DK. SHEIN: POLISI LAZIMA IJITADI UCHUNGUZI DHIDI YA VITENDO VYA WATU KUMWAGIWA TINDIKALI

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

STATE HOUSE ZANZIBAROFFICE OF THE PRESS SECRETARYPRESS RELEASE


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitahidi kuimarisha uchunguzi wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali ili wahusika wapelekwe kwenye vyombo vya sheria.

Dk. Shein ametoa wito huo leo huko hospitali la Mnazi Mmoja mjini Unguja alipokwenda kumjulia hali Padri Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Machui Unguja, ambae amelazwa katika hospitali hiyo kufuatia kumwagiwa tindikali jana jioni.

“hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee... ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake” alisisitiza Dk. Shein.

Amekieleza kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Dk. Shein amesema amesikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padri Mwang’amba na kumuomba Mwenzi Mungu ampe nafuu haraka apone ili endelee kuitumikia jamii.

Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya Wodi alipolazwa Padri huyo Dk. Shein aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati Serikali ikichukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.

“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu wenzako katika hali kama hii ya majonzi. Hakuna anayeyataka haya. Tuwe wastahamilivu Serikali tunachukua hatua”aliwaambia waumini hao.

Akizungumzia hali yake, Padri Mwang’mba alimueleza Rais kuwa hali yake ni nzuri na anaona vizuri lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua sehemu za machoni.

“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake hakuathirika sana.

Amefafanua kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Mlandege jioni wakati akitoka katika ofisi moja inayotoa huduma za intaneti/mtandao katika eneo hilo ndipo akatokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.

Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk. Jamala Adam Taibu amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo Padri Mwang’amba alipatiwa huduma zote muhimu za matibabu zinazostahiki.

Kuhusu majeraha aliyopata Dk. Jidawi alieleza kuwa kwa ujumla asilimia 30 ya mwili wa Padri Mwang’amba umeathirika na kidogo sehemu za macho.

Chanzo - ZanziNews 

Post a Comment

أحدث أقدم