Dk Shein Cup : Kitamli ya Nungwi yailaza Mwendo mdundo ya Kidoti 1-0

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akimkabidhi zawadi Kipa Bora wa mashindano ya ujirani mwema ya Dr. Sheni Cup yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Nungwi.
 Balozi Seif akimkabidhi Kepteni wa Timu ya Soka ya Kitamli ya Nungwi Makame Mohd Haji jezi na vifaa baada ya timu hiyo kuibuka bingwa wa  Dr. Sheni Cup huko Nungwi Mkoa wa Kaskazini Unguja
 Balozi Seif akimkabidhi Kikombe Kepteni ya Mabanati wa Timu ya Pete ya Tusitengane ya Nungwi Ndamu Makame Mussa baada ya kuibuka na ushindi wa Kombe la Mwanamwema Sheni dhidi ya Timu ya Pete ya Tuko Imara.
 Kepteni wa Timu ya Soka ya Kitamli ya Nungwi Makame Mohd Haji akifuahia kikombe anachokabidhiwa na mgeni rasmi balozi Seif baada ya kutawadhwa kuwa mabingwa wa kombe hilo.
Kati kati yao ni lezi wa Jimbo la Nungwi Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa wa Idara Maalum Haji Omar Kheir.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif akizungumza na Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa Khamis hapo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar katyika kubadilishana mawazo ya namna ya kufufua michezo ya ndani inayoonekana mingi kufifia.
Mwenyekiti wa Taifa wa Baraza la Michezo Zanzibar { BTMZ } Sharifa Khamis akipokea mchango wa shilingi Milioni 2,000,000/- kutoka kwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa ajili ya kusaidia ufufuaji wa michezo ya ndani inayoonekana kufifia hapa Nchini.
Picha na Hassan Issa wa – OPMR – ZNZ.
 
NA Othman Khamis Ame, OMPR
 
Hatimae Mabingwa wa Mashindano ya Ujirani mwema ya Dr. Sheni Cup yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM Jimbo la Nungwi na kufadhiliwa na Rais wa Zanzibar Dr. Ali  Mohammed Sheni amepatikana katika mchezo wa Fainali ya mashindano hayo yaliyozikutanisha Timu za Soka za Kitamli ya Nungwi  dhidi ya wapinzani wao Timu ya Soka ya Mwendo Mdundo ya Kidoti.
 
Pambano hilo la Fainali lililoshuhudiwa na umati mkubwa wa wapenzi wa soka wa Jimbo la Nungwi na Vitongoji vyake limeiwezesha Wenyeji wa mashindano hayo Timu ya Kitamli ya Nungwi kuibuka na ushindi kwa kuilaza Mwendo Mdundo ya Kidoti Goli 1-0.
 
Timu ya Kitamli ilijipatia goli lake la pekee na la ushindi lililofungwa na mchezaji Haji Wa Haji katika kipindi cha kwanza cha mchezo huo  ambapo mgeni rasmi katika pambano hilo la Fainali ya Dr. Sheni Cup alikuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
 
Mashindano hayo ya ujirani mwema  yaliyoanza kutimua vumbi Tarehe 24/8/2013 yamejumuisha Timu  Tisa kutoka katika vijiji tofauti vya Jimbo la Nungwi yakienda sambamba na yale ya mchezo wa Pete { Net Ball } kwa Wanawake yaliyojumuisha Timu Nne.

Akizungumza mara baada ya pambano hilo la Fainali Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif aliwahimiza Vijana hao kujitahidi kujifunza zaidi michezo ili wajijengee njia rahisi ya kupata ajira kupitia sekta ya michezo ambayo wakati huu imekuwa na thamani kubwa Duniani.
 
Balozi Seif alisema Ulimwengu hivi sasa umeshuhudia ongezeko kubwa la ajira kupitia Sekta ya michezo hasa Mchezo wa soka na Table Tennis ambayo imeonekana kutajirisha wanamichezo wengi wenye vipaji vikubwa vya michezo hiyo.
 
