Mwakilishi wa Mjimkongwe, Ismail Jussa Ladhu (CUF)
********
Shutuma hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka jana, katika mkutano wake na waandishi wa habari baada ya kuibuka mjadala kuhusu afya ya Waziri Nyanga katika Baraza la Wawakilishi.
Shaka alisema UVCCM inatambua kuwa suala la kuumwa ni matokeo ya mipango ya Mungu na haikuwa muafaka kumshinikiza Rais amuondoe Waziri Nyanga wakati kuna viongozi wengine kama Nyanga wakiumwa na kulazimika kutibiwa nje ya nchi.
“Sote tunafahamu Waziri Nyanga anasumbuliwa na matatizo ya kiafya, bado anastahili kuhudumiwa na serikali, hakuna ulazima wa kumkebehi, kumkejeli au kumshinikiza Rais amuondoe katika wadhifa wake kutokana na afya yake kuzorota,” alisema Shaka.
Aidha, alisema inashangaza ushauri huo umeelekezwa kwa waziri Nyanga wakati kuna viongozi wengi wenye matatizo ya kiafya.
Alitoa mfano wa Makamo wa kwanza wa Rais, Seif Sharif Hamad ambaye amelazimika kuhama katika nyumba ya serikali iliyopo Bosnia kutokana na kushindwa kupanda ngazi tangu alipofanyiwa upasuaji wa magoti na serikali kulazimika kulipa mamilioni ya fedha kumkodia nyumba nje ya mji wa Zanzibar.
Pia liwataka wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar kutambua kuwa kiongozi yeyote mwenye matatizo serikali inastahili kumhudumia na hakuna sababu za kukebehi ugonjwa wa mtu au kushinikiza kujiuzulu wadhifa wake. “Si vyema kwa wawakilishi kulitumia jukwaa la Baraza lao kuwahukumu watu wasio na nafasi ya kuingia Barazani na kujitetea au kujibu mapigo, kazi ya kuhukumu ni ya mahakama na wao ni watunga sheria na wakosoaji wa serikali," alisema.
Akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Kilimo na Maliasili Mwakilishi wa Mjimkongwe, Ladhu alisema kwamba Waziri Nyanga kwa muda mrefu ameshindwa kutekekeza majukumu yake kutokana na matatizo ya kiafya na kuomba Rais kufanya uteuzi ili kuziba nafasi yake.
CHANZO:
NIPASHE
Post a Comment