo na abiria, hapo ndipo tunakwenda
kumpekua mtu anayeshukiwa kubeba dawa hizo.
Tunapopewa taarifa tunafanya ukaguzi, mbwa
tunawanusisha, lakini mara chache kwa sababu wakati mwingine wanashindwa kugundua mizigo
yenye dawa hizo iliyopuliziwa manukato au
kunyunyiziwa kahawa,” alisema Nzowa.
Kamishina Nzowa pia alilalamika kukithiri kwa
rushwa kwa watendaji ndani ya kikosi cha
kupambana na dawa za kulevya pamoja na jamii
kuwa ni jambo ambalo linasababisha kushamiri kwa
biashara hiyo. Mbinu mpya za kusifirisha dawa za kulevya
Duru za uchunguzi zimebaini kuwepo kwa mbinu
mpya inayotumiwa na wafanyabiashara wa dawa za kulevya kusafirisha mizigo yao tofauti na ile
iliyozoeleka. Wafanyabiashara , wanasiasa na watoto wa viongozi wa serikali wanaojihusisha na biashara hiyo
sasa wameligeukia kundi la wasanii wa filamu na
wanamuziki wa kizazi kipya wanaotajwa kuwa na
tamaa ya utajiri wa haraka haraka na kulifanya
wasafirishaji wakuu wa dawa hizo. Uchunguzi unaonyesha kuwa, wasanii hususan
vijana, ndio wanaotumiwa zaidi kubeba dawa za
kulevya huku wakihakikishiwa usalama wao na matajiri na wanasiasa wanaotajwa kuwa karibu na
baadhi ya viongozi wa serikali wanaowatumia kama
kinga yao, kwa makubaliano ya kugawana kipato
kinachotokana na biashara hiyo au kuwa katika
orodha ya malipo maalumu. Mbinu zinazotajwa kutumika kusafirisha dawa za
kulevya ni pamoja na mzigo baada ya kufungwa
hunyunyiziwa pilipili, manukato au kahawa ambazo
huondoa uwezo wa mbwa wenye mafunzo
maalumu ya kutambua dawa za kulevya kubaini. Imebainika kuwa dawa za kulevya zilizofungwa
vizuri na kunyunyiziwa unga wa pilipili au kahawa
juu yake huondoa uwezo wa mbwa kunusa harufu
kwa usahihi na badala yake humfanya apige chafya. Njia nyingine inayotajwa ni kufunga dawa za
kulevya ndani ya karatasi ya kaboni ambayo
mashine za ukaguzi zilizo katika uwanja wa ndege
hazina uwezo wa kubaini kilichofungwa ndani
pamoja na uvaaji wa nguo maalumu za ndani za
wanawake zinazofahamika zaidi kwa jina la ‘tight’ zilizoshonewa dawa za kulevya ndani ambazo
hazitambuliwi kirahisi na maofisa wa ukaguzi, bali
humuonyesha mwanamke akiwa amejazia. jamiiforums
إرسال تعليق