“ Tumeshuhudia wachezaji mbali mbali Duniani wakiwemo pia wale wanaotokea Bara letu la Afrika wakicheza mpira wa kulipwa katika timu mbali mbali za bara la Ulaya hasa ndani ya Uingereza. Huo ni Mfano halisi mmaopaswa kuutilia maanani ili na nyinyi siku moja mjikute mmetinga katika vilabu hivyo maarufu Duniani “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Mapema Mlezi wa Jimbo la Numngwi ambae pia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Idara Maalum Haji Omar Kheir alisema mashindano hayo yaliyoandaliwa na Umoja wa Vijana wa CCM wa Jimbo hilo kwa  ushauri wa Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi ni utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2010.
 
Haji Omar alisema ilani hiyo imeeleza umuhimu wa uimarisha michezo katika maeneo mbali mbali nchini   lengo likiwa  kuwajengea afya njema pamoja na ajira wananchi wanaoshiriki michezo hiyo.
 
Katika kuunga mkono uendelevu wa mashindano hayo Waziri Haji Omar aliahidi kuchukuwa dhamana ya malipo kwa deni linalodaiwa Kamati ya mashindano hayo linalohusu malipo ya posho za waamuzi pamoja na baadhi ya vifaa vya mashindano hayo.
 
Katika fainali hiyo  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi Kikombe kwa Mabingwa wa Mashindano hayo Timu ya Kitamli ya Nungwi, Jezi, Mpira pamoja na Shilingi laki 300,000/-.
 
Balozi Seif pia alimkabidhi mshindi wa pili Mwendo Mdundo ya Kidoti Jezi, Mpira na Shilingi Laki 150,000/- wakati mshindi wa Tatu Timu ya Mapinduzi ya Kidagoni ikakabidhiwa  Jezi, Mpira na Shilingi 75,000/-.
 
Baadae Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar akakabidhi shilingi 50,000/- kwa kila Timu bora , Mchezaji bora, mfungaji bora, Muamuzi bora, Mchezaji mdogo kuliko wote,kipa bora  pamoja na kocha bora kwenye mashindano hayo.
 
 Mashindano hayo yaliyopewa jina la Dr. Sheni Cup kwa mchezo wa Soka na Mwanamwema Sheni Cup kwa mchezo wa Pete { Net Ball } yamegharimu jumla ya shilingi milioni Sita Nukta Tano { 6,500,000/- }.
 
Wakati huo huo Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alikabidhi mchango wa shilingi Milioni 2,000,000/- kwa ajili ya kusaidia ufufuaji wa michezo ya ndani { Indo games } hapa Nchini ambayo mingi inaonekana kufifia na mengije kufa kabisa kwa  kipindi kirefu sasa.
 
Akikabidhi mchango huo kwa Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar  { BTMZ } Sharifa Khamis hapo Ofisini kwake vuga Mjini Zanzibar Balozi Seif alisema Zanzibar ilikuwa ikisifika kimataifa kwa michezo ya ndani sifa ambayo hivi sasa imekufa kutokana na kufifia kwa michezo hiyo.
 
Alisema juhudi za pamoja zinahitajika kuchukuliwa katika kuona michezo hiyo inachipuka tena hapa Nchini kwa kuwapa nguvu za uwezeshaji na vifaa wachezaji wanaojihusisha na  michezo hiyo.
 
“ Vijana lazima waendeleze pia michezo ya ndani kama vile Table Tennis, Vinyoya, Beach Ball, Triatholon na riadha badala ya kuelekezaa  nguvu zao zaidi kwenye soka ili kurejesha sifa hiyo Kimataifa “. Alisisitiza Balozi Seif.
 
Akipokea mchango huo Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar             { BTMZ } Sharifa Khamis { Sherry } alisema msaada huo wa Balozi Seif ni hatua ya awali katika kuunga mkono juhudi zinazochukuliwa na Taasisi za Michezo Nchini katika kufufua vuguvugu la michezo hapa Nchini.
 
Mwenyekiti Sharifa { Sherry } alisema katika kwenda samba mba na ufufuaji huo Baraza la Taifa la Michezo Zanzibar kwa kushirikiana na Chama cha Soka Zanzibar        { ZFA } hivi karibuni  vinatarajiwa kufungua vuguvugu la michezo katika kutimia miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964

Post a Comment

أحدث أقدم